“Usimamizi wa ubora, usalama, hadhi, mahusiano, ushirikiano, na sera ya ofisi ni mambo muhimu ya kumfanya mfanyakazi aridhike na mazingira yake ya kazi”

Mwisho wa kunukuu maneno ya msomi wa enzi hizo ndugu Fredrick Herzeberg, ambaye alikuja kumwagia zege nadharia iliyofanyiwa utafiti mwaka 1927 mpaka 1932 na Profesa Elton Mayo.


Profesa alifanya utafiti wa kuchunguza mazingira ya kazi na tija, pindi alipoona mfumo wa kuwaweka watu wengi wenye historia tofauti katika eneo moja la kazi.

 Alisisitiza kuwa mahusiano mazuri kazini huongeza tija ya kazi, kwani utendaji wa kila siku wa wafanyakazi unategemea sana mahusiano baina yao.

ONYESHA MTAZAMO CHANYA

Kuna kampeni ya usafi Dar es Salaam ina msemo usemao “Usijifanye mstaarabu bali kuwa mstaarabu”. Hata katika mtazamo pia unapaswa usijifanye una mtazamo chanya bali waoneshe wenzako kwa vitendo kuwa wewe una mtazamo chanya.

Mathalani mfanyakazi mwenzako amekumbana na tatizo katika utendaji wake na anaonyesha kuchanganyikiwa ila wewe ukawa mtuliza dhoruba kwa kuwa chanya na tatizo lake na kumpa njia mbadala za kutoka.

Nakwambia ukiwa hivi utakuwa unawavutia wenzako kuja kwako pindi wanapokumbana na changamoto.

 ONYESHA SURA YA FURAHA KILA UTAPOTOA SALAMU

Unawezaje kuingia ofisini macho chini, umeshusha mabega, bila hata ya kutoa salamu na unaenda moja kwa moja kuanza kazi?

Kama hii ndio tabia yako, utaendelea kuwaona wafanyakazi wenzako wakikuchunia au hata kukukwepa kila wakikuona.

Kuwa na tabia ya kutoa salamu kila unapokutana na wafanyakazi wenzako huku ukionyesha uso wa furaha, hii itawapa ishara wenzako kuwa unafuraha kuwa nao eneo moja la kazi.

        JIBU BARUA PEPE NA UJUMBE WA SIMU KWA WAKATI


  Utajisikiaje pale ambapo umemtumia mtu ujumbe uwe wa barua pepe au ujumbe wa kawaida wa simu na anachukua muda mrefu kukujibu au asijibu kabisa?

  Hii itaonyesha una dharau kwa wenzako, na kwamba wao hawana umuhimu kwako. Jenga tabia ya ukarimu wa kujibu ujumbe wa mtu kwa wakati, hii itakufanya uonekane unajali na itawapa urahisi wao kukushirikisha taarifa muhimu kwa wakati.

        KUBALI UTANI ENEO LA KAZI

Simaanishi ukubali kila utani utakaotaniwa hata ule unaovuka mipaka, bali ule utani ambao ni wa kawaida usiovuka mipaka upalilie ili uwafanye wenzako wafurahie uwepo wako kwani dhumuni kubwa la utani ni kufurahi pamoja.

Usishangae mtu huna hata mazoea nae ila akaanza kukutania, hii ina maanisha anataka kupata picha wewe ni mtu wa namna gani. Hasa ukizingatia kuwa ishazoeleka kuwa mtu wa utani ni rahisi kuingilika kwa maongezi na si mtu wa kukasirika hovyo.

       TENGENEZA UAMINIFU

Unapokutana na wengine eneo la kazi hakuna anayejua kuwa wewe ni muaminifu mpaka utakapofanya tendo la uaminifu mbele yao. Hata siku moja mtu asikwambie kuwa yeye si mwizi kama eneo au mazingira anayoishi hakuna cha kuiba. 

Vivyo hivyo huwezi kuwaambia watu wewe ni muaminifu na mkweli kama haujawahi kuonyesha mbele yao tukio la uaminifu na ukweli.

Mathalani endapo umekosea jambo Fulani na ukakubali na kukiri mbele ya wenzako, hii itawajengea picha kuwa wewe ni muaminifu na msema kweli.

