Mahusiano baina ya watu ni kitu cha asili na kisichopingika duniani.
Mahusiano hayo yanaweza kuundwa na ama ni undugu wa damu, urafiki wa kawaida, au ndoa baina ya mwanaume na mwanamke.
Si kitu kigeni kusikia mwanaume au mwanamke kusema kuwa yuko katika uhusiano na mwanamke au mwanaume mwengine.
Kipindi cha ujana mahusiano huwa hayapewi umakini unaostahili sana na wahusika,
 lakini unapokuwa mtu mzima,
 umakini unatakiwa kwasababu kuoa au kuolewa huwa si kitu cha kukimbiwa sana.
Wengi wetu tunachukulia mahusiano kama kitu cha kawaida sana,
 lakini kumbe kuna changamoto nyingi ambazo kama hautakuwa makini hakuna uhusiano utakaodumu nao katika maisha yako.

Hebu leo tuangalie vitu ambavyo ukivifanya katika uhusiano wowote uwe wa kindugu au ndoa utaufanya udumu:

1.USIFICHE UNAVYOJISIKIA:

Mahusiano mazuri huwa hayatokei tu kama miujiza, au kujitunza yenyewe.
Bali yanakuwa mazuri na kudumu kwa kuwa wahusika wanatoa hisia za jinsi wanavyojisikia moyoni na akilini bila kuwaficha wenzao.
Kama umefanyiwa kitu usichopenda halafu ukatabasamu tu,
unajitengenezea mazingira ya kutofurahia uhusiano wako, 
kwani utakuwa unajaza maumivu moyoni mwako.

2.MFANYIE MAZURI, AKUFANYIE MAZURI:

Mara nyingi katika mahusiano utatendewa vile vile unavyomtendea mwenzako.
Kama ukitaka kuonyeshwa upendo na mwenzako, anza wewe kumuonyesha upendo naye atarudisha vile vile unavyomfanyia,
 ukitaka awe rafiki kwako, anza wewe kuwa rafiki kwake,
ukitaka akuelewe, anza wewe kumuelewa yeye.

3.USIMLAZIMISHE ASICHOTAKA:

Kila binadamu huwa ana vipaumbele vyake, kwahiyo ukiona kitu fulani unatamani ufanyiwe na mtu wako wa karibu na hakufanyii, usilazimishe.
Kwani kama yeye anaona wewe unastahili kufanyiwa jambo fulani,
 lazima atalifanya kwa kuwa anaona unastahili.
Usilazimishe vipaumbele vyako viwe vipaumbele vya mtu wako wa karibu.

4.USIDHARAU MCHANGO WAKE:

Katika dunia hii kila utakaye kutana naye, lazima atakuja na 
kitu katika maisha yako.
Kuna wengine watakuja kukujaribu, kuna wengine watakuja kukutumia, kuna wengine watakuja kukufundisha kitu, na kuna wengine watakusaidia wewe kuwa mtu fulani.
Jifunze kutambua tofauti za michango ya watu hawa, 
kwani ukifikiria kwa kina hakuna mchango usio na manufaa kwako, 
hata kama ulikuletea maumivu, lakini kuna kitu ulitakiwa kujifunza.

5.KUBALI MABADILIKO YA MWENZAKO:

Hakuna binadamu ambaye kila siku za maisha yake atabaki kuwa hivyo hivyo alivyo.
Kinachotakiwa kuangaliwa kwa makini ni je,
 mabadiliko haya ni mazuri au mabaya?
Kuna muda unaweza ukamuona mtu wako wa karibu amebadilika, 
kwa kuwa tu amaecha kuwa kama vile wewe siku zote ulitaka awe.
Hutakiwi kumfanya ajisikie vibaya kwa kuwa tu amependa kuwa hivyo alivyo, 
huko ni kumfanya ajisikie vibaya kuwa karibu yako.

6.FURAHA YAKO UNAIAMUA WEWE:

Kama wewe ndani yako huna furaha usitegemee mwenzako ndio akufurahishe wewe.
Wengi tunawategemea watu wetu wa karibu ndio wawe watu wa kututengenezea furaha zetu,
na ni kitu kisichowezekana.
Kwani tafsiri ya jambo lipi linakufurahisha na lipi halikufurahishi liko katika akili yako.
Wewe unapotengeneza furaha ndani yako kwanza, ndio utaweza kumshirikisha na mwenzako na mtafurahi wote.

7.KUWA MTU WA MSAMAHA:

Endapo mtu wako wa karibu amevuka mipaka na kuingia eneo ambalo wewe 
ulipendi,
lazima utaona umekosewa.
Unapokaa na kosa ulilofanyiwa moyoni litakufanya ukose furaha kila unapomuona.
Unachotakiwa kutafakari ni kuwa je,
katika kosa nililofanyiwa kuna jambo lolote la mimi kujifunza?
Lichukue hilo halafu songa mbele na mambo ya msingi ya maisha yako.

8.USILAZIMISHE KUMBADILISHA MWENZAKO:

Hakuna binadamu mwenye uwezo wa kumbadilisha binadamu mwenzake,
 mpaka mtu mwenyewe atake pia kubadilika.
Kwahiyo ukiona umemshauri mwenzako kuwa abadili mwenendo wake fulani,
na akabadili ujue juhudi yote imetoke ndani yake, mpongeze.
Ila ukitaka kulazimisha awe vile vile unavyotaka wewe awe,
labda umbadilishe awe roboti ndio itawezekana.
Cha msingi wewe mueleze vitu usivyopenda,
 na muonyeshe ushirikiano katika kumsaidia kuacha.

9.USIPENDE KUGOMBANA SANA:

Ugomvi hausaidii kitu, na ni kupoteza muda tu, kwa kitu ambacho hakitakuwa na mshindi.
Muda mwingi utakao tumia kugombana na mtu wako wa karibu, ni vyema ukautumia kuimarisha upendo kati yako na yeye.
Ni vyema ukatulia na kutafakari kwa kina halafu ujadiliane na mwenzako ili kulimaliza.

10.IHESHIMU THAMANI YAKE:

Kila binadamu ana thamani yake,
 ambayo hakuna mwengine yeyote anayeweza akawa nayo zaidi yake.
Usiwe mtu wa kumfanya mwenzako kuwa mtumwa, kwako,
 na wewe ndio uwe wa kuamua thamani yake.
Unapokuwa mtu wa kumtoa kasoro mwenzako kila wakati,
unamfanya awe mtumwa wako kwani kwa kila atakalo fanya ili kujua kama ni jema ni lazima    wewe ndiye umwambie.


NI IMANI YANGU KWAMBA HAKUNA BINADAMU AMBAYE HANA UHUSIANO NA BINADAMU MWENZAKE.


IWE NI NDUGU WA DAMU AU RAFIKI WA KARIBU,
BADO TUNAHITAJIKA KUFANYA JUHUDI KUBWA KUFANYA MAHUSIANO HAYO YAENDELKEE KUWEPO.

KWA KUTUMIA NJIA CHACHE HAPO JUU TUTAWEZA KUFANYA MAHUSIANO YETU KUWA YA FURAHA SIKU ZOTE.























Share this post:

Digg it StumbleUpon del.icio.us Google Yahoo! reddit

0 comments:

Post a Comment

 
Copyright 2013-2017 Lisha Ubongo
| Branded by www.pixelbase.co.tz