“Usimamizi wa ubora, usalama, hadhi, mahusiano, ushirikiano, na sera ya ofisi ni mambo muhimu ya kumfanya mfanyakazi aridhike na mazingira yake ya kazi”

Mwisho wa kunukuu maneno ya msomi wa enzi hizo ndugu Fredrick Herzeberg, ambaye alikuja kumwagia zege nadharia iliyofanyiwa utafiti mwaka 1927 mpaka 1932 na Profesa Elton Mayo.


Profesa alifanya utafiti wa kuchunguza mazingira ya kazi na tija, pindi alipoona mfumo wa kuwaweka watu wengi wenye historia tofauti katika eneo moja la kazi.

 Alisisitiza kuwa mahusiano mazuri kazini huongeza tija ya kazi, kwani utendaji wa kila siku wa wafanyakazi unategemea sana mahusiano baina yao.

ONYESHA MTAZAMO CHANYA

Kuna kampeni ya usafi Dar es Salaam ina msemo usemao “Usijifanye mstaarabu bali kuwa mstaarabu”. Hata katika mtazamo pia unapaswa usijifanye una mtazamo chanya bali waoneshe wenzako kwa vitendo kuwa wewe una mtazamo chanya.

Mathalani mfanyakazi mwenzako amekumbana na tatizo katika utendaji wake na anaonyesha kuchanganyikiwa ila wewe ukawa mtuliza dhoruba kwa kuwa chanya na tatizo lake na kumpa njia mbadala za kutoka.

Nakwambia ukiwa hivi utakuwa unawavutia wenzako kuja kwako pindi wanapokumbana na changamoto.

 ONYESHA SURA YA FURAHA KILA UTAPOTOA SALAMU

Unawezaje kuingia ofisini macho chini, umeshusha mabega, bila hata ya kutoa salamu na unaenda moja kwa moja kuanza kazi?

Kama hii ndio tabia yako, utaendelea kuwaona wafanyakazi wenzako wakikuchunia au hata kukukwepa kila wakikuona.

Kuwa na tabia ya kutoa salamu kila unapokutana na wafanyakazi wenzako huku ukionyesha uso wa furaha, hii itawapa ishara wenzako kuwa unafuraha kuwa nao eneo moja la kazi.

        JIBU BARUA PEPE NA UJUMBE WA SIMU KWA WAKATI


  Utajisikiaje pale ambapo umemtumia mtu ujumbe uwe wa barua pepe au ujumbe wa kawaida wa simu na anachukua muda mrefu kukujibu au asijibu kabisa?

  Hii itaonyesha una dharau kwa wenzako, na kwamba wao hawana umuhimu kwako. Jenga tabia ya ukarimu wa kujibu ujumbe wa mtu kwa wakati, hii itakufanya uonekane unajali na itawapa urahisi wao kukushirikisha taarifa muhimu kwa wakati.

        KUBALI UTANI ENEO LA KAZI

Simaanishi ukubali kila utani utakaotaniwa hata ule unaovuka mipaka, bali ule utani ambao ni wa kawaida usiovuka mipaka upalilie ili uwafanye wenzako wafurahie uwepo wako kwani dhumuni kubwa la utani ni kufurahi pamoja.

Usishangae mtu huna hata mazoea nae ila akaanza kukutania, hii ina maanisha anataka kupata picha wewe ni mtu wa namna gani. Hasa ukizingatia kuwa ishazoeleka kuwa mtu wa utani ni rahisi kuingilika kwa maongezi na si mtu wa kukasirika hovyo.

       TENGENEZA UAMINIFU

Unapokutana na wengine eneo la kazi hakuna anayejua kuwa wewe ni muaminifu mpaka utakapofanya tendo la uaminifu mbele yao. Hata siku moja mtu asikwambie kuwa yeye si mwizi kama eneo au mazingira anayoishi hakuna cha kuiba. 