        KUWA MTU WA KUTOA MSAADA KWA WENZAKO

Kutoa msaada wa maarifa na utaalamu katika eneo la nje ya muongozo wako wa kazi ni msaada tosha kwa mfanayakazi mwenzako mwenye kuhitaji msaada wako.

Kwa mfano wewe unafahamu kutengeneza kitu Fulani ambacho mfanyakazi mwenzako unamuona kimemuharibikia na anashindwa kukitengeneza, ukijitokeza kumsaidia utakuwa umeimarisha uhusiano wako na yeye na atakuona ni mtu mzuri kuishi nae eneo moja la kazi.

        HESHIMU TOFAUTI ZA UTAMADUNI KATI YAKO NA WENZAKO

Mazingira ya kazi katika zama hizi yameendelea kuwaleta pamoja watu wenye historia tofauti, kuanzia malezi mpaka jamii wanazotokea.

Jinsi wewe unavyokuwa unatumia muda wako na kiwango cha umakini lazima kitatofautiana na wenzako.

Usiwe mtu wa kujilinganisha na kuwaona wenzako ni watu wa ajabu kwakuwa hawapo kama wewe, bali fungua masikio na macho yako kujifunza kitu kutoka kwao ambacho wewe huwezi kukifanya kama wao.

Unapokuwa mtu wa kuheshimu tofauti zako na za wengine, utawafanya na wao watamani kujifunza kitu kutoka kwako, hivyo kuimarisha mahusiano yenu eneo la kazi.

 KUWA NA HESHIMA KWA WOTE

Kama unadhani heshima ni kuamkia wakubwa tu hasa wale unaofanya nao kazi, basi nakuomba utafakari upya. Heshima ni nguzo muhimu sana katika kujenga mahusiano bora eneo la kazi. 

Kumheshimu mwenzako ni pamoja na kujua mipaka ya kauli na maneno ya kuongea mbele yake hata kama umemzidi cheo au umri.

Ukiwa na heshima kwa wengine itakusaidia usiwe miongoni mwa watu wanaopenda kujadili watu wengine kwa mabaya. Ukiwaonyesha heshima watavutika kuja kwako na mahusiano yenu yataimarika.

        SHIRIKIANA NA WENZAKO KATIKA VITU WANAVYOPENDA

Muulize mfanyakazi mwenzako kuhusu vitu anavyopenda kufanya, aina ya muziki anaosikiliza, filamu amazoangalia, na hata vitabu anavyosoma. 

Baada ya kufahamu angalia chochote ambacho mnaendana shirikiana nae, kwa mfano umegundua anapenda sana kuangalia mpira sio mbaya kama ukijiunga nae kama na wewe ni muangaliaji pia.

             SHIRIKI MITOKO NA WENZAKO

Kufahamiana na wafanyakazi wenzako nje ya eneo la kazi ni jambo zuri sana. Ndio maana ofisi nyingi lazima utakuwa kila baada ya muda Fulani wanaandaa tafrija ya kuwakutanisha wafanyakazi katika bonanza ili kujenga mahusiano mazuri baina yao.

Hata kama ofisi haiandai matukio kama hayo ila sio mbaya kama utakuwa unatumia muda wako japo kidogo kutoka na kwenda mahali na wenzako kupata vinywaji au chakula nje ya muda wa kazi ili kuboresha mahusiano mazuri.







Je, unajua waajiri wakati mwingine hulipa kiwango kikubwa Cha mshahara kwa kuwa mwajiriwa ana elimu sahihi na uzoefu? Je, unaweza kuwa na uwezo wa kupata mshahara mkubwa kwa kufanya kazi moja katika kampuni kubwa? Ni dhahiri, hivi vinaweza kuwa baadhi ya  vitu vya nguvu katika mazungumzo wakati wa mapitio ya utendaji wako, usaili  wa kazi, au ombi kwa ajili ya kupandishwa cheo.

Waajiri kawaida hurekebisha taarifa za malipo wakati wa kuamua kiasi gani cha kumlipa mfanyakazi wa kufanya kazi maalumu. Baada ya wao kuamua thamani ya nafasi kwa kutafiti taarifa juu ya viwango vya malipo kwa ajili ya kazi hiyo kulinganishwa katika makampuni mengine yanayofanya shughuli sawa na wao, ila watakubali kubadilisha kwa kuzingatia elimu na uzoefu wa mwombaji.

