Kuna siku niliwahi kukaa
na kujiuliza,
ilikuwaje kati ya
viungo vyote mwilini,
MOYO
ndiyo uteuliwe kuwakilisha hisia
zote za binadamu.
Ukiwa katili, mpole, mkarimu, mwizi, au jasiri bado utatumika
moyo kubeba hizo sifa.
Si kitu cha ajabu kusikia mtu anapewa sifa ya kuwa na Moyo
mgumu, moyo mwepesi au moyo wa tamaa.
Nilipochunguza kwa kusoma vitabu vya kisayansi
nikagundua kuwa Moyo ndiyo kiungo cha kwanza kuishi
na cha mwisho kufa
kwa binadamu,
ndio maana kimepewa nafasi hiyo.
Kutokana na kiungo hiki kubeba matukio mengi muhimu katika maisha yetu ni vyema tukakitunza.
Hivi ni kweli moyo huvunjika?
Kisayansi haiwezekani,
lakini amini usiamini,
kihisia ni kweli moyo unavunjika.
Na mtu ambaye inasemekana moyo wake umevunjika,
raha ya maisha kwake haipo.
Kuna matukio yanayoongoza kuvunja mioyo ya binadamu,
Hebu tuyaangalie na tuanze kuyakwepa:
1.KURUHUSU WATU WABATILISHE UNAVYOJISIKIA
Kama kuna kitu unajisikia,
ni kweli ndivyo kilivyo.
Hakuna kingine watu watakachosema
chenye uwezo wa
kubadilisha hilo.
Hakuna anayeishi ndani yako
zaidi ya wewe mwenyewe.
Hakuna anayeweza kuelezea hisia zako
zaidi ya wewe mwenyewe,
usiruhusu mtu akuhukumu kwa ulilofanya kwa kuwa hajui ulikuwa katika hali gani.
Usiruhusu watu wakuaminishe tofauti na wewe unavyojisikia.
2.KUJUTIA KILA KOSA
Yaani
kama mpaka leo bado unaendelea
kujutia kosa ulilofanya muda mrefu uliopita unajivunja moyo wako.
Kumbuka katika kipindi ulichokosea,
ulifanya kutokana
na uelewa na uzoefu uliokuwa nao
muda ule na sio sasa.
Yawezekana kabisa,
uchanga wa akili
ndio ulikufanya ufanye vile
ulivyofanya,
na ndio maana kama ungepewa nafasi ya leo kufanya maamuzi
uliofanya miaka iliyopita
usingefanya kama vile hata kidogo.
Muda na uzoefu vinatupa nafasi ya kufanikiwa katika yale tunayoyafanyia maamuzi,
kwa hiyo sahau yaliyopita songa mbele.
3.KUWAPOTEZEA WANAOKUPENDA
Unajua
kuna kipindi unakuwa na watu
wanakuonyesha upendo halafu wewe unashindwa kuwaonyesha shukrani.
Hii ni sawa na
kujiandalia bomu ambalo litakuja
kukulipukia siku ile watakapoondoka kabisa machoni pako.
Na kuna kipindi,
utatamani angekuwepo karibu yako umueleze unavyojisikia
au akikusaidia shughuli fulani.
Unatakiwa umuonyeshe shukrani yule anayekufanyia upendo kila muda utakaopata.
4.KURUHUSU MATAMANIO KUKUTAWALA
Kuna kipindi tunafanya uamuzi mbaya,
sio kwasababu ni wabaya ila
ni kwasababu
tumejali zaidi kuwafurahisha wengine
kuliko fahari yetu.
Unapokubali
kufanya uamuzi wa tamaa ya kutaka
uonekane mtu fulani
ni
kujitengenezea uasi wa ndani.
5.KUTAKA KUBISHANA KILA HOJA
Kuwa shujaa sio kupigana kila vita
inayokuja mbele yako,
au
si kujibu kila shutuma dhidi yako.
Kama unaona hilo jambo
litakushushia heshima na utu wako,
ni heri ukaachana nayo ili yasiweze kuzaa mengine mapya
na mabaya zaidi.
6.KUHARAKISHA UHUSIANO
Uhusiano
mzuri ni wa watu ambao kila mmoja
amempokea mwenzake kwa hali yake
aliyonayo,
na kumsaidia atoke
hapo alipo kwenda katika hali
iliyobora zaidi ya aliyomkuta nayo.
Usikimbilie
kuwa katika uhusiano na mtu kwa kuwa, mazingira au
nafasi imetokea tu.
Tafuta mwenza ambaye atakuhimiza kukua,
asiyeng'ang'ania ufanye
anachopenda yeye kila wakati,
atakayekuruhusu uchangamane na watu wengine, na atakayekuamini.
7.KUMNG'ANG'ANIA ANAYETAKA KUONDOKA
Ni uchungu sana,
kumuaga mtu unayetaka abaki,
lakini ni maumivu zaidi kumng'ang'ania anayetaka kuondoka.
Kama unayemuonyesha upendo na,
hataki kurudisha upendo kwako
usikae kulazimisha kwani utaendelea kujiumiza tu na
kuwa mtumwa kwake.
Mtu pekee unayepaswa kuwa naye ni yule anayekuheshimu na anatambua umuhimu wako katika maisha yake.
8.KUKATAA KILA USHAURI
Si kila
ushauri utakao pewa
utakuwa sahihi sawa,
lakini
si kila ushauri utakuwa mbaya kwako.
Kubali kupokea
marekebisho kutoka kwa watu
wengine.
Usijitengenezee mazingira ya kuja kuuvunja moyo wako siku zijazo kwa kujuta.
RAHA YA MAISHA NI KUISHI KWA AMANI NA FURAHA,
KAMA UTAENDELEA KUJIWEKA
KATIKA MAZINGIRA YA KUJA
KUUVUNJA MOYO WAKO,
HAUTAONA LADHA
YA MAISHA KAMWE.
ANZA LEO KUUTUNZA MOYO WAKO.
0 comments:
Post a Comment