Vivyo hivyo huwezi kuwaambia watu wewe ni muaminifu na mkweli kama haujawahi kuonyesha mbele yao tukio la uaminifu na ukweli.

Mathalani endapo umekosea jambo Fulani na ukakubali na kukiri mbele ya wenzako, hii itawajengea picha kuwa wewe ni muaminifu na msema kweli.

        KUWA MTU WA KUTOA MSAADA KWA WENZAKO

Kutoa msaada wa maarifa na utaalamu katika eneo la nje ya muongozo wako wa kazi ni msaada tosha kwa mfanayakazi mwenzako mwenye kuhitaji msaada wako.

Kwa mfano wewe unafahamu kutengeneza kitu Fulani ambacho mfanyakazi mwenzako unamuona kimemuharibikia na anashindwa kukitengeneza, ukijitokeza kumsaidia utakuwa umeimarisha uhusiano wako na yeye na atakuona ni mtu mzuri kuishi nae eneo moja la kazi.

        HESHIMU TOFAUTI ZA UTAMADUNI KATI YAKO NA WENZAKO

Mazingira ya kazi katika zama hizi yameendelea kuwaleta pamoja watu wenye historia tofauti, kuanzia malezi mpaka jamii wanazotokea.

Jinsi wewe unavyokuwa unatumia muda wako na kiwango cha umakini lazima kitatofautiana na wenzako.

Usiwe mtu wa kujilinganisha na kuwaona wenzako ni watu wa ajabu kwakuwa hawapo kama wewe, bali fungua masikio na macho yako kujifunza kitu kutoka kwao ambacho wewe huwezi kukifanya kama wao.

Unapokuwa mtu wa kuheshimu tofauti zako na za wengine, utawafanya na wao watamani kujifunza kitu kutoka kwako, hivyo kuimarisha mahusiano yenu eneo la kazi.

 KUWA NA HESHIMA KWA WOTE

Kama unadhani heshima ni kuamkia wakubwa tu hasa wale unaofanya nao kazi, basi nakuomba utafakari upya. Heshima ni nguzo muhimu sana katika kujenga mahusiano bora eneo la kazi. 

Kumheshimu mwenzako ni pamoja na kujua mipaka ya kauli na maneno ya kuongea mbele yake hata kama umemzidi cheo au umri.

Ukiwa na heshima kwa wengine itakusaidia usiwe miongoni mwa watu wanaopenda kujadili watu wengine kwa mabaya. Ukiwaonyesha heshima watavutika kuja kwako na mahusiano yenu yataimarika.

        SHIRIKIANA NA WENZAKO KATIKA VITU WANAVYOPENDA

Muulize mfanyakazi mwenzako kuhusu vitu anavyopenda kufanya, aina ya muziki anaosikiliza, filamu amazoangalia, na hata vitabu anavyosoma. 

Baada ya kufahamu angalia chochote ambacho mnaendana shirikiana nae, kwa mfano umegundua anapenda sana kuangalia mpira sio mbaya kama ukijiunga nae kama na wewe ni muangaliaji pia.

             SHIRIKI MITOKO NA WENZAKO

Kufahamiana na wafanyakazi wenzako nje ya eneo la kazi ni jambo zuri sana. Ndio maana ofisi nyingi lazima utakuwa kila baada ya muda Fulani wanaandaa tafrija ya kuwakutanisha wafanyakazi katika bonanza ili kujenga mahusiano mazuri baina yao.

Hata kama ofisi haiandai matukio kama hayo ila sio mbaya kama utakuwa unatumia muda wako japo kidogo kutoka na kwenda mahali na wenzako kupata vinywaji au chakula nje ya muda wa kazi ili kuboresha mahusiano mazuri.







Je, unajua waajiri wakati mwingine hulipa kiwango kikubwa Cha mshahara kwa kuwa mwajiriwa ana elimu sahihi na uzoefu? Je, unaweza kuwa na uwezo wa kupata mshahara mkubwa kwa kufanya kazi moja katika kampuni kubwa? Ni dhahiri, hivi vinaweza kuwa baadhi ya  vitu vya nguvu katika mazungumzo wakati wa mapitio ya utendaji wako, usaili  wa kazi, au ombi kwa ajili ya kupandishwa cheo.