Miaka ya uzoefu

Kwa kawaida, ukiwa na uzoefu zaidi huchangia kulipwa kiwango cha juu cha mshahara. Vile vile, kama nafasi imetangazwa na anahitajika mtu mwenye uzoefu wa miaka 10 katika kazi fulani, na wewe huna wala haukidhi mahitaji hayo, ukibahatika ukapata hiyo kazi tambua lazima utalipwa kiwango kidogo.

Elimu

Uwiano kati ya elimu yako na kiwango kinachohitajika kwa ajili ya kazi kwa kawaida huathiri mshahara utakaolipwa. Pia, ubora wa elimu unaweza kuathiri mshahara. Kupata shahada kutoka katika kozi inayoheshimika, kawaida ina ushawishi chanya juu ya kulipwa kwako, wakati kupata shahada kutoka katika chuo ambacho huchukuliwa dhaifu hupunguza uwezo wako wa kupata mshahara mkubwa.

Utendaji  wa kitaalamu

Tangu kitambo waajiri wengi hutumia msingi wa maamuzi yao kulipa mshahara angalau kwa kiwango cha juu kwa kuzingatia utendaji wa mtu binafsi, hiki ndio kipimo cha kutofautisha  viwango vya mshahara wakati wa kutaka kuongeza mshahara au cheo. Hata wakati unapoomba kazi mpya, habari hii inaweza kuwa muhimu kwa mwajiri wako, kwani inatoa picha kamili juu ya uwezo wako.

Mkuu wako wa kazi

Mchango wako na uhusiano wako wa kiutendaji katika mafanikio ya kampuni yako, endapo mkuu wako wa kitengo cha kazi ana nafasi kubwa katika maamuzi ya kampuni, mapendekezo yake kuhusiana na malipo yako yana nafasi kidogo ya kupingwa wakati wa mapitio.
Idadi ya wanaoripoti kwako

Jinsi unavyokuwa na idadi ya wafanyakazi wengi wa kuwasimamia na kuleta ripoti kwako, ndivyo utakavyoweza kulipwa kiwango cha juu katika kazi fulani. Bila shaka, ngazi yako ya mafanikio inategemea msingi wa utendaji wa wafanyakazi ambao unawasimamia.

Kutunukiwa na vyama vya Kitaalamu

Vyeti na uanachama katika bodi za kitaalamu au vyama vya biashara unaweza kuwa chagizo chanya kuathiri juu ya kulipwa kwako kwa kiwango cha juu. Hata hivyo, kama kazi uliyopata na hauna vyeti vinavyohitajika, kulipwa kwako lazima kuanzie kiwango kidogo. Baadhi ya waajiri wanahimiza wafanyakazi wao watafute vyeti vyenye vigezo.

Tofauti ya zamu

Katika kazi fulani, wafanyakazi wanaweza kutarajiwa kufanya kazi katika nyakati ambazo si muda ambao ni mzuri na unaopendwa na wengi. Wafanyakazi wa nyakati hizi ni kawaida kulipwa kiwango cha juu kutokana na gharama kubwa za kijamii na kimwili kushiriki katika kufanya kazi nje ya "masaa ya kawaida ya kazi." Katika kazi ambazo hakuna zamu za kuingia kazini, tofauti ya malipo ni kidogo.

“Hakuna binadamu mkamilifu”, huu msemo hatujaanza kuusikia leo, ila ni wachache kati yetu tunaoweza kuupa maana yake kamili pale ambapo kuna kosa limefanyika iwe na mtu mwengine au sisi wenyewe. Ukiwa unajua kuupa maana msemo huu hautakuwa mgumu kusamehe au kujisamehe na kutafuta njia mbadala za kutatua hilo tatizo kwa kuwa unatambua wazi binadamu hatuwezi kufanya jambo sahihi kila siku.
Wote ni mashahidi tulipokuwa tunaangalia mashindano ya Copa Amerika Lionel Messi katika hatua za awali alijituma sana kuifikisha nchi yake fainali na wote walimwona shujaa, lakini siku ya mwisho alikosa penati iliyowafanya kukosa kombe. 

