JE, UNADHANI HISIA ZAKO ZIMESHAKUA, UNAJUA SIFA ZA HISIA ZILIZOKUA? SOMA HAPA UJITAMBUE KAMA BADO UJIPANGE.
Vijana wengi,
wanapoona wamepata urefu,
mabadiliko ya mwili, kupanda kielimu,
na hata kazi
wanajiona tayari wameshakua.
Katika mazingira ya elimu kama chuo
au kazini,
vijana wengi wamekuwa kitaaluma na kiujuzi, lakini
kihisia bado wanakuwa ni wadogo lakini wanashindwa kulitambua hilo.
Jibu linaweza kuja kwa haraka kwamba,
hiki ni kizazi cha vijana wanaojua vitu vingi mapema kabla ya umri wao.
Kiuhalisia kijana anatakiwa apate muda wa kukomaa kihisia ili kukabiliana na
changamoto za ukubwani.
Vijana wengi siku hizi,
wanatumia taarifa ambazo hawawezi kuzikabili katika umri wao.
Ubongo unakuwa bado hauja komaa kwa shughuli hiyo yeye anakuwa tayari ameshaianza.
Akili yake,
inazichukua taarifa hizo na kuzihifadhi lakini hisia zake haziko tayari kuzitumia katika namna inayopaswa.
Jamii huwa inafurahi sana kumuona kijana anajitambua na
anaonyesha ishara za kukua kihisia,
kwa jinsi anavyokabiliana na changamoto kubwa,
katika namna inayostahili.
ZIFUATAZO NI ISHARA ZA KUKUA KIHISIA:
1.KUWA MVUMILIVU
Hii ni ishara inayomtofautisha mtu ambaye amekua na
yule ambaye hajakua kihisia.
Sifa moja ya watu ambao hawajakua kihisia ni kutosubiria muda muafaka wa kufanya mambo yake,
yawezekana watu wengine wakaumia lakini kwa kuwa yeye amefurahi,
ni sawa tu.
Aliyekuwa kihisia hata kama
hilo jambo ni la kumfurahisha,
atasubiri tu muda muafaka ufike.
2.HAYUMBISHWI NA KUKOSOLEWA
Aliyekuwa kihisia anaelewa kabisa kwamba,
kukosolewa ni
sehemu ya kujifunza.
Watu waliokua kihisia,
huwa wanapokea kukosolewa bila
kuruhusu ukosoaji huo uharibu mambo yake mengine.
Wanajielewa wanataka nini na wao ni nani.
3.WANAKUWA NA ROHO YA UNYENYEKEVU
Unyenyekevu huwa unaenda sambamba na ukuaji wa hisia.
Unyenyekevu si kuwafikiria wenzako tu
kwanza na wewe ukajitelekeza,
hapana.
Wanakuwa si watu wa kujipendelea wao
tu kwa kila kitu.
Ila ni watu wa kwanza
kutambua kuwa uwezo waliopewa na Mungu
ni kwa ajili ya viumbe na watu wanaoishi nao.
4.WANASIMAMIA MAAMUZI YAO
Wana misimamo inayotawala maamuzi yao,
wako tayari kufuata
misimamo yao na kupita njia ya maisha waliyochagua kwa
ujasiri bila kubabaika na wanakuwa tayari kuwajibika kutokana na
maamuzi yao.
Tabia zao ndio zinaongoza maamuzi yao ya kila siku.
5.WEPESI WA SHUKRANI
Iko wazi kabisa,
kuwa unavyozidi kukua ndio kuonyesha shukrani kwa watu na Mungu
si kitu cha kuficha katika mambo madogo
hadi makubwa
unayofanyiwa.
Mtu ambaye hajakua anaona yote yanayomtokea anayastahili kwahiyo
kushukuru hawezi.
6.ANATUMIA HEKIMA KABLA HAJAFANYA JAMBO
Mtu ambaye amekuwa anafundishika,
hajioni kuwa ana majibu
ya kila kitu.
Jinsi anavyozidi kujua vitu ndivyo anavyozidi kutafuta hekima.
Huwa hawaoni aibu kufuata ushauri kwa mwalimu, au mzazi
pale anapoona amekwama.
JARIBU KUJICHUNGUZA,
KAMA UMEKOSA SIFA HATA MOJA KATI YA HIZO HAPO JUU.
