“Usimamizi wa ubora, usalama, hadhi, mahusiano,
ushirikiano, na sera ya ofisi ni mambo muhimu ya kumfanya mfanyakazi aridhike
na mazingira yake ya kazi”
Mwisho wa kunukuu maneno ya msomi wa enzi hizo ndugu
Fredrick Herzeberg, ambaye alikuja kumwagia zege nadharia iliyofanyiwa utafiti
mwaka 1927 mpaka 1932 na Profesa Elton Mayo.
Profesa alifanya utafiti wa kuchunguza mazingira ya
kazi na tija, pindi alipoona mfumo wa kuwaweka watu wengi wenye historia
tofauti katika eneo moja la kazi.
Alisisitiza kuwa mahusiano mazuri kazini
huongeza tija ya kazi, kwani utendaji wa kila siku wa wafanyakazi unategemea
sana mahusiano baina yao.
ONYESHA
MTAZAMO CHANYA
Kuna kampeni ya usafi Dar es Salaam
ina msemo usemao “Usijifanye mstaarabu bali kuwa mstaarabu”. Hata katika
mtazamo pia unapaswa usijifanye una mtazamo chanya bali waoneshe wenzako kwa
vitendo kuwa wewe una mtazamo chanya.
Mathalani mfanyakazi mwenzako
amekumbana na tatizo katika utendaji wake na anaonyesha kuchanganyikiwa ila
wewe ukawa mtuliza dhoruba kwa kuwa chanya na tatizo lake na kumpa njia mbadala
za kutoka.
Nakwambia ukiwa hivi utakuwa
unawavutia wenzako kuja kwako pindi wanapokumbana na changamoto.
ONYESHA
SURA YA FURAHA KILA UTAPOTOA SALAMU
Unawezaje kuingia ofisini macho
chini, umeshusha mabega, bila hata ya kutoa salamu na unaenda moja kwa moja
kuanza kazi?
Kama hii ndio tabia yako, utaendelea
kuwaona wafanyakazi wenzako wakikuchunia au hata kukukwepa kila wakikuona.
Kuwa na tabia ya kutoa salamu kila unapokutana na
wafanyakazi wenzako huku ukionyesha uso wa furaha, hii itawapa ishara wenzako
kuwa unafuraha kuwa nao eneo moja la kazi.
JIBU
BARUA PEPE NA UJUMBE WA SIMU KWA WAKATI
Utajisikiaje pale ambapo
umemtumia mtu ujumbe uwe wa barua pepe au ujumbe wa kawaida wa simu na
anachukua muda mrefu kukujibu au asijibu kabisa?
Hii itaonyesha una dharau
kwa wenzako, na kwamba wao hawana umuhimu kwako. Jenga tabia ya ukarimu wa
kujibu ujumbe wa mtu kwa wakati, hii itakufanya uonekane unajali na itawapa
urahisi wao kukushirikisha taarifa muhimu kwa wakati.
KUBALI
UTANI ENEO LA KAZI
Simaanishi ukubali kila utani
utakaotaniwa hata ule unaovuka mipaka, bali ule utani ambao ni wa kawaida
usiovuka mipaka upalilie ili uwafanye wenzako wafurahie uwepo wako kwani
dhumuni kubwa la utani ni kufurahi pamoja.
Usishangae mtu huna hata mazoea nae
ila akaanza kukutania, hii ina maanisha anataka kupata picha wewe ni mtu wa
namna gani. Hasa ukizingatia kuwa ishazoeleka kuwa mtu wa utani ni rahisi
kuingilika kwa maongezi na si mtu wa kukasirika hovyo.
TENGENEZA
UAMINIFU
Unapokutana na wengine eneo la kazi
hakuna anayejua kuwa wewe ni muaminifu mpaka utakapofanya tendo la uaminifu
mbele yao. Hata siku moja mtu asikwambie kuwa yeye si mwizi kama eneo au mazingira
anayoishi hakuna cha kuiba.