Wote tunajua maamuzi aliyochukua baada ya mechi, alitangaza kujiuzulu kwani alikosa msamaha kwake mwenyewe kwakuwa alijihisi alipaswa kuwa mkamilifu kwa kuwa anajua watu wanamwona kama mtu asiyekosea. Kukosea tumeumbiwa wanadamu, na mara nyingi tunapogundua tumekosea katika eneo letu la kazi, tunajikuta tunaingia hatia mioyoni mwetu na hatujui tunaweza kumudu vipi hali hiyo. 

 KUBALI KOSA LAKO, NA MSHIRIKISHE MTU ANAYESTAHILI KUAMBIWA
Kama upo eneo la kazi na umefanya kosa, ni lazima kuna watu wataathirika na tukio lako. Jinsi unavyochukua muda mrefu kuelezea ulichokosea kwa litakaye mwathiri, ndivyo litakavyochukua muda mrefu kurekebisha makossa uliyofanya. Inaogofya kukubali kuchukua lawama za makosa uliyotenda, hasa ukizingatia unajua wazi kuna mtu atakukasirikia baada ya kusema ukweli, lakini nakwambia ni bora kulamba ncha ya kisu na kusema mapema kuliko kusubiri madhara yawe makubwa.

 Kama unajiona unaweza kurekebisha vitu wewe mwenyewe, bila kusimamiwa wala kuelekezwa na mtu, haitakuumiza kujaribu mwenyewe, ila ikitokea umekosea usiache kuomba msaada na si kujipa moyo kwamba utaweza kurekebisha kimya kimya. Watu wenye tabia ya kurekebisha makosa kimya kimya bila kumshirikisha mtu mwengine, hujitahidi kwa bidi zote ili kuficha aibu ya kuonekana wamekosea.
Ukweli ni kwamba kosa ulilofanya unaweza kuliona dogo, lakini kumbe jinsi unavyoliweka kimya huku hupati suluhisho la haraka linakuwa kubwa lisilorekebishika kuliko ulivyotarajia. 

Katika mahojiano na chuo cha biashara cha Harvard, mwenyekiti wa kampuni ya Toyota Katsuaki Watanabe alielezea kwanini ni vyema kuweka wazi tatizo: “Tatizo lililofichwa ndio huja kuwa janga kubwa. Kama tatizo likiwekwa wazi kila mtu akalitambua, najisikia salama. Hii ni kwasababu tatizo linapowekwa katika lugha ya picha, hata kama watu wetu hawakulitanbua tangu mapema, watazisumbua akili zao kutafuta suluhisho.


” Unapoenda kumwelezea mkuu wako wa kazi kilichotokea, ukweli ni sera bora kuliko zote. Achana na udhuru wa kutaka kuwaangushia wengine tatizo lako ili muathirike wote bali kubali kulibeba mwenyewe na ueleze ukweli wa kilichotokea. Kama kuna kazi ulipewa na ukasahau kuifanya kwa wakati, mweleze mkuu wako na kama una sababu ya maana ya kwanini haukufanya weka wazi. 


Kama ulipewa kazi na wakati unaifanya haikwenda sawa, usiogope kama ulijitahidi kutumia nguvu na akili yako kutimiza wajibu wako. Usiache tatizo kubwa liwe kubwa Zaidi kwa kujifanya hakuna kilichotokea. Hakikisha unaonyesha na hata kuwaomba msamaha wale wote walioathirika na makosa yako. Ulichokifanya sio kwamba umedhamilia kwajili ya kumuumiza mtu,bali unatakiwa kuchukua mzigo wote wa lawama na na kuomba radhi mwisho wa siku. 

  LETA SULUHISHO MBADALA LA KUTATUA TATIZO
Nadhani hautapenda uwe mtu anayeleta matatizo katika eneo lako la kazi pasipo kuleta suluhisho,haijalishi hilo tatizo limeletwa na wewe au mtu mwengine.Unapokuwa umekosea jambo Fulani na ukajitahidi uwe na na njia chache za suluhisho tayari kichwani hii itakusaidia kupunguza ukubwa wa nyundo zitakazokushukia.


