“Usimamizi wa ubora, usalama, hadhi, mahusiano,
ushirikiano, na sera ya ofisi ni mambo muhimu ya kumfanya mfanyakazi aridhike
na mazingira yake ya kazi”
Mwisho wa kunukuu maneno ya msomi wa enzi hizo ndugu
Fredrick Herzeberg, ambaye alikuja kumwagia zege nadharia iliyofanyiwa utafiti
mwaka 1927 mpaka 1932 na Profesa Elton Mayo.
Profesa alifanya utafiti wa kuchunguza mazingira ya
kazi na tija, pindi alipoona mfumo wa kuwaweka watu wengi wenye historia
tofauti katika eneo moja la kazi.
Alisisitiza kuwa mahusiano mazuri kazini
huongeza tija ya kazi, kwani utendaji wa kila siku wa wafanyakazi unategemea
sana mahusiano baina yao.
ONYESHA
MTAZAMO CHANYA
Kuna kampeni ya usafi Dar es Salaam
ina msemo usemao “Usijifanye mstaarabu bali kuwa mstaarabu”. Hata katika
mtazamo pia unapaswa usijifanye una mtazamo chanya bali waoneshe wenzako kwa
vitendo kuwa wewe una mtazamo chanya.
Mathalani mfanyakazi mwenzako
amekumbana na tatizo katika utendaji wake na anaonyesha kuchanganyikiwa ila
wewe ukawa mtuliza dhoruba kwa kuwa chanya na tatizo lake na kumpa njia mbadala
za kutoka.
Nakwambia ukiwa hivi utakuwa
unawavutia wenzako kuja kwako pindi wanapokumbana na changamoto.
ONYESHA
SURA YA FURAHA KILA UTAPOTOA SALAMU
Unawezaje kuingia ofisini macho
chini, umeshusha mabega, bila hata ya kutoa salamu na unaenda moja kwa moja
kuanza kazi?
Kama hii ndio tabia yako, utaendelea
kuwaona wafanyakazi wenzako wakikuchunia au hata kukukwepa kila wakikuona.
Kuwa na tabia ya kutoa salamu kila unapokutana na
wafanyakazi wenzako huku ukionyesha uso wa furaha, hii itawapa ishara wenzako
kuwa unafuraha kuwa nao eneo moja la kazi.
JIBU
BARUA PEPE NA UJUMBE WA SIMU KWA WAKATI
Utajisikiaje pale ambapo
umemtumia mtu ujumbe uwe wa barua pepe au ujumbe wa kawaida wa simu na
anachukua muda mrefu kukujibu au asijibu kabisa?
Hii itaonyesha una dharau
kwa wenzako, na kwamba wao hawana umuhimu kwako. Jenga tabia ya ukarimu wa
kujibu ujumbe wa mtu kwa wakati, hii itakufanya uonekane unajali na itawapa
urahisi wao kukushirikisha taarifa muhimu kwa wakati.
KUBALI
UTANI ENEO LA KAZI
Simaanishi ukubali kila utani
utakaotaniwa hata ule unaovuka mipaka, bali ule utani ambao ni wa kawaida
usiovuka mipaka upalilie ili uwafanye wenzako wafurahie uwepo wako kwani
dhumuni kubwa la utani ni kufurahi pamoja.
Usishangae mtu huna hata mazoea nae
ila akaanza kukutania, hii ina maanisha anataka kupata picha wewe ni mtu wa
namna gani. Hasa ukizingatia kuwa ishazoeleka kuwa mtu wa utani ni rahisi
kuingilika kwa maongezi na si mtu wa kukasirika hovyo.
TENGENEZA
UAMINIFU
Unapokutana na wengine eneo la kazi
hakuna anayejua kuwa wewe ni muaminifu mpaka utakapofanya tendo la uaminifu
mbele yao. Hata siku moja mtu asikwambie kuwa yeye si mwizi kama eneo au mazingira
anayoishi hakuna cha kuiba.
Vivyo hivyo huwezi kuwaambia watu wewe ni muaminifu
na mkweli kama haujawahi kuonyesha mbele yao tukio la uaminifu na ukweli.
Mathalani endapo umekosea jambo
Fulani na ukakubali na kukiri mbele ya wenzako, hii itawajengea picha kuwa wewe
ni muaminifu na msema kweli.
