Kama hujawahi gundua kuwa tabia yako inajengwa na matendo yako ya kila siku,
basi kuanzia leo tambua hilo.
Namna unavyowaza au kutenda kila siku ndio inaamua wewe kesho uwe wapi.
Ni vizuri uwe makini na nini unawaza, na kitu gani unakifanya 
mbele ya jamii yako.
Kuna tabia ambazo ni dhahiri kabisa tunapaswa kuziacha kwani zitatufanya
 baadaye tuwe katika mazingira ambayo hata sisi wenyewe hatutayapenda.

Hebu tujaribu kuona tabia ambazo tunapaswa kuziacha ili tuwe sehemu nzuri baadaye:

1.ACHA KUAHIRISHA MIPANGO YAKO:

Kuna watu wanapenda kuota mafanikio,
 lakini kuna wengine wanaamka kuyatafuta mafanikio.
Kuahirisha jambo mara kwa mara kunalifanya hilo jambo kuwa gumu na la kuogopwa.
Kumbuka, jambo lolote ambalo haujalianza leo, usitarajie kuwa kesho litakuwa limekamilika.

2.ACHA KULAUMU NA KUSINGIZIA WENGINE:

Ukikaa kuwalaumu watu wengine kuwa ndio chanzo cha wewe kukosa au 
kuwa katika mazingira fulani ni kukwepa majukumu yako.
Ukiwa mtu wa kila unapopatwa na jambo usilolipenda unatafuta mtu wa kumbwagia lawama hautasonga mbele daima.
Hii ni sawa na kutafuta visingizio vya kutaka kuonyesha kuwa wewe 
hauwezi kukosea, bali kuna wengine wanaosababisha wewe ukosee.

3.ACHA KUPINGA MABADILIKO:

Kama ikitokea siku moja kusitokee badiliko lolote duniani, basi jua wazi kwamba hakutakuwa na kesho yake.
Wengi wetu tunaridhika na hali ile ile tuliyonayo hata kama ulimwengu unabadilika kila siku.
Kila tunapopokea mabadiliko, maana yake tunakua na kuanza kuona
 fursa ambazo mwanzo hatukuweza kuziona kama zinawezekana.

4.ACHA KUTAKA KUTAWALA USIYOYAWEZA:

Ukiwa mtu wa kutaka kila kitu kiwe chini ya utawala wako,
 utakuwa mtu wa kujawa hofu na kuchanganyikiwa pale jambo linapokushinda.
Kiuhalisia haiwezekani binadamu akaweza kila kitu anachofanya.
Cha msingi kufanya ni kutambua kuwa kitu gani unaweza na 
kipi huwezi na kuikubali hiyo hali.

5.ACHA KUJIDHARAU:

Hakuna kitu kinachomshusha binadamu haraka chini,
 kama wewe mwenyewe ukijidharau.
Akili ni nzuri sana ikiwa utaitumia vizuri,
lakini huaribu haraka sana kama utaitumia vibaya.
Unapaswa kuwa makini unailisha kitu gani, je kitasaidia kukujenga au kitakubomoa?
Mara nyingi tunafanya mazungumzo na nafsi zetu  ndani kwa ndani, 
na tunachoamua baada ya hapo ni kutimiza tulilowaza kwa vitendo.
Anza kubadilisha leo aina ya maongezi unayofanya na akili yako.

6.ACHA KUKOSOA WENGINE:

Ukiwa mtu wa kutafuta makosa kwa wengine,
 ili uwalaumu utakuwa unajikosesha furaha wewe mwenyewe.
Tabia hii itakufanya usiwe unaona mazuri kwa watu wengine.
Yaani hata mtu awe amefanya vizuri vitu tisa kati ya kumi we unashughulika na kukosoa lile alilokosea tu.

7.ACHA KUKIMBIA MATATIZO YAKO:

Amini usiamini, ikiwa leo hii kila mtu aruhusiwe kuyarusha 
matatizo yake hewani, haitakuchukua sekunde mbili kuyachukua ya kwako 
na kuona kumbe wewe huna matatizo kabisa.
Unatakiwa ukae kuyakabili matatizo yanayokukuta, kwani ndio njia pekee ya kuyamaliza.
Ukiendelea kujijengea uoga ndani yako utakufanya uogope kufanya maamuzi sahihi.

8.ACHA KUISHI NA MAMBO YALIYOPITA:

Wengi wetu tunapoteza muda kuishi vipindi ambavyo hatunavyo tena.
Haitasaidia kitu kuendelea kushikilia  matukio yaliyopita katika maisha yako, 
hata kama ulifanikiwa kiasi 
gani kuyakumbushia haitabadilisha kitu chochote katika wakati uliopo.
Maisha ya kesho hayajengwi na tukio la kukumbushia bali tukio utalolifanya wakati ulionao sasa.

9.ACHA KUTAKA KUWA MTU MWENGINE:

Kuna changamoto kubwa sana ya sisi kuishi uhalisia wetu,
 katika dunia hii ya utandawazi,
 ambayo tumekuwa tunaonyeshwa zaidi maisha ya watu wengine kupitia teknolojia na kutamani kuwa kama wao.
Tunawaona watu ambao ni warembo, wanapendeza, wanaishi maisha mazuri kutuzidi.
Jambo la kujikumbusha ni kuwa pamoja na kutamani walivyo au vitu wanavyomiliki hatuwezi kuwa wao.
Hatuhitaji kuigiza kuwa kama fulani ili tupendwe na watu, 
bali tukiwa halisi tutapendwa na watu sahihi.

10.ACHA TABIA YA KUTOSHUKURU:

Sio kila jambo utakalolifanya kwa mara ya kwanza litakwenda kama unavyotaka,
kitu cha msingi ni kushukuru kwamba ulipata nafasi ya kulifanya.
Shukuru kwa mambo ambayo haujaweza kuyafanikisha, 
kwani yameacha nafasi kwa mambo ambayo utayafanikisha.
Hata uwe una magumu kiasi gani, kila siku usiache kushukuru katika maisha yako.



HIZO TULIZOZIONA NI BAADHI YA TABIA AMBAZO BILA SHAKA YOYOTE TUNAPASWA KUZIACHA IL TUWEZE KUISHI MAISHA TUNAYOTAMANI.

TUKIWEKA NIA YA DHATI TUNAWEZA KUJISAIDIA SISI WENYEWE NA WATU WANAOTUZUNGUKA.








Share this post:

Digg it StumbleUpon del.icio.us Google Yahoo! reddit

0 comments:

Post a Comment

 
Copyright 2013-2017 Lisha Ubongo
| Branded by www.pixelbase.co.tz