Vivyo hivyo huwezi kuwaambia watu wewe ni muaminifu
na mkweli kama haujawahi kuonyesha mbele yao tukio la uaminifu na ukweli.
Mathalani endapo umekosea jambo
Fulani na ukakubali na kukiri mbele ya wenzako, hii itawajengea picha kuwa wewe
ni muaminifu na msema kweli.
KUWA
MTU WA KUTOA MSAADA KWA WENZAKO
Kutoa msaada wa maarifa na utaalamu
katika eneo la nje ya muongozo wako wa kazi ni msaada tosha kwa mfanayakazi
mwenzako mwenye kuhitaji msaada wako.
Kwa mfano wewe unafahamu kutengeneza
kitu Fulani ambacho mfanyakazi mwenzako unamuona kimemuharibikia na anashindwa
kukitengeneza, ukijitokeza kumsaidia utakuwa umeimarisha uhusiano wako na yeye
na atakuona ni mtu mzuri kuishi nae eneo moja la kazi.
HESHIMU
TOFAUTI ZA UTAMADUNI KATI YAKO NA WENZAKO
Mazingira ya kazi katika zama hizi
yameendelea kuwaleta pamoja watu wenye historia tofauti, kuanzia malezi mpaka
jamii wanazotokea.
Jinsi wewe unavyokuwa unatumia muda
wako na kiwango cha umakini lazima kitatofautiana na wenzako.
Usiwe mtu wa kujilinganisha na
kuwaona wenzako ni watu wa ajabu kwakuwa hawapo kama wewe, bali fungua masikio
na macho yako kujifunza kitu kutoka kwao ambacho wewe huwezi kukifanya kama
wao.
Unapokuwa mtu wa kuheshimu tofauti
zako na za wengine, utawafanya na wao watamani kujifunza kitu kutoka kwako,
hivyo kuimarisha mahusiano yenu eneo la kazi.
KUWA
NA HESHIMA KWA WOTE
Kama unadhani heshima ni kuamkia
wakubwa tu hasa wale unaofanya nao kazi, basi nakuomba utafakari upya. Heshima
ni nguzo muhimu sana katika kujenga mahusiano bora eneo la kazi.
Kumheshimu
mwenzako ni pamoja na kujua mipaka ya kauli na maneno ya kuongea mbele yake
hata kama umemzidi cheo au umri.
Ukiwa na heshima kwa wengine
itakusaidia usiwe miongoni mwa watu wanaopenda kujadili watu wengine kwa mabaya.
Ukiwaonyesha heshima watavutika kuja kwako na mahusiano yenu yataimarika.
SHIRIKIANA
NA WENZAKO KATIKA VITU WANAVYOPENDA
Muulize mfanyakazi mwenzako kuhusu
vitu anavyopenda kufanya, aina ya muziki anaosikiliza, filamu amazoangalia, na
hata vitabu anavyosoma.
Baada ya kufahamu angalia chochote ambacho mnaendana
shirikiana nae, kwa mfano umegundua anapenda sana kuangalia mpira sio mbaya
kama ukijiunga nae kama na wewe ni muangaliaji pia.
SHIRIKI MITOKO NA WENZAKO
Kufahamiana na wafanyakazi wenzako nje
ya eneo la kazi ni jambo zuri sana. Ndio maana ofisi nyingi lazima utakuwa kila
baada ya muda Fulani wanaandaa tafrija ya kuwakutanisha wafanyakazi katika
bonanza ili kujenga mahusiano mazuri baina yao.
Hata kama ofisi haiandai matukio kama
hayo ila sio mbaya kama utakuwa unatumia muda wako japo kidogo kutoka na kwenda
mahali na wenzako kupata vinywaji au chakula nje ya muda wa kazi ili kuboresha
mahusiano mazuri.
0 comments:
Post a Comment