KUWA
MTU WA KUTOA MSAADA KWA WENZAKO
Kutoa msaada wa maarifa na utaalamu
katika eneo la nje ya muongozo wako wa kazi ni msaada tosha kwa mfanayakazi
mwenzako mwenye kuhitaji msaada wako.
Kwa mfano wewe unafahamu kutengeneza
kitu Fulani ambacho mfanyakazi mwenzako unamuona kimemuharibikia na anashindwa
kukitengeneza, ukijitokeza kumsaidia utakuwa umeimarisha uhusiano wako na yeye
na atakuona ni mtu mzuri kuishi nae eneo moja la kazi.
HESHIMU
TOFAUTI ZA UTAMADUNI KATI YAKO NA WENZAKO
Mazingira ya kazi katika zama hizi
yameendelea kuwaleta pamoja watu wenye historia tofauti, kuanzia malezi mpaka
jamii wanazotokea.
Jinsi wewe unavyokuwa unatumia muda
wako na kiwango cha umakini lazima kitatofautiana na wenzako.
Usiwe mtu wa kujilinganisha na
kuwaona wenzako ni watu wa ajabu kwakuwa hawapo kama wewe, bali fungua masikio
na macho yako kujifunza kitu kutoka kwao ambacho wewe huwezi kukifanya kama
wao.
Unapokuwa mtu wa kuheshimu tofauti
zako na za wengine, utawafanya na wao watamani kujifunza kitu kutoka kwako,
hivyo kuimarisha mahusiano yenu eneo la kazi.
KUWA
NA HESHIMA KWA WOTE
Kama unadhani heshima ni kuamkia
wakubwa tu hasa wale unaofanya nao kazi, basi nakuomba utafakari upya. Heshima
ni nguzo muhimu sana katika kujenga mahusiano bora eneo la kazi.
Kumheshimu
mwenzako ni pamoja na kujua mipaka ya kauli na maneno ya kuongea mbele yake
hata kama umemzidi cheo au umri.
Ukiwa na heshima kwa wengine
itakusaidia usiwe miongoni mwa watu wanaopenda kujadili watu wengine kwa mabaya.
Ukiwaonyesha heshima watavutika kuja kwako na mahusiano yenu yataimarika.
SHIRIKIANA
NA WENZAKO KATIKA VITU WANAVYOPENDA
Muulize mfanyakazi mwenzako kuhusu
vitu anavyopenda kufanya, aina ya muziki anaosikiliza, filamu amazoangalia, na
hata vitabu anavyosoma.
Baada ya kufahamu angalia chochote ambacho mnaendana
shirikiana nae, kwa mfano umegundua anapenda sana kuangalia mpira sio mbaya
kama ukijiunga nae kama na wewe ni muangaliaji pia.
SHIRIKI MITOKO NA WENZAKO
Kufahamiana na wafanyakazi wenzako nje
ya eneo la kazi ni jambo zuri sana. Ndio maana ofisi nyingi lazima utakuwa kila
baada ya muda Fulani wanaandaa tafrija ya kuwakutanisha wafanyakazi katika
bonanza ili kujenga mahusiano mazuri baina yao.
Hata kama ofisi haiandai matukio kama
hayo ila sio mbaya kama utakuwa unatumia muda wako japo kidogo kutoka na kwenda
mahali na wenzako kupata vinywaji au chakula nje ya muda wa kazi ili kuboresha
mahusiano mazuri.
Je, unajua waajiri wakati mwingine hulipa kiwango kikubwa
Cha mshahara kwa kuwa mwajiriwa ana elimu sahihi na uzoefu? Je, unaweza kuwa na
uwezo wa kupata mshahara mkubwa kwa kufanya kazi moja katika kampuni kubwa? Ni
dhahiri, hivi vinaweza kuwa baadhi ya vitu vya nguvu katika mazungumzo wakati wa
mapitio ya utendaji wako, usaili wa
kazi, au ombi kwa ajili ya kupandishwa cheo.
Waajiri kawaida hurekebisha taarifa za malipo wakati wa
kuamua kiasi gani cha kumlipa mfanyakazi wa kufanya kazi maalumu. Baada ya wao
kuamua thamani ya nafasi kwa kutafiti taarifa juu ya viwango vya malipo kwa
ajili ya kazi hiyo kulinganishwa katika makampuni mengine yanayofanya shughuli
sawa na wao, ila watakubali kubadilisha kwa kuzingatia elimu na uzoefu wa
mwombaji.