BASI UJUE BADO HUJAKUA KIHISIA
USI HARAKIE VITU AMBAVYO UNAONA KABISA MUDA WAKE BADO.
Kisukari,
ni ugonjwa unaotokea katika mfumo wa mmeng'enyo wa chakula,
ambapo kiwango cha sukari rahisi(glucose) kinazidi katika damu.
Kawaida, kiwango cha sukari katika damu kinarekebishwa na kemikali
inayoitwa insulini inayotolewa na
kongosho.
Hebu tazama video ya mfumo wa chakula ulivyo hapa:
Sasa inapotokea kemikali ya insulini kutoka katika kongosho,
utengenezaji wake ni duni au seli za mwili zinashindwa kuifanyia
kazi kemikali hiyo
kama inavyotakiwa,
na hivyo kuruhusu sukari kuongezeka katika damu.
Kuna dalili kadhaa zinazotokea pale sukari inapokuwa imezidi katika damu:
1.Kupatwa na haja ndogo mara nyingi;
2.kiu kali ya maji;
3.kuhisi njaa kali.
Aina za kisukari:
1.KUTOTENGENEZWA KWA INSULINI
Mwili unashindwa kutengeneza kemikali ya insulini,
kwahiyo mhusika huwa ana
hitaji la kujiwekea
kemikali hiyo mwilini.
Aina hii inaweza kumpata mtu kabla hajafikisha miaka 40,
sana sana ni kipindi cha ujana.
Asilimia 10 ya wagonjwa wa kisukari wanaugua aina hii ya kwanza.
Mgonjwa atatakiwa ajichome sindano ya kemikali ya insulini
katika maisha yake yote.
Na mara nyingi huwa
wanatembea na kifaa
maalumu cha kupimia kiwango cha sukari katika damu,
mara anapoona imezidi
anatakiwa ajichome
sindano ya insulini
ili kuipunguza katika kiwango maalumu.
2.KIWANGO KIDOGO CHA INSULINI
Katika
aina hii mwili unashindwa kutengeneza kemikali ya
insulini ya kutosha,
au mwili unashindwa kuitumia kemikali hiyo.
Asilimia 90
ya wagonjwa wa kisukari wanaugua aina hii ya pili.
Aina hii inaweza kuzuiwa kwa:
1.Kupunguza uzito;
2.Chakula kamili;
3.Mazoezi mengi;
4.Kufuatilia kiwango cha sukari katika damu.
Na ikiwa aina hii itashindwa kuzuiwa na mgonjwa,
itampeleka katika hatua
ya kujiwekea kemikali
ya insulini sana sana kwa njia ya kunywa vidonge.
Tazama video ya aina ya pili ya kisukari hapa:
3.KISUKARI WAKATI WA UJAUZITO
Inawapata sana wakina mama
wakati wakiwa
wajawazito,
na kuwafanya wawe na kiwango kikubwa sana cha sukari katika damu.
Inaweza kuzuiwa kwa
mazoezi na chakula kamili.
Inaposhindwa
kuzuiwa kwa mama mjamzito inamsababishia matatizo wakati wa kujifungua,
mwili wa mtoto unaweza kuwa mkubwa kuliko unavyopaswa kuwa.
Uchunguzi
unaonyesha kuwa wanawake wengi ambao lishe yao kabla hawajawa
wajawazito ilikuwa na
kiwango kikubwa cha mafuta ya wanyama na chenye kolesto wanakuwa katika
hatari ya kupata aina hii ya kisukari.
Vitu gani vinaweza kusababisha ugonjwa huu wa kisukari:
1.UZITO KUPITILIZA
Unapokuwa na uzito mkubwa,
unajiweka katika hatari
ya kupata ugonjwa
wa kisukari.
Uzito wa mwili kupitiliza unaufanya mwili kutengeneza kemikali
ambayo inaenda kuvuruga
mfumo wa mmeng'enyo
wa chakula.
2.KIWANGO KIDOGO CHA HOMONI ZA TESTOSTERONE
Ikiwa
mtu atakuwa na
kiwango kidogo cha utengenezwaji wa homoni hii kutoka katika korodani za mwanaume
na ovari za mwanamke,
basi
kiwango chake
katika damu kikishuka
kinamuweka mtu katika
hatari ya kupata aina
ya pili ya kisukari.
