ULISHAWAHI KUFIKIRIA KUJIAJIRI MWENYEWE?
Hili ni swali ambalo litakuwa linakuja kwako kila utakapokuwa unalalamika kukosa kazi uliyoisomea.

Kila mmoja wetu amezaliwa na uwezo huu wa kujiajiri. 
Tumezaliwa na shauku, kiu, kufanya mambo ya hatari, uvumbuzi, akili na vitu vingine vingi ambavyo 
huonyesha wazi kuwa mtu hawezi kufundishwa ujasiliamali bali uko ndani yake kiasili, kinachohitajika ni yeye 
tu kujiweka katika mazingira ya 
kuruhusu akili yake kutatua tatizo lililojitokeza sehemu husika.

Hapa ninakuletea mfululizo wa vitu ambavyo unapaswa kufanya ili kuiamsha hamasa ya ujasiliamali ndani yako:

1.TENGENEZA MARAFIKI:

Yeyote anayetaka kuwa mjasiliamali ni lazima atengeneze marafiki wengi wenye mtazamo  chanya kama yeye.
Usiwe na marafiki ambao unatofautiana nao mtazamo, watakuwa wanakukatisha tamaa kwani kwao hilo wazo wanaona haliwezekani na watakwambia huwezi.
Kauli kama hizo zitakukatisha tamaa na ukizingatia wazo lolote mwanzo huwa gumu na haliwezekani mpaka uanze kulifanyia kazi.
Ndio ule msemo wa ukitembea na mwizi na wewe utakuwa mwizi unaingia hapa.

2.TENGENEZA LENGO:

Kutengeneza lengo la biashara ni hatua muhimu katika hatua za kuwa mjasiliamali.
Lengo hili uliweke katika maandishi na litakusaidia katika kuwashawishi watu kukusaidia mtaji.
Mara utakapokuwa umeandika lengo la biashara unayotaka kufanya usiweke maandishi hayo kabatini, 
anza kuyatafutia njia ya kuwa kitu halisi kutokana na hayo maandishi.
Na pia lengo hili litakusaidia wewe usiyumbe na kutoka katika mstari wa lengo ulilojiwekea na litakuwa ni muongozo wako.

3.JENGA NIDHAMU:

Unapotaka kuwa mjasiliamali ni lazima utengeneze nidhamu yako ya kazi.
Kabla hujaanza kuingia hatua ya kujiajiri ili uepuke hatari ya kupoteza kila kitu jiulize kama una nidhamu ya kutosha kuingia katika hiyo shughuli.
Huwezi ukawa mjasiliamali ambaye hauheshimu hata muda wako wa kazi.

4.TAMBUA JAMII INAHITAJI NINI:

Kama unataka kuwa mjasiliamali ni lazima uwe na uwezo wa kuchemsha akili yako katika kuyasoma mazingira uliyopo yanahitaji kitu gani na wewe uje na utatuzi wake.
Lenga eneo moja ambalo unaona kweli lina uhitaji na unaweza ukaja na utatuzi wake.

5.HOJIANA NA WAJASILIAMALI WALIOKUTANGULIA:

Kama unataka kuwa mjasiliamali utapata faida kubwa sana kuzungumza na watu ambao tayari wanafanya ujasiliamali.
Ukiwa na bahati kumpata mwenye moyo wa dhati wa ujasiliamali hatokuficha kitu ili kukusaidia ufikie ndoto yako.
Kwani kiasili mjasiliamali huwa anajitoa kuisadia jamii yake na hana haja ya kuwa mchoyo wa maarifa.

6.TENGENEZA WAZO RAHISI KUTEKELEZEKA:

Kama unataka kuwa mjasiliamali ni vyema ukawa umechagua eneo moja maalumu la kulitafutia ufumbuzi na ambalo 
rahisi kutekelezeka.
Na pia kuwa makini hilo jambo unalotaka kulifanyia kazi uwe na uzoefu nalo japo kidogo, 
kwani huwezi kutibu ugonjwa usijua hata unakaa wapi.