Miaka ya uzoefu
Kwa kawaida, ukiwa na uzoefu zaidi huchangia kulipwa kiwango
cha juu cha mshahara. Vile vile, kama nafasi imetangazwa na anahitajika mtu
mwenye uzoefu wa miaka 10 katika kazi fulani, na wewe huna wala haukidhi
mahitaji hayo, ukibahatika ukapata hiyo kazi tambua lazima utalipwa kiwango
kidogo.
Elimu
Uwiano kati ya elimu yako na kiwango kinachohitajika kwa
ajili ya kazi kwa kawaida huathiri mshahara utakaolipwa. Pia, ubora wa elimu
unaweza kuathiri mshahara. Kupata shahada kutoka katika kozi inayoheshimika,
kawaida ina ushawishi chanya juu ya kulipwa kwako, wakati kupata shahada kutoka
katika chuo ambacho huchukuliwa dhaifu hupunguza uwezo wako wa kupata mshahara
mkubwa.
Utendaji wa kitaalamu
Tangu kitambo waajiri wengi hutumia msingi wa maamuzi yao
kulipa mshahara angalau kwa kiwango cha juu kwa kuzingatia utendaji wa mtu
binafsi, hiki ndio kipimo cha kutofautisha
viwango vya mshahara wakati wa kutaka kuongeza mshahara au cheo. Hata
wakati unapoomba kazi mpya, habari hii inaweza kuwa muhimu kwa mwajiri wako,
kwani inatoa picha kamili juu ya uwezo wako.
Mkuu wako wa kazi
Mchango wako na uhusiano wako wa kiutendaji katika mafanikio
ya kampuni yako, endapo mkuu wako wa kitengo cha kazi ana nafasi kubwa katika
maamuzi ya kampuni, mapendekezo yake kuhusiana na malipo yako yana nafasi
kidogo ya kupingwa wakati wa mapitio.
Idadi ya wanaoripoti kwako
Jinsi unavyokuwa na idadi ya wafanyakazi wengi wa
kuwasimamia na kuleta ripoti kwako, ndivyo utakavyoweza kulipwa kiwango cha juu
katika kazi fulani. Bila shaka, ngazi yako ya mafanikio inategemea msingi wa
utendaji wa wafanyakazi ambao unawasimamia.
Kutunukiwa na vyama
vya Kitaalamu
Vyeti na uanachama katika bodi za kitaalamu au vyama
vya biashara unaweza kuwa chagizo chanya kuathiri juu ya kulipwa kwako kwa kiwango
cha juu. Hata hivyo, kama kazi uliyopata na hauna vyeti vinavyohitajika, kulipwa
kwako lazima kuanzie kiwango kidogo. Baadhi ya waajiri wanahimiza wafanyakazi
wao watafute vyeti vyenye vigezo.
Tofauti ya zamu
Katika kazi fulani, wafanyakazi wanaweza kutarajiwa kufanya
kazi katika nyakati ambazo si muda ambao ni mzuri na unaopendwa na wengi.
Wafanyakazi wa nyakati hizi ni kawaida kulipwa kiwango cha juu kutokana na
gharama kubwa za kijamii na kimwili kushiriki katika kufanya kazi nje ya
"masaa ya kawaida ya kazi." Katika kazi ambazo hakuna zamu za kuingia
kazini, tofauti ya malipo ni kidogo.
“Hakuna binadamu mkamilifu”, huu msemo hatujaanza kuusikia leo, ila ni wachache kati yetu tunaoweza kuupa maana yake kamili pale ambapo kuna kosa limefanyika iwe na mtu mwengine au sisi wenyewe. Ukiwa unajua kuupa maana msemo huu hautakuwa mgumu kusamehe au kujisamehe na kutafuta njia mbadala za kutatua hilo tatizo kwa kuwa unatambua wazi binadamu hatuwezi kufanya jambo sahihi kila siku.
Wote ni mashahidi tulipokuwa tunaangalia mashindano ya Copa Amerika Lionel Messi katika hatua za awali alijituma sana kuifikisha nchi yake fainali na wote walimwona shujaa, lakini siku ya mwisho alikosa penati iliyowafanya kukosa kombe.
Wote tunajua maamuzi aliyochukua baada ya mechi, alitangaza kujiuzulu kwani alikosa msamaha kwake mwenyewe kwakuwa alijihisi alipaswa kuwa mkamilifu kwa kuwa anajua watu wanamwona kama mtu asiyekosea.