Katika mazingira ya siku hizi ya kazi, kama unataka kuwa mfanyakazi mwenye kuthaminiwa, usliwe mleta matatizo kwa meneja wako bali leta suluhisho. Unajua kwanini? Kwasababu kuna matatizo mengi meneja anatakiwa kutatua wenyewe, sasa hutakiwi kuwa sehemu ya tatizo.
Njoo na njia lukuki za kutatua makosa yako, na chagua moja unalohisi ndio sahihi kabisa. Weka katika maandishi kabisa kama kuna ulazima na uwe na majibu tayari kwaajili ya maswali utakayoulizwa na meneja wako. 

Mpe muhtasari meneja wako wa hilo suluhisho lako sahihi lakini pia uwe na masuluhisho mengine karibu ikiwa meneja wako hajakubaliana na suluhisho lako la kwanza.Ndio yawezekana kabisa umezamisha meli lakini haimaanishi usionyeshe juhudi za kuiokoa mbele ya meneja wako. Unaweza kutafunwa kama bazooka, lakini utakuwa sehemu salama kwa kuwa umeonyesha juhudi za kuokoa jahazi baada ya kukosea. 

  JISAMEHE MWENYEWE NA JIFUNZE KUPITIA MAKOSA
Kuyakabili makosa yako ni jambo gumu, lakini ni muhimu kujisamehe mwenyewe punde tu unapokuwa umekosea.Umekosea kweli, lakini sio kitu cha ajabu kila binadamu huwa anakosea kwa nafasi yake. Ufanye msamaha kuwa sehemu ya maisha yako kila siku,na unapojikuta umefanya kosa kubwa, jitahidi kufikiria namna ya kutatua tatizo badala ya kukaa kujilaumu kila wakati.

Wewe sio mtu wa kwanza kufanya kosa kubwa kama hilo, jaribu kufuatilia watu ambao unao waangalia kama mfano kwako na uwadadisi na utagundua kumbe makossa ni sehemu ya binadamu katika kufikia mambo mazuri na kuwa yote waliyopitia ni sehemu ya mchakato. 
  TENGENEZA UAMINIFU TENA KWA MENEJA WAKO
Baada ya kufanya kosa kubwa na meneja wako akaligundua hutakiwi kufikiria kuacha kazi badala yake jitahidi uonyeshe kwamba haujarudishwa nyuma na kosa lile bali una nafasi ya kufanya tena jambo linguine kwa usahihi. 


Anza kujenga uaminifu tena kwa mambo madogo madogo na sio ushikwe na munkari utake kuonyesha umahiri katika mambo makubwa ambayo huna uzoefu nayo na yanaweza kukurudisha tena katika kukosea.



Acha ukweli usemwe, furaha ya kweli si kutokuwa na matatizo, lakini ni uwezo wa kukabiliana nayo kwa ujasiri. Mara zote angalia kile ulicho nacho mkononi, badala ya kufikiria ulichopoteza. Sababu haijalishi dunia imechukua nini kutoka kwako, bali utafanya nini na kile ulichobaki nacho mkononi.



Yafuatayo ni mambo sita unayopaswa kujikumbusha kila unapopatwa na jambo gumu linalotaka kukukatisha tamaa ili usisonge mbele.  
    
      1.       MAUMIVU NI SEHEMU KATIKA UKUAJI



Kuna kipindi maisha yanafunga mlango sababu ni muda muafaka kusonga mbele. Na hiki ni kipindi kizuri sababu mara nyingi hatuwezi kusonga mbele wenyewe mpaka matukio Fulani yatokee kutusukuma ndo tunasonga.
Mambo yanapokuwa magumu jikumbushe kuwa hakuna maumivu yanayokuja bila dhumuni maalumu. Songa mbele baada ya maumivu lakini usisahau ulichojifunza kipindi cha maumivu.

Eti kwasababu una pata mahangaiko ndo imaanishe kuwa unafeli maisha. Kila jambo lolote kubwa la mafanikio huwa haliji kirahisi mpaka liambatane na mahangaiko ya hapa na pale. Mambo mazuri huchukua kipindi kirefu kukamilika. Kuwa mvumilivu na kuwa na mtazamo chanya. Kila kitu kitaenda kuwa sawa, labda sio kwa kasi unayoitaka wewe lakini mambo yatakuwa sawa tu.

Kumbuka kuna maumivu ya aina mbili, kuna yale yanayokuumuiza na yale yanayokubadilisha. Ukiwa unaenda na mtiririko wa jinsi maisha yanavyokwenda, badala ya kupingana na mabadiliko, itakusaidia kukua.