7.FANYA UTAFITI WA WAZO LAKO:

Ukiwa tayari umeshategeneza utatuzi juu ya jambo fulani jaribu kutafuta maoni kwa watu uliolenga kuwasaidia. 
Yawezekana usiwaeleze kwa kina kuhusu wazo ulilokuja nalo lakini tafuta namna ya kulijaribu na uone wanatoa maoni gani juu ya utatuzi huo kwa kupitia huduma za bure na mitandao ya kijamii.
Njia hii ndio itakusaidia kutambua kama wamependa njia yako ya utatuzi au la.

8.FANYA BIDII KULIKO WENGINE:

Hapa lazima utambue kuwa kila mtu anaweza kuwa mjasiliamali,
 lakini tofauti huja katika bidii wanayoweka katika shughuli waliyochagua.
Kama umejitolea kuwa mjasiliamali ni lazima ujitoe kufanya kazi kwa bidii kuliko mtu yeyote yule.

9.TAFUTA MSHAURI:

Ukitaka kuwa mjasiliamali ni vizuri ukawa na mtu anayekuongoza kwa mawazo kwani si kila wakati utakuwa unawazo sahihi.
Si kwamba yeye ndio awe anakutengenezea wazo bali anaweza akawa 
anapitia wazo lako na kukushauri kama uboreshe au kuna vitu uondoe.
Ikiwa utampata mshauri mzuri itakusaidia kupunguza hatari ya kuumia mapema.
Kuwa makini na mtu utakayemchagua, uwe unamuamini na awe hana ushindani na wewe.

10.HAKIKISHA UNAFURAHIA:

Hapa ni lazima ujue, kama unataka kuwa mjasiliamali mzuri na utakayefanikiwa ni lazima ufanye kitu unachokipenda.
Unapokuwa unafanya kitu unachokipenda unajitengenezea mazingira ya kuwa na furaha muda mwingi.

11.JIUNGE NA WAJASILIAMALI:

Ikiwa unataka kuwa mjasiliamali ni muhimu kutafuta eneo ambalo wajasiliamali wengi wanakutana kujadiliana.
Katika mazingira kama haya utakuwa kama yai linaloatamiwa na kuku ili lije kutoa kifaranga.
Wengi wao huwa wamepitia magumu kufika walipofika na hivyo wakiwa wanasimulia habari zao watakufanya ujiamini.

12.KUWA NA MAONO:

Kama unataka kuwa mjasiliamali ni lazima uandike maono yako ya unatarajia kuwa wapi katika shughuli unayotaka kufanya siku zinazokuja.

13.JITANGAZE:

Kama unataka kuwa mjasiliamali utakayefanikiwa ni lazima ujitangaze watu wakufahamu wewe ni nani na unafanya shughuli gani.
Siku zote mjasiliamali anauza jina na si kitu kingine.
Watu wanapokuamini unawafanya waamini kila kitu kinachokuja kwa jina lako.

14.HUDHURIA SEMINA NA MAKONGAMANO:

Wewe kama unataka kuwa mjasiliamali ni lazima utenge muda wako kuhudhuria semina mbali mbali, zinazohusiana na shughuli unazotaka kuja kufanya.
Unapohudhuria maeneo kama hayo itakusaidia kutengeneza mtandao na watu wengine na hata kukutana na watu wanaoweza kukusaidia kufika unapotaka.

15.FANYIA KAZI HATARI UNAYOIFAHAMU:

Sifa ya mjasiliamali wa kweli, ni yule asiyeingia kichwa kichwa kutaka kutatua tatizo pasipo kupiga hesabu za kutosha za hatari iliyopo.
Mjasiliamali, kweli huwa anachukua hatari za jamii na kujibebesha yeye lakini anapaswa achukue hatari ambayo hesabu zake anazifahamu.



KWA WALE WOTE WENYE MAWAZO YA KUTAKA KUJIAJIRI, HIZO NI BAADHI YA HATUA AMBAZO UNAWEZA KUZITUMIA KATIKA KUFIKIA NDOTO YAKO.

TUTAENDELEA NA MFULULIZO WA VIDOKEZO VYA NJIA ZA KUWA MJASILIAMALI VILIVYOBAKI, WEWE ENDELEA KUFUATILIA HAPA HAPA.









Share this post:

Digg it StumbleUpon del.icio.us Google Yahoo! reddit

0 comments:

Post a Comment

 
Copyright 2013-2017 Lisha Ubongo
| Branded by www.pixelbase.co.tz