Kukosea tumeumbiwa wanadamu, na mara nyingi tunapogundua tumekosea katika eneo letu la kazi, tunajikuta tunaingia hatia mioyoni mwetu na hatujui tunaweza kumudu vipi hali hiyo.
KUBALI KOSA LAKO, NA MSHIRIKISHE MTU ANAYESTAHILI KUAMBIWA
Kama upo eneo la kazi na umefanya kosa, ni lazima kuna watu wataathirika na tukio lako. Jinsi unavyochukua muda mrefu kuelezea ulichokosea kwa litakaye mwathiri, ndivyo litakavyochukua muda mrefu kurekebisha makossa uliyofanya. Inaogofya kukubali kuchukua lawama za makosa uliyotenda, hasa ukizingatia unajua wazi kuna mtu atakukasirikia baada ya kusema ukweli, lakini nakwambia ni bora kulamba ncha ya kisu na kusema mapema kuliko kusubiri madhara yawe makubwa.
Kama unajiona unaweza kurekebisha vitu wewe mwenyewe, bila kusimamiwa wala kuelekezwa na mtu, haitakuumiza kujaribu mwenyewe, ila ikitokea umekosea usiache kuomba msaada na si kujipa moyo kwamba utaweza kurekebisha kimya kimya. Watu wenye tabia ya kurekebisha makosa kimya kimya bila kumshirikisha mtu mwengine, hujitahidi kwa bidi zote ili kuficha aibu ya kuonekana wamekosea.
Ukweli ni kwamba kosa ulilofanya unaweza kuliona dogo, lakini kumbe jinsi unavyoliweka kimya huku hupati suluhisho la haraka linakuwa kubwa lisilorekebishika kuliko ulivyotarajia.
Katika mahojiano na chuo cha biashara cha Harvard, mwenyekiti wa kampuni ya Toyota Katsuaki Watanabe alielezea kwanini ni vyema kuweka wazi tatizo:
“Tatizo lililofichwa ndio huja kuwa janga kubwa. Kama tatizo likiwekwa wazi kila mtu akalitambua, najisikia salama. Hii ni kwasababu tatizo linapowekwa katika lugha ya picha, hata kama watu wetu hawakulitanbua tangu mapema, watazisumbua akili zao kutafuta suluhisho.
”
Unapoenda kumwelezea mkuu wako wa kazi kilichotokea, ukweli ni sera bora kuliko zote. Achana na udhuru wa kutaka kuwaangushia wengine tatizo lako ili muathirike wote bali kubali kulibeba mwenyewe na ueleze ukweli wa kilichotokea.
Kama kuna kazi ulipewa na ukasahau kuifanya kwa wakati, mweleze mkuu wako na kama una sababu ya maana ya kwanini haukufanya weka wazi.
Kama ulipewa kazi na wakati unaifanya haikwenda sawa, usiogope kama ulijitahidi kutumia nguvu na akili yako kutimiza wajibu wako. Usiache tatizo kubwa liwe kubwa Zaidi kwa kujifanya hakuna kilichotokea.
Hakikisha unaonyesha na hata kuwaomba msamaha wale wote walioathirika na makosa yako. Ulichokifanya sio kwamba umedhamilia kwajili ya kumuumiza mtu,bali unatakiwa kuchukua mzigo wote wa lawama na na kuomba radhi mwisho wa siku.
LETA SULUHISHO MBADALA LA KUTATUA TATIZO
Nadhani hautapenda uwe mtu anayeleta matatizo katika eneo lako la kazi pasipo kuleta suluhisho,haijalishi hilo tatizo limeletwa na wewe au mtu mwengine.Unapokuwa umekosea jambo Fulani na ukajitahidi uwe na na njia chache za suluhisho tayari kichwani hii itakusaidia kupunguza ukubwa wa nyundo zitakazokushukia.
Katika mazingira ya siku hizi ya kazi, kama unataka kuwa mfanyakazi mwenye kuthaminiwa, usliwe mleta matatizo kwa meneja wako bali leta suluhisho. Unajua kwanini? Kwasababu kuna matatizo mengi meneja anatakiwa kutatua wenyewe, sasa hutakiwi kuwa sehemu ya tatizo.