      2.       KILA KITU KIPO KWA MUDA TU



Kila wakati mvua inaponyesha, huwa kuna muda itaacha. Kila wakati wewe unapopata madhara, kuna wakati wa wewe kupona. Baada ya giza daima kuna mwanga - wewe hili unakumbushwa kila asubuhi, lakini bado mara nyingi unasahau, na badala yake unachagua kuamini kwamba usiku utadumu milele. Haitakuwa hivyo. Hakuna kinacho dumu milele.

Hivyo kama mambo ni nzuri sasa hivi, furahia. Sababu haitadumu milele. Kama mambo ni mabaya, msiwe na wasiwasi kwa sababu haitakuwa milele. Kwa sababu tu maisha si rahisi wakati huu, haina maana huwezi kucheka. Kwa sababu tu kitu  kinakusumbua wewe, haina maana huwezi tabasamu. Kila wakati unakupa mwanzo mpya na mwisho mpya. Unapata nafasi ya pili, kila wakati . Wewe unapaswa kuchukua nafasi na kuufanya kuwa ni wakati bora zaidi.

     3.       KUWA NA HOFU NA KULALAMIKA HAKUBADILISHI KITU


Wale ambao wanalalamika zaidi, kukamilisha mambo inakuwa ni ngumu. Ni vyema kujaribu kufanya jambo kubwa na kushindwa kuliko usijaribu kufanya chochote na utarajie kufanikiwa. Sio mwisho kama umefanya jambo na ukashindwa; na sio mwisho pia kama haujafanya jambo lolote lakini ukaishia kulalamika kuhusu hilo jambo.

Kama unaamini katika kitu, usiache kuendelea kujaribu. Usikubali vivuli vya zamani vikazima hatua zako za maisha yako ya baadaye. Ukiwa unaitumia leo kulalamika kuhusu jana hautaifanya kesho kuwa nzuri. 

Badala yake chukua hatua. Hebu tumia ulichoweza kujifunza kuboresha jinsi ya kuishi. Endelea kufanya mabadiliko na kamwe usiangalie nyuma.

Furaha ya kweli utaipata pale tu utakapoacha kulalamika kuhusu matatizo yanayokukuta bali unatakiwa uanze kushukuru kwa matatizo ambayo hauna.

      4.       MAKOVU YAKO NDIO NGUVU YAKO


Usije kuona aibu hata siku moja kutokana na makovu ambayo maisha  yamekupa. Kovu ina maana uliwahi kuumizwa na tatizo limekwisha na jeraha limefunga. Ina maana wewe alishinda maumivu, umejifunza somo, umekuwa na nguvu, na umesonga mbele. Kovu ni alama ya ushindi ya kujivunia. 

Usije kuruhusu makovu yako yakushikilie mateka. Usije kuyaruhusu yakufanye uishi maisha yako katika hofu. Huwezi kufanya makovu katika maisha yako kutoweka, lakini unaweza kubadilisha mtazamo wa jinsi unavyoyaangalia. Unaweza kuanza kuona makovu yako kama ishara ya nguvu na si maumivu.

      5.       KILA KIKWAZO KIMOJA NI HATUA YA KUKUA


Katika maisha, uvumilivu si kuhusu kusubiri tu; ni uwezo wa kushikilia tabia nzuri wakati wa kufanyia kazi kwa bidii ndoto yako, ukijua kwamba kazi unayofanya ni ya thamani. Hivyo kama unakwenda kujaribu, jitahidi kuweka muda wako wote huko.

Vinginevyo, hakuna faida kuanzisha jambo. Hii inaweza kuwa na maana ya kupoteza utulivu na faraja kwa wakati, na labda hata akili yako juu ya tukio. Na inaweza kumaanisha kukosa kula, au kukosa kulala, kama ulivyozoea, kwa siku kadhaa.

Na inaweza kuwa na maana kutoka eneo lako la faraja na ukaruruhusu kuumizwa na baridi kwa ajili ya jambo unalojaribu. Inaweza kumaanisha kutoa sadaka mahusiano na yote yale ambayo ni yako. Inaweza kuwa na maana ya kukubali kejeli kutoka kwa wenzako.