Ndio maana watu wenye umri mkubwa
hatari inakuwa kubwa
kwasababu,
kiwango cha utengezaji wa homoni hii unapungua kiasili,
na kuzuia insulini isifanya kazi yake sawa sawa.
Matatizo yanayoweza kutokea ikiwa utashindwa kuzuia ongezeko la sukari katika damu:
1.Matatizo ya Macho
Glaucoma-kuharibika
kwa mishipa kuona na
inaweza kutibiwa kwa
dawa ya matone ya macho.
Cataracts-ukungu katika macho unazuia kuona vizuri ambao unaweza
kuondolewa kwa oparesheni
maalumu ikiwa kuna ulazima.
2.Matatizo ya miguu
3.Matatizo ya ngozi
4.Matatizo ya moyo
5.Matatizo ya kusikia
6.Matatizo ya nguvu za kiume
7.Matatizo ya tumbo
8.Kiharusi
9.Michubuko kushindwa kupona haraka
10.Matatizo ya fizi za meno
Tazama video ya jumla hapa:
HUO NDIO UGONJWA WA KISUKARI KWA UFUPI.
JE, UNATAMANI KUWEKA ALAMA MWILINI(TATTOO)? UNAJUA INAFANYWAJE NA MADHARA GANI UNAWEZA KUYAPATA KWA KUWEKA HIYO ALAMA.
Siku hizi limekuwa ni jambo la kawaida,
kukutana na kijana au mtu mzima
mwenye alama fulani mwilini.
Anaonekana ana alama ya michoro mwilini maarufu kama tatuu.
Hapo mwanzo,
ilikuwa ni michoro maalumu kwa watu wa aina fulani,
mathalani wahuni, lakini siku hizi michoro hiyo mwili inawekwa na mtu yeyote hata wenye heshima zao.
Kwa siku za karibuni watu wengi wanatumia michoro hiyo
kuelezea hisia zao.
Kuwasilisha hisia zao kwa watu wengine,
kwa kuchora mchoro wa
aina fulani mwilini mwake.
Yawezekana hata wewe umetamani kuweka alama hii mwilini mwako,
lakini kabla hujafanya hivyo kuna vitu kwanza unapaswa kuvifahamu.
MCHORO WA MWILINI(TATTOO) NI NINI?
Ni alama inayotokea mwilini
baada ya ngozi kutobolewa
mpaka ndani,
halafu yale matobo yanajazwa wino maalumu ambao unaonyesha
alama ya mchoro.
Kuna alama nyingine zinafanywa kienyeji kwa kutumia
sindano ya kawaida,
na nyingine za siku
hizi zinatumia mashine maalumu ambayo inapotoboa ngozi inaingiza
wino moja kwa moja.
Na kitendo hiki kinafanyika bila
kutumia ganzi,
kwa hiyo tarajia maumivu
na damu kutoka.
Kinachoifanya alama hiyo kukaa muda mrefu,
ni kwa kuwa ngozi
imetobolewa mpaka ndani.
Ngozi zetu binadamu zina safu mbili za juu zinazofikiwa na sindano wakati wa kuweka alama:
Yakwanza,
yajuu ambayo ndio huwa ina tabia ya kukua na ndio maana ukiumia bado
inakuja kufunika lile eneo kwa kuotesha nyingine.
Ya pili,
ambayo ni ya ndani kabisa ambayo seli zake ni imara sana kwa hiyo,
inapotobolewa hii na kujazwa wino sio rahisi kufutika.
Mwanzo kabisa waweka hizi alama walikuwa wanatumia sindano kutoboa
ngozi halafu baadaye
wanaweka wino kwa juu
kwa mkono ili alama itokee.
JE, HUWA INAUMA?
Hakuna ubishi kwamba zoezi la kuweka alama mwilini linauma,
kwasababu ngozi yako inatobolewa mara kibao na sindano ya
mashine hiyo.
JE, UNAFIKIRIA KUWEKA?
Kama una wazo,
la kwenda kuweka alama hii mwilini mwako, unapaswa kujua
katika akili yako
kuwa lazima ufanye
katika mazingira salama.
Kwani unapaswa utambue kuwa unachoweka mwilini ni kidonda kilichojazwa wino,
usipokuwa makini kuitunza ndio utakuwa umefungua mlango kwa maradhi mwilini mwako.