Njoo na njia lukuki za kutatua makosa yako, na chagua moja unalohisi ndio sahihi kabisa. Weka katika maandishi kabisa kama kuna ulazima na uwe na majibu tayari kwaajili ya maswali utakayoulizwa na meneja wako.
Mpe muhtasari meneja wako wa hilo suluhisho lako sahihi lakini pia uwe na masuluhisho mengine karibu ikiwa meneja wako hajakubaliana na suluhisho lako la kwanza.Ndio yawezekana kabisa umezamisha meli lakini haimaanishi usionyeshe juhudi za kuiokoa mbele ya meneja wako. Unaweza kutafunwa kama bazooka, lakini utakuwa sehemu salama kwa kuwa umeonyesha juhudi za kuokoa jahazi baada ya kukosea.
JISAMEHE MWENYEWE NA JIFUNZE KUPITIA MAKOSA
Kuyakabili makosa yako ni jambo gumu, lakini ni muhimu kujisamehe mwenyewe punde tu unapokuwa umekosea.Umekosea kweli, lakini sio kitu cha ajabu kila binadamu huwa anakosea kwa nafasi yake.
Ufanye msamaha kuwa sehemu ya maisha yako kila siku,na unapojikuta umefanya kosa kubwa, jitahidi kufikiria namna ya kutatua tatizo badala ya kukaa kujilaumu kila wakati.
Wewe sio mtu wa kwanza kufanya kosa kubwa kama hilo, jaribu kufuatilia watu ambao unao waangalia kama mfano kwako na uwadadisi na utagundua kumbe makossa ni sehemu ya binadamu katika kufikia mambo mazuri na kuwa yote waliyopitia ni sehemu ya mchakato.
TENGENEZA UAMINIFU TENA KWA MENEJA WAKO
Baada ya kufanya kosa kubwa na meneja wako akaligundua hutakiwi kufikiria kuacha kazi badala yake jitahidi uonyeshe kwamba haujarudishwa nyuma na kosa lile bali una nafasi ya kufanya tena jambo linguine kwa usahihi.
Anza kujenga uaminifu tena kwa mambo madogo madogo na sio ushikwe na munkari utake kuonyesha umahiri katika mambo makubwa ambayo huna uzoefu nayo na yanaweza kukurudisha tena katika kukosea.
MAMBO SITA UNAYOPASWA KUJIKUMBUSHA KILA WAKATI UNAPOKUTANA NA UGUMU KATIKA KUFANIKISHA MALENGO YAKO.
Acha ukweli usemwe, furaha ya kweli si kutokuwa na matatizo,
lakini ni uwezo wa kukabiliana nayo kwa ujasiri. Mara zote angalia kile ulicho
nacho mkononi, badala ya kufikiria ulichopoteza. Sababu haijalishi dunia imechukua
nini kutoka kwako, bali utafanya nini na kile ulichobaki nacho mkononi.
Yafuatayo ni mambo sita unayopaswa kujikumbusha kila
unapopatwa na jambo gumu linalotaka kukukatisha tamaa ili usisonge mbele.
1.
MAUMIVU NI SEHEMU KATIKA UKUAJI
Kuna kipindi maisha yanafunga mlango sababu
ni muda muafaka kusonga mbele. Na hiki ni kipindi kizuri sababu mara nyingi
hatuwezi kusonga mbele wenyewe mpaka matukio Fulani yatokee kutusukuma ndo
tunasonga.
Mambo yanapokuwa magumu jikumbushe kuwa
hakuna maumivu yanayokuja bila dhumuni maalumu. Songa mbele baada ya maumivu
lakini usisahau ulichojifunza kipindi cha maumivu.
Eti kwasababu una pata mahangaiko ndo
imaanishe kuwa unafeli maisha. Kila jambo lolote kubwa la mafanikio huwa haliji
kirahisi mpaka liambatane na mahangaiko ya hapa na pale. Mambo mazuri huchukua
kipindi kirefu kukamilika. Kuwa mvumilivu na kuwa na mtazamo chanya. Kila kitu
kitaenda kuwa sawa, labda sio kwa kasi unayoitaka wewe lakini mambo yatakuwa
sawa tu.
Kumbuka kuna maumivu ya aina mbili, kuna
yale yanayokuumuiza na yale yanayokubadilisha. Ukiwa unaenda na mtiririko wa
jinsi maisha yanavyokwenda, badala ya kupingana na mabadiliko, itakusaidia
kukua.
