Ukikutana na
mtafuta ajira kilio chake kikubwa ni nimefanyiwa usaili mara nyingi ila baada
ya hapo sijaitwa tena.
Waajiri huwa wanatumia vigezo gani katika kujaza nafasi za kazi
katika ofisi zao? Kama unadhani una jibu moja litakalo wawakilisha waajiri wote
kutokana na swali hilo, naomba nikwambie tafakari Zaidi.
Waajiri wote si sawa, anachokitafuta mwajiri mmoja kinaweza
kuwa tofauti na mwajiri mwengine. Sababu inaweza kuwa ni kuwa mazingira ya kazi
ya mwajiri mmoja yanatofautiana na mwajiri mwengine, kwahiyo watakapokuwa
wanakusaili watakuwa wanaangalia vitu tofauti kutoka kwako.
Kila mwajiri anatafuta stadi za mwombaji zitakazoendana na
kazi alizonazo katika ofisi yake ili kuboresha ufanisi wa kazi ili kutoa bidhaa
au huduma nzuri kwa wakati na ubora unaotarajiwa na mteja. Lakini nje ya stadi
kuna vitu ambavyo waajiri wengi wanafanana katika kuviangalia kutoka kwa
mwombaji wa ajira.
Habari nzuri ni kuwa watafuta ajira wengi wanazo hizo sifa
ila tu wanashindwa kuzionyesha wanapopata nafasi ya kuzionyesha. Na habari
nzuri Zaidi ni kuwa kwa wale ambao hawana wanaweza kujijengea tabia hizi na
zikawapa nafasi nzuri ya kuajiriwa kwa kupata mtu sahihi wa kuwaelimisha.
Na habari nzuri Zaidi ni kuwa utakapozijua hizi tabia utaweza
kuboresha mfumo wako wa uombaji kwa kuelekeza moja kwa moja katika wasifu wako
kile anachotafuta mwajiri katika kazi husika. BAdala ya kujaza masifa kibao
katika wasifu wako utajua namna ya kuweka zile za muhimu.
1. UWEZO
WA KUWASILIANA
Uwezo wa kuwasiliana upo katika pande
tatu moja ni uwezo wa kusikiliza, pili ni uwezo kuongea na tatu ni uwezo wa
kuandika. Na kama unavyojua lugha yetu ya kiofisi ni kiingereza sasa ukiwa
vizuri katika pande hizo tatu utajiweka katika nafasi nzuri katika soko la ajira.
Unapokuwa na uwezo wa kupokea maelekezo kwa haraka na kuyahamishia katika
maandishi na ukaweza kueleza matokea yake iwe kwa maandishi au mdomo ufanisi
kazini utakuwa juu.
Utajisikiaje unampa maelekezo mfanyakazi wako jinsi ya
kufanya kazi Fulani na akashindwa kufanya kama ulivyomuelekeza kisa hamuelewani
lugha?
2.UWEZO
WA KUTUMIA KOMPYUTA
Hapa tuelewane vizuri, kujua kompyuta
haimaanishi lazima uwe umesomea kozi yake miaka kadhaa chuo labda kama kazi
unayoomba inahusiana moja kwa moja na uweledi wa kompyuta kwa kusomea kozi
husika. Ila kama unaomba kazi ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na masomo
ya kompyuta, nataka nikwambie haimaanishi ndo usijue kitu kuhusu kompyuta.
Dunia hii ya utandawazi kila kazi kwa namna moja ama nyingine ili kuikamilisha lazima
kompyuta itaingia kati sasa kama hujui kuitumia kabisa utakuwa unajipunguzia
soko. Mathalani uweze kutuma barua pepe (E-mail), programu ya maandishi
(Microsoft word) na program ya namba na maandishi (Microsoft Excel)
3.UWEZO
WA KUBADILIKA/KUFANYA KAZI ZAIDI YA MOJA
Katika dunia hii ambayo ukuaji wa
teknolojia na ushindani wa huduma na bidhaa umekuwa mkubwa ofisi nyingi
hupunguza gharama kwa kuajiri watu wachache wenye uwezo wa kufanya kazi Zaidi
ya moja ili gharama za kuzalisha ziwe ndogo na wao waweze kushusha bei
kupunguza ushindani na kuliteka soko.
Hivyo ukiwa na sifa ya uelewa wa kazi
Zaidi ya moja utajiongezea nafasi katika soko la ajira.
4.UWEZO
WA KUCHANGANYIKA NA WENGINE
Katika mazingira ya ofisi ambayo
binadamu Zaidi ya mmoja wanashirikiana kufanikisha lengo moja la ofisi, uwezo wa mfanyakazi mmoja
kuchangamana na mwengine bila tatizo ni jambo la muhimu sana.
Ofisi inaweza
kuruhusu mtofautiane kwa hoja ili kupata kitu kizuri lakini si kugombana sababu
wazo la mmoja limepingwa na wengi na kuwanunia, hii italeta utengano na
kushusha ufanisi mahali.
Ukiwa na uwezo wa kuchangamana na wengine mathalani
katika wasifu wako ukaweza kuonyesha kwamba uliwahi kufanya kazi na watu Fulani
na kufanikisha jambo Fulani.
5.UWEZO
WA KUONGOZA
Sehemu yoyote ambayo wanakutana watu
Zaidi ya wawili lazima kuwe na kiongozi na lazima ujue miongoni mwenu lazima
atoke kiongozi.
Waajiri wengi wanapenda mtu mwenye uwezo wa kuongoza sababu
wenye tabia hii huwa na uwezo wa kufanya maamuzi ya kibunifu hivyo wanatarajia
hata wakati wa utendaji wako utakuwa unafanya kwa ubunifu na kuwaongoza wengine
na si kufuata njia zile zile
zilizopitiwa na wengine na hivyo kuongeza ufanisi kazini.
HAUJACHELEWA KUFANYA MAREKEBISHO PALE AMBAPO UNAONA UNA MAPUNGUFU ILI KUONGEZA UWEZO WAKO WA KUAJIRIKA KATIKA SOKO LA USHINDANI WA AJIRA.
HAKUNA ALIYEZALIWA NA SIFA ZOTE HIZO BALI WENGINE WAMEZITENGENEZA NA WAKAWEZA KUZIFANYA KUWA SEHEMU YA MAISHA YAO NA MATOKEO MAZURI WAKAYAPATA.
ANZA SASA KUPIGA HATUA...
1 comments:
Nakubaliana na wewe. Ila labda ungekwenda mbali zaidi. Stadi za kazi zipo takribani 60. kwa kiingereza zinaitwa soft skills. Hizi hazifundishwi shuleni. Watu wote, na hata wale ambao sio waajiriwa wanatakiwa kujifunza na kuzifanyia mazoezi. Stadi yeyote hata zile zinazoitwa hard skills, lazima mtu ajufunze halfu aziafanyie mazoezi (practice). Tupo pamoja.
Post a Comment