Kila kitu kingine ni mtihani wa dhamira yako ni kiasi gani cha wewe kweli unataka kutimiza jambo uliloanzisha.
Na kama unataka kutimiza jambo, itabidi kufanya, hata kama litaambatana na matukio ya  kushindwa na kukataliwa. Na kila hatua utakayopiga utajisikia vizuri kuliko kitu kingine chochote unaweza kufikiria. 

Utagundua kuwa mapambano hayapatikani katika njia, bali ni njia. Na ni thamani yake. Hivyo kama wewe unakwenda kujaribu,nenda njia yote. Hakuna hisia bora katika dunia ... hakuna  hisia bora kuliko kujua nini maana ya kuwa hai.

      6.       MITAZAMO HASI YA WENGINE SIO TATIZO LAKO


Kuwa na mtazamo chanya wakati mazingira yametawaliwa na mitazamo hasi. Tabasamu wakati wengine wanajaribu kukurudisha chini. Si jambo rahisi kudumisha shauku yako na kuzingatia unakoelekea. Wakati watu wengine wanakutenda vibaya, endelea kuwa wewe. Milele usiruhusu tabia chungu za mtu mwingine zilete mabadiliko kwako.

Zaidi ya yote, milele usikubali kubadilika ili kumvutia mtu ambaye anasema wewe hauna uwezo. Badilika sababu itakufanya mtu bora na itaenda kubadilisha kitu katika maisha ya mbeleni. Watu wataendelea kuzungumza bila kujali nini unafanya, hata iwe unafanya vizuri kiasi gani. Hivyo kuwa na wasiwasi kuhusu mwenyewe kabla ya kuwa na wasiwasi kuhusu nini wengine wana kufikiria. Kama unaamini kwa dhati katika kitu, wala hupaswi kuwa na hofu ya kupambana kwa ajili yake. Nguvu kubwa inatokana na kushinda kitu ambacho wengine walifikiria hakiwezekani.


Utani wote weka pembeni, maisha yako yanakuja mara moja tu. Huo ndio ukweli. Hivyo kufanya kitu kinachokupa furaha ndio kinapaswa kuwa kipaumbele chako.



Ukikutana na mtafuta ajira kilio chake kikubwa ni nimefanyiwa usaili mara nyingi ila baada ya hapo sijaitwa tena.

Waajiri huwa wanatumia vigezo gani katika kujaza nafasi za kazi katika ofisi zao? Kama unadhani una jibu moja litakalo wawakilisha waajiri wote kutokana na swali hilo, naomba nikwambie tafakari Zaidi.


Waajiri wote si sawa, anachokitafuta mwajiri mmoja kinaweza kuwa tofauti na mwajiri mwengine. Sababu inaweza kuwa ni kuwa mazingira ya kazi ya mwajiri mmoja yanatofautiana na mwajiri mwengine, kwahiyo watakapokuwa wanakusaili watakuwa wanaangalia vitu tofauti kutoka kwako.

Kila mwajiri anatafuta stadi za mwombaji zitakazoendana na kazi alizonazo katika ofisi yake ili kuboresha ufanisi wa kazi ili kutoa bidhaa au huduma nzuri kwa wakati na ubora unaotarajiwa na mteja. Lakini nje ya stadi kuna vitu ambavyo waajiri wengi wanafanana katika kuviangalia kutoka kwa mwombaji wa ajira.


Habari nzuri ni kuwa watafuta ajira wengi wanazo hizo sifa ila tu wanashindwa kuzionyesha wanapopata nafasi ya kuzionyesha. Na habari nzuri Zaidi ni kuwa kwa wale ambao hawana wanaweza kujijengea tabia hizi na zikawapa nafasi nzuri ya kuajiriwa kwa kupata mtu sahihi wa kuwaelimisha.

Na habari nzuri Zaidi ni kuwa utakapozijua hizi tabia utaweza kuboresha mfumo wako wa uombaji kwa kuelekeza moja kwa moja katika wasifu wako kile anachotafuta mwajiri katika kazi husika. BAdala ya kujaza masifa kibao katika wasifu wako utajua namna ya kuweka zile za muhimu.