Waajiri kawaida hurekebisha taarifa za malipo wakati wa kuamua kiasi gani cha kumlipa mfanyakazi wa kufanya kazi maalumu. Baada ya wao kuamua thamani ya nafasi kwa kutafiti taarifa juu ya viwango vya malipo kwa ajili ya kazi hiyo kulinganishwa katika makampuni mengine yanayofanya shughuli sawa na wao, ila watakubali kubadilisha kwa kuzingatia elimu na uzoefu wa mwombaji.

Miaka ya uzoefu

Kwa kawaida, ukiwa na uzoefu zaidi huchangia kulipwa kiwango cha juu cha mshahara. Vile vile, kama nafasi imetangazwa na anahitajika mtu mwenye uzoefu wa miaka 10 katika kazi fulani, na wewe huna wala haukidhi mahitaji hayo, ukibahatika ukapata hiyo kazi tambua lazima utalipwa kiwango kidogo.

Elimu

Uwiano kati ya elimu yako na kiwango kinachohitajika kwa ajili ya kazi kwa kawaida huathiri mshahara utakaolipwa. Pia, ubora wa elimu unaweza kuathiri mshahara. Kupata shahada kutoka katika kozi inayoheshimika, kawaida ina ushawishi chanya juu ya kulipwa kwako, wakati kupata shahada kutoka katika chuo ambacho huchukuliwa dhaifu hupunguza uwezo wako wa kupata mshahara mkubwa.

Utendaji  wa kitaalamu

Tangu kitambo waajiri wengi hutumia msingi wa maamuzi yao kulipa mshahara angalau kwa kiwango cha juu kwa kuzingatia utendaji wa mtu binafsi, hiki ndio kipimo cha kutofautisha  viwango vya mshahara wakati wa kutaka kuongeza mshahara au cheo. Hata wakati unapoomba kazi mpya, habari hii inaweza kuwa muhimu kwa mwajiri wako, kwani inatoa picha kamili juu ya uwezo wako.

Mkuu wako wa kazi

Mchango wako na uhusiano wako wa kiutendaji katika mafanikio ya kampuni yako, endapo mkuu wako wa kitengo cha kazi ana nafasi kubwa katika maamuzi ya kampuni, mapendekezo yake kuhusiana na malipo yako yana nafasi kidogo ya kupingwa wakati wa mapitio.
Idadi ya wanaoripoti kwako

Jinsi unavyokuwa na idadi ya wafanyakazi wengi wa kuwasimamia na kuleta ripoti kwako, ndivyo utakavyoweza kulipwa kiwango cha juu katika kazi fulani. Bila shaka, ngazi yako ya mafanikio inategemea msingi wa utendaji wa wafanyakazi ambao unawasimamia.

Kutunukiwa na vyama vya Kitaalamu

Vyeti na uanachama katika bodi za kitaalamu au vyama vya biashara unaweza kuwa chagizo chanya kuathiri juu ya kulipwa kwako kwa kiwango cha juu. Hata hivyo, kama kazi uliyopata na hauna vyeti vinavyohitajika, kulipwa kwako lazima kuanzie kiwango kidogo. Baadhi ya waajiri wanahimiza wafanyakazi wao watafute vyeti vyenye vigezo.

Tofauti ya zamu

Katika kazi fulani, wafanyakazi wanaweza kutarajiwa kufanya kazi katika nyakati ambazo si muda ambao ni mzuri na unaopendwa na wengi. Wafanyakazi wa nyakati hizi ni kawaida kulipwa kiwango cha juu kutokana na gharama kubwa za kijamii na kimwili kushiriki katika kufanya kazi nje ya "masaa ya kawaida ya kazi." Katika kazi ambazo hakuna zamu za kuingia kazini, tofauti ya malipo ni kidogo.