Kama una matatizo ya moyo,
aleji, kisukari, matatizo ya ngozi,
matatizo ya kinga za
mwili au ukiwa mjamzito ni vyema ukakwepa kuweka alama hii.
MADHARA YAKE
*Matatizo ya aleji:
Wino unaoingia ndani ya ngozi yako uwe wa rangi nyekundu, kijani, njano au bluu unaweza ukakusababishia aleji ya ngozi.
Unaweza ukatokwa na vipere vinavyowasha katika eneo uliloweka alama yako.
Na hali hii inaweza kukutokea hata mwaka mmoja baada ya kuweka alama hiyo.
*Ugonjwa wa ngozi:
Uambukizo katika ngozi unaweza ukaleta wekundu katika ngozi yako, kuvimba kwa ngozi, au maumivu ya muda mrefu, yanaweza kukutokea ukiwa umeweka alama hii.
*Tetenasi:
Magonjwa ya kuambukiza kwa damu:
Ikiwa sindano iliyotumiwa na muweka hiyo alama ilikuwa ina chembe za damu
za mtu mwenye maambukizi au
haijasafishwa kwa muda
mrefu utakuwa katika
hatari ya kuambikizwa.
KWA WEWE UNAYETAMANI KUWEKA ALAMA HII MWILINI MWAKO,
UNAPASWA UWE MAKINI NA UAMUZI WAKO.
KWANI,
UKISHAIWEKA MWILINI GHARAMA YA KUIONDOA NI KUBWA SANA.
JE, UNAWEKA ILI IWEJE?
UNAPASWA KUJIULIZA HILI SWALI.
JE, UNATAKA KUSAFIRI NJE YA NCHI, UNAJUA MAHITAJI GANI YA ZIADA YANAHITAJIKA KUAMBATANISHWA WAKATI WA KUOMBA PASIPOTI AU HATI YA KUSAFIRIA? SOMA HAPA UJIELIMISHE.
Kipindi kilichopita tuliona aina za pasipoti zinazotolewa nchini Tanzania na baadhi ya taarifa unazotakiwa kuwa nazo ili uweze kuipata.
Leo tutaangalia hati zitazokusaidia pia upate pasipoti kwa urahisi endapo utaambatanisha katika maombi yako kutokana na aina ya safari unayotaka kufanya:
1.SAFARI BINAFSI
Maombi yako unatakiwa uambatanishe na:
*Ushahidi wa shughuli unayofanya;
*Barua ya mualiko;
*Tiketi ya kurudi;
*Barua ya ruhusa ya mzazi kama muombaji yuko chini ya miaka 18;
*Barua ya ruhusa kutoka kwa muajiri wako kama umeajiriwa;
*Barua kutoka kwa mjumbe wa eneo unalokaa muombaji.
2.SAFARI YA AJIRA
Unatakiwa uambatanishe na:
*Tangazo la kazi;
*Tiketi ya kurudi;
*Barua kutoka kwa mjumbe wa eneo unaloishi.
3.SAFARI YA KIMASOMO
Maombi yako yaambatane na:
*Barua ya kuchaguliwa na shule/chuo;
*Vyeti vyako vya masomo;
*Barua ya udhamini;
*Ushahidi wa malipo kama unajilipia binafsi;
*Barua ya ruhusa kutoka kwa muajiri wako kama umeajiriwa;
*Barua ya ruhusa kutoka kwa mzazi kama una umri chini ya miaka 18.
4.SAFARI YA KIDINI
Maombi yako yanatakiwa yaambatane na:
*Barua ya mualiko;
*Barua kutoka katika taasisi ya dini iliyoandaa safari.
5.SAFARI YA KIMATIBABU
Maombi yako yaambatane na:
*Barua kutoka kwa mganga mkuu;
*Ushahidi wa barua kutoka kwa daktari aliyekuwa anakutibu;
*Barua kutoka wizara ya Afya.
6.SAFARI YA KIMICHEZO
*Barua kutoka shirikisho la mpira TFF au ZFA;
*Barua kutoka katika chama cha michezo kilichosajiliwa;
*Barua ya kualikwa.
7.SAFARI YA SKAUTI
Maombi yanatakiwa yaambatanishwe na:
*Barua kutoka kwa chama husika cha skauti;
*Barua ya ruhusa kutoka kwa mzazi kama una umri chini ya miaka 18;
*Barua ya mualiko.
