Wivu ni hali ambayo binadamu karibu wote tunaoishi katika hii sayari ya dunia tunaifahamu.

 Tunaifahamu kwa kuwa kama haipo ndani yetu kwenda kwa mtu mwengine, basi hata kutoka kwa mtu mwengine kuja kwetu.

Ni hali ya kuona anachofanya mwengine au alichopata hastaili kuwa nacho 
kwa kuwa wewe huna au unataka uwe nacho peke yako.
Na hali hii ukiiangalia kwa kina ndio inachangia sana kurudisha maendeleo ya jamii yetu kuanzia nyanja ya elimu, kazi au hata afya.

Yaani kuna watu wanataka hadi kunenepa wanenepe wao tu!!!
Na muda mwengine anayefanya chuki kwa mwenzake anakuwa hajui imetokana na nini, yeye ukimuuliza jibu lake linakuwa ni;
 "mi namchukia tu".

Sasa ili tusaidiane kuliondoa tatizo hili katika jamii yetu na kuhamasisha 
upendo na hivyo kuleta maendeleo kwa kila mmoja wetu.

Tuangalie hatua chache ambazo unaweza kuzifanya ili kuepuka chuki:

1.SHUGHULIKA NA MAMBO UNAYOYAWEZA:

Wekeza muda wako mwingi kufikiria kitu gani unaweza zaidi kufanya kuliko kupoteza muda katika vitu usivyoweza.
Kwani chuki huzaliwa katika kufikiria vitu hasi katika maisha.
Wewe ni mtu pekee unayeweza kujua kitu kipi unaweza zaidi na kipi huwezi.
Unapofikiria kosa ulilolifanya fikiria katika mtazamo wa kulisahihisha na kuboresha utendaji wako.

2.USIJILINGANISHE NA WENGINE:

Na hii ndio sababu kuu kabisa ya chuki kuzaliwa ndani yako, 
ikiwa utajilinganisha uwezo wako na mtu mwengine na nini anachomiliki.
Sisi wote duniani kila mtu ameumbwa na uwezo wake, na ukiligundua hili utaona kabisa kuchukia alichoweza mwenzako
 ni kupoteza muda.
Ukiangalia kwa undani hata wewe una vitu ambavyo huyo unayejilinganisha naye hana.
Kujilinganisha na 
mwengine ni kutaka kuwa yeye, na hiki kitu hakitawezekana kamwe 
labda upewe nafasi ya kujiumba upya mwenyewe.

3.JIKUMBUSHE MWENYEWE MATOKEO YA CHUKI:

Je, kuna jema lolote utakalolipata kwa kumchukia mtu mwengine?
Mara nyingi zinatufanya tujisikie maumivu ya kujiona waovu ndani yetu.
Japo kiuhalisia kuitawala chuki katika maisha yetu ni kitu kigumu lakini kwa kujitambua wewe kwanza hiki kitu kinawezekana.
Haujiangushi wewe tu unapomchukia mwengine bali pia unawaumiza unaowachukia
 kwani mara nyingine inabidi hata utumie nguvu ya ziada kuzuia jitihada zao.
Kaa na tafakari je ni kweli unataka kuwa mzizi wa uovu huu kwa wenzako?

4.UTAFAKARI MFUMO WAKO WA MAISHA:

Jaribu kuangalia kwa kina mwenendo wako wa maisha.
Yawezekana kabisa kuwa chanzo cha chuki yako kwa wenzako inatokana na hauli vizuri, hufanyi mazoezi, au unajishughulisha zaidi na vitu visivyokujenga.
Unapokuwa huna vitu nilivyoorodhesha hapo juu ni lazima kisaikolojia utaathirika.
Ukijishughulisha na vitu ambavyo unapenda kufanya ni hatua moja
 wapo ya kukufanya ujitambue wewe ni mzuri katika kufanya nini.

5.ITUMIE CHUKI KATIKA KUKUTIA HAMASA:

Kuliko kuiacha chuki ikutafune katika mambo mabaya, fikiria namna 
utakavyoitumia kukutia hamasa.
Ukiiacha ikupeleke katika vitu hasi itakufanya uchanganyikiwe.
Elekeza nguvu na muda unaotumia katika kuchukia wengine kufanikisha mambo ambayo yatakufaidisha maishani.
Itumie chuki katika mtazamo wa kukufanya uwe mtu mwema katika jamii kuliko ulivyo sasa.
Itumie katika mlengo wa kukuboresha.

KUMBUKA: KILA MMOJA WETU AMEUMBWA NA UWEZO TOFAUTI NA MWENZAKE, USIHUZUNIKE KUONA MWENZAKO AMEWEZA KITU  FULANI NA WEWE UMESHINDWA.

BALI TUMIA MUDA MWINGI KUJITAFAKARI WEWE MWENYEWE, USIITAFUTE TASWIRA YAKO NDANI YA WATU WENGINE.

TUANZE SASA KUIFANYA JAMII YETU KUWA SEHEMU SALAMA YA KILA MMOJA WETU KUONYESHA UWEZO WAKE.

Share this post:

Digg it StumbleUpon del.icio.us Google Yahoo! reddit

0 comments:

Post a Comment

 
Copyright 2013-2017 Lisha Ubongo
| Branded by www.pixelbase.co.tz