2.
KILA KITU KIPO KWA MUDA TU
Kila wakati mvua inaponyesha, huwa kuna
muda itaacha. Kila wakati wewe unapopata madhara, kuna wakati wa wewe kupona.
Baada ya giza daima kuna mwanga - wewe hili unakumbushwa kila asubuhi, lakini
bado mara nyingi unasahau, na badala yake unachagua kuamini kwamba usiku
utadumu milele. Haitakuwa hivyo. Hakuna kinacho dumu milele.
Hivyo kama mambo ni nzuri sasa hivi,
furahia. Sababu haitadumu milele. Kama mambo ni mabaya, msiwe na wasiwasi kwa
sababu haitakuwa milele. Kwa sababu tu maisha si rahisi wakati huu, haina maana
huwezi kucheka. Kwa sababu tu kitu kinakusumbua
wewe, haina maana huwezi tabasamu. Kila wakati unakupa mwanzo mpya na mwisho
mpya. Unapata nafasi ya pili, kila wakati . Wewe unapaswa kuchukua nafasi na
kuufanya kuwa ni wakati bora zaidi.
3.
KUWA NA HOFU NA KULALAMIKA HAKUBADILISHI KITU
Wale ambao wanalalamika zaidi, kukamilisha
mambo inakuwa ni ngumu. Ni vyema kujaribu kufanya jambo kubwa na kushindwa
kuliko usijaribu kufanya chochote na utarajie kufanikiwa. Sio mwisho kama
umefanya jambo na ukashindwa; na sio mwisho pia kama haujafanya jambo lolote lakini
ukaishia kulalamika kuhusu hilo jambo.
Kama unaamini katika kitu, usiache
kuendelea kujaribu. Usikubali vivuli vya zamani vikazima hatua zako za maisha
yako ya baadaye. Ukiwa unaitumia leo kulalamika kuhusu jana hautaifanya kesho
kuwa nzuri.
Badala yake chukua hatua. Hebu tumia ulichoweza kujifunza kuboresha
jinsi ya kuishi. Endelea kufanya mabadiliko na kamwe usiangalie nyuma.
Furaha ya kweli utaipata pale tu utakapoacha
kulalamika kuhusu matatizo yanayokukuta bali unatakiwa uanze kushukuru kwa
matatizo ambayo hauna.
4.
MAKOVU YAKO NDIO NGUVU YAKO
Usije kuona aibu hata siku moja kutokana na
makovu ambayo maisha yamekupa. Kovu ina
maana uliwahi kuumizwa na tatizo limekwisha na jeraha limefunga. Ina maana wewe
alishinda maumivu, umejifunza somo, umekuwa na nguvu, na umesonga mbele. Kovu
ni alama ya ushindi ya kujivunia.
Usije kuruhusu makovu yako yakushikilie
mateka. Usije kuyaruhusu yakufanye uishi maisha yako katika hofu. Huwezi
kufanya makovu katika maisha yako kutoweka, lakini unaweza kubadilisha mtazamo
wa jinsi unavyoyaangalia. Unaweza kuanza kuona makovu yako kama ishara ya nguvu
na si maumivu.
5.
KILA KIKWAZO KIMOJA NI HATUA YA KUKUA
Katika maisha, uvumilivu si kuhusu kusubiri
tu; ni uwezo wa kushikilia tabia nzuri wakati wa kufanyia kazi kwa bidii ndoto yako, ukijua kwamba kazi unayofanya ni ya thamani. Hivyo kama unakwenda
kujaribu, jitahidi kuweka muda wako wote huko.
Vinginevyo, hakuna faida kuanzisha jambo.
Hii inaweza kuwa na maana ya kupoteza utulivu na faraja kwa wakati, na labda
hata akili yako juu ya tukio. Na inaweza kumaanisha kukosa kula, au kukosa
kulala, kama ulivyozoea, kwa siku kadhaa.
Na inaweza kuwa na maana kutoka eneo lako
la faraja na ukaruruhusu kuumizwa na baridi kwa ajili ya jambo unalojaribu. Inaweza
kumaanisha kutoa sadaka mahusiano na yote yale ambayo ni yako. Inaweza kuwa na maana
ya kukubali kejeli kutoka kwa wenzako.
Kila kitu kingine ni mtihani wa dhamira
yako ni kiasi gani cha wewe kweli unataka kutimiza jambo uliloanzisha.