“Hakuna binadamu mkamilifu”, huu msemo hatujaanza kuusikia leo, ila ni wachache kati yetu tunaoweza kuupa maana yake kamili pale ambapo kuna kosa limefanyika iwe na mtu mwengine au sisi wenyewe. Ukiwa unajua kuupa maana msemo huu hautakuwa mgumu kusamehe au kujisamehe na kutafuta njia mbadala za kutatua hilo tatizo kwa kuwa unatambua wazi binadamu hatuwezi kufanya jambo sahihi kila siku.
Wote ni mashahidi tulipokuwa tunaangalia mashindano ya Copa Amerika Lionel Messi katika hatua za awali alijituma sana kuifikisha nchi yake fainali na wote walimwona shujaa, lakini siku ya mwisho alikosa penati iliyowafanya kukosa kombe. 

Wote tunajua maamuzi aliyochukua baada ya mechi, alitangaza kujiuzulu kwani alikosa msamaha kwake mwenyewe kwakuwa alijihisi alipaswa kuwa mkamilifu kwa kuwa anajua watu wanamwona kama mtu asiyekosea. Kukosea tumeumbiwa wanadamu, na mara nyingi tunapogundua tumekosea katika eneo letu la kazi, tunajikuta tunaingia hatia mioyoni mwetu na hatujui tunaweza kumudu vipi hali hiyo. 

 KUBALI KOSA LAKO, NA MSHIRIKISHE MTU ANAYESTAHILI KUAMBIWA
Kama upo eneo la kazi na umefanya kosa, ni lazima kuna watu wataathirika na tukio lako. Jinsi unavyochukua muda mrefu kuelezea ulichokosea kwa litakaye mwathiri, ndivyo litakavyochukua muda mrefu kurekebisha makossa uliyofanya. Inaogofya kukubali kuchukua lawama za makosa uliyotenda, hasa ukizingatia unajua wazi kuna mtu atakukasirikia baada ya kusema ukweli, lakini nakwambia ni bora kulamba ncha ya kisu na kusema mapema kuliko kusubiri madhara yawe makubwa.

 Kama unajiona unaweza kurekebisha vitu wewe mwenyewe, bila kusimamiwa wala kuelekezwa na mtu, haitakuumiza kujaribu mwenyewe, ila ikitokea umekosea usiache kuomba msaada na si kujipa moyo kwamba utaweza kurekebisha kimya kimya. Watu wenye tabia ya kurekebisha makosa kimya kimya bila kumshirikisha mtu mwengine, hujitahidi kwa bidi zote ili kuficha aibu ya kuonekana wamekosea.
Ukweli ni kwamba kosa ulilofanya unaweza kuliona dogo, lakini kumbe jinsi unavyoliweka kimya huku hupati suluhisho la haraka linakuwa kubwa lisilorekebishika kuliko ulivyotarajia. 

Katika mahojiano na chuo cha biashara cha Harvard, mwenyekiti wa kampuni ya Toyota Katsuaki Watanabe alielezea kwanini ni vyema kuweka wazi tatizo: “Tatizo lililofichwa ndio huja kuwa janga kubwa. Kama tatizo likiwekwa wazi kila mtu akalitambua, najisikia salama. Hii ni kwasababu tatizo linapowekwa katika lugha ya picha, hata kama watu wetu hawakulitanbua tangu mapema, watazisumbua akili zao kutafuta suluhisho.


” Unapoenda kumwelezea mkuu wako wa kazi kilichotokea, ukweli ni sera bora kuliko zote. Achana na udhuru wa kutaka kuwaangushia wengine tatizo lako ili muathirike wote bali kubali kulibeba mwenyewe na ueleze ukweli wa kilichotokea. Kama kuna kazi ulipewa na ukasahau kuifanya kwa wakati, mweleze mkuu wako na kama una sababu ya maana ya kwanini haukufanya weka wazi. 


