Enzi za utotoni wengi wetu kufurahi ilikuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku.
Lakini umri ulivyozidi kusogea, furaha ndio kimekuwa kitu adimu kukutana nacho, yawezekana ni kutokana na mabadiliko ya maisha.
Kuna vitu vingi katika maisha yetu vinavyotupunguzia furaha siku hadi siku.
Nadhani kila mtu katika dunia hii angependa kuwa na furaha ya kudumu, lakini kuna vitu katika maisha yetu ambavyo vinachangia kuondoa furaha.
Pindi unapojikuta uko ndani ya vitu hivyo furaha inapotea, mpaka utakapo rekebisha ndio utaipata tena.
Hebu tujaribu kuviangalia kwa ufupi kimoja baada ya kingine.
1.KUJARIBU KUMFURAHISHA KILA MTU:
Mtego huu wengi unatunasa, kwa kuogopa kusemwa vibaya na wengine.
Tunapenda kujiingiza kufanya vitu tusivyopenda ili tu kumfurahisha kila mtu, pasipokujua tunajiumiza wenyewe.
Kumbuka hata ufanye mazuri mangapi, lakini hautaweza kumfurahisha kila mtu.
Ni heri uelekeze nguvu zako kwa watu wanaothamini unachofanya kuliko wasiothamini.
2.KUJAWA NA TAMAA:
Sawa tunahitaji pesa kuishi maisha mazuri, lakini kuwa mtumwa wa pesa ni kujikosesha furaha mwenyewe.
Ridhika kutafuta riziki yako kwa uwezo wako uliojaaliwa.
3.KUJAWA NA WIVU:
Mara nyingi ni vigumu kuwa na furaha halisi pale unapoona mtu unayemdharau amefanikiwa zaidi yako.
Na hii inasababishwa na kujilinganisha kwetu na wao pasipokuangalia uwezo tumetofautiana.
Unapojilinganisha na mtu kuna mawili la wewe uje kujivunia kwa kufanikwa zaidi yake au uone wivu kwa kupitwa.
Ni heri ukaangalia maisha katika mtazamo wa kila mtu ana nafasi ya kufanikiwa, na ndipo utakapoona na wewe pia unaweza.
4.KUTOSAMEHE:
Kusamehe ni ufunguo muhimu katika kuleta furaha ya kweli maishani.
Unaposhindwa kusamehe unautwisha mzigo mzito moyo wako.
Unapojizoeza kubeba mizigo hii furaha ndio inazidi kukukimbia, kwani muda mwingi unatumia kuwaza namna ya kuadhibu aliyekukosea.
Pia sio tu kusamehe wengine bali pia na kujisamehe mwenyewe.
Yawezekana kuna makosa uliwahi kuyafanya na unapokumbuka yanakuumiza moyoni, unachopaswa kujua kuwa hakuna asiyekosa duniani, unachotakiwa ni kujisamehe na maisha yaendelee.
5.KUACHA KUFANYA UNACHOKIPENDA:
Katika maisha yetu binadamu kuna vitu huwa tunapovifanya, tunafanya kwa msisimko na furaha moyoni.
Yawezekana kikawa kimoja au zaidi ya kimoja ikitegemea uwezo uliojaaliwa kufanya hayo mambo.
Unapolazimisha kufanya usichopenda ni kuiondoa furaha maishani mwako. Siku hadi siku jizoeshe kufanya shughuli unazozipenda na furaha utaiona.
6.KULAZIMISHA FURSA:
Unatakiwa uwe mtu wa kutafuta fursa maishani mwako na si mlazimisha fursa.
Unaporukia kila kitu ili mradi kinavutia ni kujipotezea muda na hautaweza kujua eneo gani hasa ndio unaweza ukafanya vizuri zaidi.
7.KUWA MBINAFSI:
Hili ni jambo linalosumbua nakuondoa furaha pindi linapokuwa ni sehemu ya maisha yako.
Maisha ya kujifikiria wewe tu ni maisha yanayoumiza kwani hautaweza kuwa na furaha na watu wanaokuzunguka.
Unapodhani kwamba kwa kujitimizia mahitaji yako tu ndio furaha itakuja ni kujidanganya.
8.KUPUUZA DHAMIRA YAKO:
Mara kwa mara tunapotaka kufanya jambo lolote lazima kuna sauti au mazungumzo ya ndani yanayotuongoza katika kufanya maamuzi sahihi.
Na hii inatokana na tafsiri ya jambo lipi ni sahihi na lipi si sahihi ipo ndani ya anayetenda.
Kwahiyo unapofanya jambo kinyume na nadhiri yako inavyokuambia, ni kufungua milango ya kujilaumu au kulaumiwa na kujikosesha furaha maishani.
9.KUJAWA NA UVIVU:
Unaweza ukajua kabisa kwamba jambo fulani linapaswa kufanywa na wewe, na unapolikwepa unafungua milango ya kuwajibishwa na kukosa furaha moyoni mwako.
10.KUTOJIKUBALI:
Yawezekana kabisa kuna vitu hauvikubali kwako wewe mwenyewe, labda ungependa ungekuwa mrefu, mwembamba, mnene, mweupe, tajiri au hata historia yako ya maisha uliyopitia ingekuwa tofauti.
Vitu hivi unapoviwaza kila siku vinakuondolea furaha na kukufanya mnyonge.
Unachopaswa kufanya ni kujikubali na kusonga mbele kwa vyovyote vile ulivyo jua ndivyo ulivyopaswa kuwa.
JE, UMESHATAMBUA KIPI KATI YA VITU HIVYO HAPO JUU NDICHO KINACHOKUPOKA FURAHA YAKO?
NAFASI BADO UNAYO ANZA KUREKEBISHA SASA.
0 comments:
Post a Comment