Na kama unataka kutimiza jambo, itabidi
kufanya, hata kama litaambatana na matukio ya kushindwa na kukataliwa. Na kila hatua utakayopiga
utajisikia vizuri kuliko kitu kingine chochote unaweza kufikiria.
Utagundua
kuwa mapambano hayapatikani katika njia, bali ni njia. Na ni thamani yake.
Hivyo kama wewe unakwenda kujaribu,nenda njia yote. Hakuna hisia bora katika
dunia ... hakuna hisia bora kuliko kujua nini maana ya kuwa hai.
6.
MITAZAMO HASI YA WENGINE SIO TATIZO LAKO
Kuwa na mtazamo chanya wakati mazingira yametawaliwa
na mitazamo hasi. Tabasamu wakati wengine wanajaribu kukurudisha chini. Si
jambo rahisi kudumisha shauku yako na kuzingatia unakoelekea. Wakati watu
wengine wanakutenda vibaya, endelea kuwa wewe. Milele usiruhusu tabia chungu za
mtu mwingine zilete mabadiliko kwako.
Zaidi
ya yote, milele usikubali kubadilika ili kumvutia mtu ambaye anasema wewe hauna
uwezo. Badilika sababu itakufanya mtu bora na itaenda kubadilisha kitu katika
maisha ya mbeleni. Watu wataendelea kuzungumza bila kujali nini unafanya, hata
iwe unafanya vizuri kiasi gani. Hivyo kuwa na wasiwasi kuhusu mwenyewe kabla ya
kuwa na wasiwasi kuhusu nini wengine wana kufikiria. Kama unaamini kwa dhati
katika kitu, wala hupaswi kuwa na hofu ya kupambana kwa ajili yake. Nguvu kubwa
inatokana na kushinda kitu ambacho wengine walifikiria hakiwezekani.
Utani wote weka pembeni, maisha yako yanakuja
mara moja tu. Huo ndio ukweli. Hivyo kufanya kitu kinachokupa furaha ndio
kinapaswa kuwa kipaumbele chako.
JE, UNAZIFAHAMU STADI AMBAZO WAAJIRI WENGI WANAZIANGALIA KWA WAFANYAKAZI/WAOMBAJI WA KAZI? SOMA UJIELIMISHE.
Ukikutana na
mtafuta ajira kilio chake kikubwa ni nimefanyiwa usaili mara nyingi ila baada
ya hapo sijaitwa tena.
Waajiri huwa wanatumia vigezo gani katika kujaza nafasi za kazi
katika ofisi zao? Kama unadhani una jibu moja litakalo wawakilisha waajiri wote
kutokana na swali hilo, naomba nikwambie tafakari Zaidi.
Waajiri wote si sawa, anachokitafuta mwajiri mmoja kinaweza
kuwa tofauti na mwajiri mwengine. Sababu inaweza kuwa ni kuwa mazingira ya kazi
ya mwajiri mmoja yanatofautiana na mwajiri mwengine, kwahiyo watakapokuwa
wanakusaili watakuwa wanaangalia vitu tofauti kutoka kwako.
Kila mwajiri anatafuta stadi za mwombaji zitakazoendana na
kazi alizonazo katika ofisi yake ili kuboresha ufanisi wa kazi ili kutoa bidhaa
au huduma nzuri kwa wakati na ubora unaotarajiwa na mteja. Lakini nje ya stadi
kuna vitu ambavyo waajiri wengi wanafanana katika kuviangalia kutoka kwa
mwombaji wa ajira.
Habari nzuri ni kuwa watafuta ajira wengi wanazo hizo sifa
ila tu wanashindwa kuzionyesha wanapopata nafasi ya kuzionyesha. Na habari
nzuri Zaidi ni kuwa kwa wale ambao hawana wanaweza kujijengea tabia hizi na
zikawapa nafasi nzuri ya kuajiriwa kwa kupata mtu sahihi wa kuwaelimisha.
Na habari nzuri Zaidi ni kuwa utakapozijua hizi tabia utaweza
kuboresha mfumo wako wa uombaji kwa kuelekeza moja kwa moja katika wasifu wako
kile anachotafuta mwajiri katika kazi husika. BAdala ya kujaza masifa kibao
katika wasifu wako utajua namna ya kuweka zile za muhimu.