8.SAFARI YA KIKAZI
Maombi yako yaambatane na:
*Barua kutoka kwa muajiri;
*Barua ya mualiko;
*Kitambulisho chako.
9.SAFARI YA KIBIASHARA
Maombi yako yanatakiwa yaambatanishwe na:
*Leseni halali ya biashara;
*Tiketi ya kurudi.
10.SAFARI YA UBAHARIA
Maombi yako yanatakiwa yaambatane na:
*Mkataba wa ajira;
*Vyeti vya taaluma;
*Barua kutoka kwa umoja wa mabaharia.
MAHITAJI YANAYOTAKIWA ILI UPATE HATI YA KUSAFIRIA:
1.HATI YA KUSAFIRIA YA DHARURA
Maombi yako yanatakiwa yaambatane na:
*Picha nne ndogo za pasipoti
2.CHETI CHA UTAMBULISHO
Muombaji wa cheti cha utambulisho anatakiwa awe na:
*Ripoti maalumu ya polisi ikiwa hakuna ubalozi;
*Picha mbili za pasipoti.
3.HATI YA KUSAFIRIA YA AGANO LA GENEVA
Muombaji wa hati hii anatakiwa awe na:
*Barua kutoka kwa mkurugenzi anayesimamia idara ya wakimbizi;
*Nakala ya kitambulisho cha ukimbizi;
*Picha mbili za pasipoti.
MAOMBI YA KUBADILISHIWA PASIPOTI NA HATI ZA KUSAFIRIA ZILIZOHARIBIKA:
Ikiwa pasipoti au hati yako ya kusafiria imeharibika kabisa au
iko katika hali ambayo ni
lazima ibadilishwe,
muombaji anatakiwa
atume maombi kwenda kwa
kamishna wa huduma za uhamiaji.
1.KUBADILISHIWA PASIPOTI
Muombaji anatakiwa awe na:
*Pasipoti iliyoharibika;
*Picha nne za pasipoti.
2.KUBADILISHIWA HATI YA KUSAFIRIA
Muombaji anatakiwa awe na:
*Hati za kusafiria zilizoharibika;
*Picha mbili za pasipoti.
MAOMBI YA KUTENGENEZEWA PASIPOTI MPYA KWA ILIYOPOTEA AU KUIBWA:
Ikiwa pasipoti imepotea au kuibiwa maombi ya kutengenezewa mpya
yanatakiwa yaambatane
na kiapo pamoja
ripoti ya mamlaka ambayo
muombaji alitoa taarifa ya kupotelewa au kuibiwa.
Muombaji anatakiwa awe na:
*Ripoti kutoka katika kituo cha polisi alichopeleka taarifa ya kuibiwa;
*Taarifa uliyotoa kupotelewa na pasipoti katika gazeti la kila siku.
KUBATILISHWA PASIPOTI AU HATI YA KUSAFIRIA
Kamishna wa idara ya uhamiaji katika muda wowote ana mamlaka ya
kubatilisha pasipoti au
hati ya kusafiria kwa aliyepewa ikiwa aliyenayo amefanya yafuatayo:
*Ameruhusu pasipoti yake itumiwe na mtu mwengine;
*Amefukuzwa nchini na serikali;
*Ikiwa aliyenayo amesitisha uraia wake wa Tanzania;
*Ikiwa aliyenayo amejihusisha na biashara ya madawa ya kulevya,
utengenezaji wa hela bandia, kuingiza isivyo halali wahamiaji,
amejihusisha na ugaidi,
na hata uhamishaji wa hela kimagendo;
*Ikiwa kwa ajili ya kulinda usalama wa nchi.
ADA YA MAOMBI YA PASIPOTI NA HATI ZA KUSAFIRIA:
1.Pasipoti ya kawaida-50,000/=
2.Pasipoti ya kidiplomasia-50,000/=
3.Pasipoti ya huduma-50,000/=
4.Pasipoti ya afrika Mashariki-15,000/=
5.Hati ya kusafiria ya dharura-10,000/=
6.Chet cha utambulisho-10,000/=
7.Hati ya kusafiria ya agano la Geneva-20,000/=
SASA KAZI INABAKI KWAKO,
KUWA NA MAHITAJI HAYO MUHIMU WAKATI UNAOMBA PASIPOTI AU HATI YA KUSAFIRIA ILI USIJE KUSUMBUKA.
Subscribe to:
Posts (Atom)