   1. UWEZO WA KUWASILIANA



Uwezo wa kuwasiliana upo katika pande tatu moja ni uwezo wa kusikiliza, pili ni uwezo kuongea na tatu ni uwezo wa kuandika. Na kama unavyojua lugha yetu ya kiofisi ni kiingereza sasa ukiwa vizuri katika pande hizo tatu utajiweka katika nafasi nzuri katika soko la ajira. 

Unapokuwa na uwezo wa kupokea maelekezo kwa haraka na kuyahamishia katika maandishi na ukaweza kueleza matokea yake iwe kwa maandishi au mdomo ufanisi kazini utakuwa juu. 

Utajisikiaje unampa maelekezo mfanyakazi wako jinsi ya kufanya kazi Fulani na akashindwa kufanya kama ulivyomuelekeza kisa hamuelewani lugha?

  2.UWEZO WA KUTUMIA KOMPYUTA



Hapa tuelewane vizuri, kujua kompyuta haimaanishi lazima uwe umesomea kozi yake miaka kadhaa chuo labda kama kazi unayoomba inahusiana moja kwa moja na uweledi wa kompyuta kwa kusomea kozi husika. Ila kama unaomba kazi ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na masomo ya kompyuta, nataka nikwambie haimaanishi ndo usijue kitu kuhusu kompyuta. 

Dunia hii ya utandawazi kila kazi kwa namna moja ama nyingine ili kuikamilisha lazima kompyuta itaingia kati sasa kama hujui kuitumia kabisa utakuwa unajipunguzia soko. Mathalani uweze kutuma barua pepe (E-mail), programu ya maandishi (Microsoft word) na program ya namba na maandishi (Microsoft Excel)

  3.UWEZO WA KUBADILIKA/KUFANYA KAZI ZAIDI YA MOJA


Katika dunia hii ambayo ukuaji wa teknolojia na ushindani wa huduma na bidhaa umekuwa mkubwa ofisi nyingi hupunguza gharama kwa kuajiri watu wachache wenye uwezo wa kufanya kazi Zaidi ya moja ili gharama za kuzalisha ziwe ndogo na wao waweze kushusha bei kupunguza ushindani na kuliteka soko. 

Hivyo ukiwa na sifa ya uelewa wa kazi Zaidi ya moja utajiongezea nafasi katika soko la ajira.


  4.UWEZO WA KUCHANGANYIKA NA WENGINE



Katika mazingira ya ofisi ambayo binadamu Zaidi ya mmoja wanashirikiana kufanikisha lengo moja  la ofisi, uwezo wa mfanyakazi mmoja kuchangamana na mwengine bila tatizo ni jambo la muhimu sana. 

Ofisi inaweza kuruhusu mtofautiane kwa hoja ili kupata kitu kizuri lakini si kugombana sababu wazo la mmoja limepingwa na wengi na kuwanunia, hii italeta utengano na kushusha ufanisi mahali.

Ukiwa na uwezo wa kuchangamana na wengine mathalani katika wasifu wako ukaweza kuonyesha kwamba uliwahi kufanya kazi na watu Fulani na kufanikisha jambo Fulani.

  5.UWEZO WA KUONGOZA




Sehemu yoyote ambayo wanakutana watu Zaidi ya wawili lazima kuwe na kiongozi na lazima ujue miongoni mwenu lazima atoke kiongozi.

Waajiri wengi wanapenda mtu mwenye uwezo wa kuongoza sababu wenye tabia hii huwa na uwezo wa kufanya maamuzi ya kibunifu hivyo wanatarajia hata wakati wa utendaji wako utakuwa unafanya kwa ubunifu na kuwaongoza wengine  na si kufuata njia zile zile zilizopitiwa na wengine na hivyo kuongeza ufanisi kazini.

HAUJACHELEWA KUFANYA MAREKEBISHO PALE AMBAPO UNAONA UNA MAPUNGUFU ILI KUONGEZA UWEZO WAKO WA KUAJIRIKA KATIKA SOKO LA USHINDANI WA AJIRA.

HAKUNA ALIYEZALIWA NA SIFA ZOTE HIZO BALI WENGINE WAMEZITENGENEZA NA WAKAWEZA KUZIFANYA KUWA SEHEMU YA MAISHA YAO NA MATOKEO MAZURI WAKAYAPATA.

ANZA SASA KUPIGA HATUA...

 
Copyright 2013-2017 Lisha Ubongo
| Branded by www.pixelbase.co.tz