1. UWEZO
WA KUWASILIANA
Uwezo wa kuwasiliana upo katika pande
tatu moja ni uwezo wa kusikiliza, pili ni uwezo kuongea na tatu ni uwezo wa
kuandika. Na kama unavyojua lugha yetu ya kiofisi ni kiingereza sasa ukiwa
vizuri katika pande hizo tatu utajiweka katika nafasi nzuri katika soko la ajira.
Unapokuwa na uwezo wa kupokea maelekezo kwa haraka na kuyahamishia katika
maandishi na ukaweza kueleza matokea yake iwe kwa maandishi au mdomo ufanisi
kazini utakuwa juu.
Utajisikiaje unampa maelekezo mfanyakazi wako jinsi ya
kufanya kazi Fulani na akashindwa kufanya kama ulivyomuelekeza kisa hamuelewani
lugha?
2.UWEZO
WA KUTUMIA KOMPYUTA
Hapa tuelewane vizuri, kujua kompyuta
haimaanishi lazima uwe umesomea kozi yake miaka kadhaa chuo labda kama kazi
unayoomba inahusiana moja kwa moja na uweledi wa kompyuta kwa kusomea kozi
husika. Ila kama unaomba kazi ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na masomo
ya kompyuta, nataka nikwambie haimaanishi ndo usijue kitu kuhusu kompyuta.
Dunia hii ya utandawazi kila kazi kwa namna moja ama nyingine ili kuikamilisha lazima
kompyuta itaingia kati sasa kama hujui kuitumia kabisa utakuwa unajipunguzia
soko. Mathalani uweze kutuma barua pepe (E-mail), programu ya maandishi
(Microsoft word) na program ya namba na maandishi (Microsoft Excel)
3.UWEZO
WA KUBADILIKA/KUFANYA KAZI ZAIDI YA MOJA
Katika dunia hii ambayo ukuaji wa
teknolojia na ushindani wa huduma na bidhaa umekuwa mkubwa ofisi nyingi
hupunguza gharama kwa kuajiri watu wachache wenye uwezo wa kufanya kazi Zaidi
ya moja ili gharama za kuzalisha ziwe ndogo na wao waweze kushusha bei
kupunguza ushindani na kuliteka soko.
Hivyo ukiwa na sifa ya uelewa wa kazi
Zaidi ya moja utajiongezea nafasi katika soko la ajira.
4.UWEZO
WA KUCHANGANYIKA NA WENGINE
Katika mazingira ya ofisi ambayo
binadamu Zaidi ya mmoja wanashirikiana kufanikisha lengo moja la ofisi, uwezo wa mfanyakazi mmoja
kuchangamana na mwengine bila tatizo ni jambo la muhimu sana.
Ofisi inaweza
kuruhusu mtofautiane kwa hoja ili kupata kitu kizuri lakini si kugombana sababu
wazo la mmoja limepingwa na wengi na kuwanunia, hii italeta utengano na
kushusha ufanisi mahali.
Ukiwa na uwezo wa kuchangamana na wengine mathalani
katika wasifu wako ukaweza kuonyesha kwamba uliwahi kufanya kazi na watu Fulani
na kufanikisha jambo Fulani.
5.UWEZO
WA KUONGOZA
Sehemu yoyote ambayo wanakutana watu
Zaidi ya wawili lazima kuwe na kiongozi na lazima ujue miongoni mwenu lazima
atoke kiongozi.
Waajiri wengi wanapenda mtu mwenye uwezo wa kuongoza sababu
wenye tabia hii huwa na uwezo wa kufanya maamuzi ya kibunifu hivyo wanatarajia
hata wakati wa utendaji wako utakuwa unafanya kwa ubunifu na kuwaongoza wengine
na si kufuata njia zile zile
zilizopitiwa na wengine na hivyo kuongeza ufanisi kazini.
HAUJACHELEWA KUFANYA MAREKEBISHO PALE AMBAPO UNAONA UNA MAPUNGUFU ILI KUONGEZA UWEZO WAKO WA KUAJIRIKA KATIKA SOKO LA USHINDANI WA AJIRA.
HAKUNA ALIYEZALIWA NA SIFA ZOTE HIZO BALI WENGINE WAMEZITENGENEZA NA WAKAWEZA KUZIFANYA KUWA SEHEMU YA MAISHA YAO NA MATOKEO MAZURI WAKAYAPATA.
ANZA SASA KUPIGA HATUA...
Subscribe to:
Posts (Atom)