Kama ulipewa kazi na wakati unaifanya haikwenda sawa, usiogope kama ulijitahidi kutumia nguvu na akili yako kutimiza wajibu wako. Usiache tatizo kubwa liwe kubwa Zaidi kwa kujifanya hakuna kilichotokea. Hakikisha unaonyesha na hata kuwaomba msamaha wale wote walioathirika na makosa yako. Ulichokifanya sio kwamba umedhamilia kwajili ya kumuumiza mtu,bali unatakiwa kuchukua mzigo wote wa lawama na na kuomba radhi mwisho wa siku. 

  LETA SULUHISHO MBADALA LA KUTATUA TATIZO
Nadhani hautapenda uwe mtu anayeleta matatizo katika eneo lako la kazi pasipo kuleta suluhisho,haijalishi hilo tatizo limeletwa na wewe au mtu mwengine.Unapokuwa umekosea jambo Fulani na ukajitahidi uwe na na njia chache za suluhisho tayari kichwani hii itakusaidia kupunguza ukubwa wa nyundo zitakazokushukia.


Katika mazingira ya siku hizi ya kazi, kama unataka kuwa mfanyakazi mwenye kuthaminiwa, usliwe mleta matatizo kwa meneja wako bali leta suluhisho. Unajua kwanini? Kwasababu kuna matatizo mengi meneja anatakiwa kutatua wenyewe, sasa hutakiwi kuwa sehemu ya tatizo.
Njoo na njia lukuki za kutatua makosa yako, na chagua moja unalohisi ndio sahihi kabisa. Weka katika maandishi kabisa kama kuna ulazima na uwe na majibu tayari kwaajili ya maswali utakayoulizwa na meneja wako. 

Mpe muhtasari meneja wako wa hilo suluhisho lako sahihi lakini pia uwe na masuluhisho mengine karibu ikiwa meneja wako hajakubaliana na suluhisho lako la kwanza.Ndio yawezekana kabisa umezamisha meli lakini haimaanishi usionyeshe juhudi za kuiokoa mbele ya meneja wako. Unaweza kutafunwa kama bazooka, lakini utakuwa sehemu salama kwa kuwa umeonyesha juhudi za kuokoa jahazi baada ya kukosea. 

  JISAMEHE MWENYEWE NA JIFUNZE KUPITIA MAKOSA
Kuyakabili makosa yako ni jambo gumu, lakini ni muhimu kujisamehe mwenyewe punde tu unapokuwa umekosea.Umekosea kweli, lakini sio kitu cha ajabu kila binadamu huwa anakosea kwa nafasi yake. Ufanye msamaha kuwa sehemu ya maisha yako kila siku,na unapojikuta umefanya kosa kubwa, jitahidi kufikiria namna ya kutatua tatizo badala ya kukaa kujilaumu kila wakati.

Wewe sio mtu wa kwanza kufanya kosa kubwa kama hilo, jaribu kufuatilia watu ambao unao waangalia kama mfano kwako na uwadadisi na utagundua kumbe makossa ni sehemu ya binadamu katika kufikia mambo mazuri na kuwa yote waliyopitia ni sehemu ya mchakato. 
  TENGENEZA UAMINIFU TENA KWA MENEJA WAKO
Baada ya kufanya kosa kubwa na meneja wako akaligundua hutakiwi kufikiria kuacha kazi badala yake jitahidi uonyeshe kwamba haujarudishwa nyuma na kosa lile bali una nafasi ya kufanya tena jambo linguine kwa usahihi. 


Anza kujenga uaminifu tena kwa mambo madogo madogo na sio ushikwe na munkari utake kuonyesha umahiri katika mambo makubwa ambayo huna uzoefu nayo na yanaweza kukurudisha tena katika kukosea.

 
Copyright 2013-2017 Lisha Ubongo
| Branded by www.pixelbase.co.tz