Moja kati ya vitu vigumu maishani, ni kuishi kama unavyotaka wewe maisha yawe.
Mara kwa mara utajikuta unachanganywa na vitegemezi kama chakula, manunuzi, matukio ya televisheni, mitandao ya kijamii na hata simu za mkononi.
Vitegemezi hivi vinachangia kukuondoa katika uhalisia wako wa maisha na kukusahaulisha hisia za kweli na unajikuta unapoteza fursa zilizopo.
Unapokuwa mpweke ndio unapata muda wa kuzitafakari hisia zako halisi kwa kina:
uoga, hofu, furaha, hasira, au hata huzuni.
Haijalishi hisia zako ni hasi au chanya lakini zinakupa picha halisi ya unataka nini katika maisha.

Tuangalie kwa pamoja sababu zinazochangia 
mpaka unapoteza fursa zilizopo:

1.KUTAKA KUFANYA KILA KITU:

Karibu kila binadamu kuna kipindi anahisi anapitwa na vitu vinavyofanyika duniani, ambavyo anatamani pia angekuwa anavifanya.
Lakini hakika unaweza ukazunguka kila sehemu na kutaka kujihusisha na kila kitu, mathalani  kufanya kazi,au burudani masaa 24  bila kulala lakini bado hautaweza kujihusisha na kila kitu.
Kwahiyo achana na hisia za kwamba unapitwa na mambo na tambua kila unachotakiwa kufanya kipo katika mazingira yako.

2.KUKWEPA MAUMIVU NA KUSHINDWA:

Usijaribu kuukimbia ukweli wa maisha yanayokukabili, kwani maumivu na kushindwa ndio vitu vinavyosaidia ukuaji wako wa akili.
Kumbuka, kuna tofauti kati ya kuwa katika mazingira ya kushindwa na kuwa umeshindwa tayari .
Hautaweza kuvikimbia vitu hivi mpaka viwe vimekufundisha unachopaswa kukijua katika maisha yako, ili uchukue hatua nyingine mbele.

3.KUENDELEA KUSHIKILIA KUMBUKUMBU ZA ZAMANI:

Usijaribu kutumia muda wako mwingi kufikiria mambo mabaya ambayo yalishapita kwani kufanya hivyo ni kuyaruhusu yaharibu wakati uliopo.
Usijaribu kuishi wakati mwengine, unatakiwa ukubali kumaliza hizo kumbukumbu ili uanze kujenga mwanzo mpya.
Anza kufunga kumbukumbu za mambo mabaya ya zamani sasa na jua hayatakuongoza unapotaka kufika.

4.KUJIKUMBUSHIA MATUKIO YA KUSHINDWA:

Kama ukiendelea kujisimulia historia za matukio uliyoshindwa kichwani mwako, utayaamini na kujiona ni mtu wa kushindwa daima.
Swali ni: Historia unayojisimulia inakutia nguvu?
Usiendelee kuweka makosa yako kichwani, kwani uzito wake utaangusha uwezo wako halisi.
Unapaswa utambue kuwa kila kitu mwanzo huwa ni kigumu kabla hakijawa rahisi.

5.KUIGIZA MAISHA YA MWENGINE:

Vita kali zaidi uliyowahi kupigana nayo ni vita ya kutaka kuwa wewe, hivyo ulivyo sasa.
Hautawezi kuwa wewe kama kila siku unajitafuta kwa watu wengine.
Kumbuka, unapoigiza maisha ya mtu mwengine unapoteza nafasi ya kujitumia wewe mwenyewe na uwezo wako wa asili utakufa kwa kuwa hautumiki.

6.PICHA YAKO KICHWANI YA UNAVYOTAKA VITU VIWE:

Moja kati ya vitu vinavyokuangusha katika maisha ni picha unayoijenga kichwani 
na kutaka kila kitu kiwe kama ulivyokiona wewe mawazoni.
Maisha yanasonga na mara kwa mara sio kama ulivyotaka yawe, bali kadri yalivyopaswa yawe.
Maisha ni kama muziki unaochezwa ambao haukuuchagua, lakini unaweza ukachagua namna ya kuucheza.

7.KUJIONA UNA KASORO:

Usijihukumu mwenyewe, kuna watu wengi wanatamani kufanya hiyo kazi kwa ajili yako.
Fanya unayopaswa kufanya kwa uwezo wako na mengine yanayobaki yasalimishe kwa wengine.
Jipende na jionee fahari na kila kitu unachofanya hata kama umekosea kwani hata makosa yanaonyesha ulijaribu kufanya.

8.KUENDELEA KUSUBIRI:

Acha kuendelea kuisubiri kesho, kwani muda wa leo hautaupata tena.
Maisha ni mafupi sana kama kila siku unaomba udhuru.
Achana na mitazamo ya kutaka kufanya kila kitu kesho, anza leo kufanya hatua japo moja ya jambo lako kwa ujasiri.
Kama huna hakika ni njia gani hasa unayopaswa kupita, kufuata moyo wako ndio njia bora iliyobaki.

KAA TAFAKARI NI JAMBO LIPI KATI HAYO HAPO JUU LIMEKUWA TATIZO KWA WEWE KUFIKIA MALENGO YAKO.

ANZA KULISHUGHULIKIA SASA NA UTAONA MATUNDA YAKE.





Share this post:

Digg it StumbleUpon del.icio.us Google Yahoo! reddit

1 comments:

frank Victor

Karibuni kutoa maoni katika hili..

Post a Comment

 
Copyright 2013-2017 Lisha Ubongo
| Branded by www.pixelbase.co.tz