UNAWEZA KUFANYA NINI PALE UNAPOGUNDUA UMEFANYA KOSA KATIKA ENEO LAKO LA KAZI?

“Hakuna binadamu mkamilifu”, huu msemo hatujaanza kuusikia leo, ila ni wachache kati yetu tunaoweza kuupa maana yake kamili pale ambapo kuna kosa limefanyika iwe na mtu mwengine au sisi wenyewe. Ukiwa unajua kuupa maana msemo huu hautakuwa mgumu kusamehe au kujisamehe na kutafuta njia mbadala za kutatua hilo tatizo kwa kuwa unatambua wazi binadamu hatuwezi kufanya jambo sahihi kila siku.
Wote ni mashahidi tulipokuwa tunaangalia mashindano ya Copa Amerika Lionel Messi katika hatua za awali alijituma sana kuifikisha nchi yake fainali na wote walimwona shujaa, lakini siku ya mwisho alikosa penati iliyowafanya kukosa kombe. 

Wote tunajua maamuzi aliyochukua baada ya mechi, alitangaza kujiuzulu kwani alikosa msamaha kwake mwenyewe kwakuwa alijihisi alipaswa kuwa mkamilifu kwa kuwa anajua watu wanamwona kama mtu asiyekosea. Kukosea tumeumbiwa wanadamu, na mara nyingi tunapogundua tumekosea katika eneo letu la kazi, tunajikuta tunaingia hatia mioyoni mwetu na hatujui tunaweza kumudu vipi hali hiyo. 

 KUBALI KOSA LAKO, NA MSHIRIKISHE MTU ANAYESTAHILI KUAMBIWA
Kama upo eneo la kazi na umefanya kosa, ni lazima kuna watu wataathirika na tukio lako. Jinsi unavyochukua muda mrefu kuelezea ulichokosea kwa litakaye mwathiri, ndivyo litakavyochukua muda mrefu kurekebisha makossa uliyofanya. Inaogofya kukubali kuchukua lawama za makosa uliyotenda, hasa ukizingatia unajua wazi kuna mtu atakukasirikia baada ya kusema ukweli, lakini nakwambia ni bora kulamba ncha ya kisu na kusema mapema kuliko kusubiri madhara yawe makubwa.

 Kama unajiona unaweza kurekebisha vitu wewe mwenyewe, bila kusimamiwa wala kuelekezwa na mtu, haitakuumiza kujaribu mwenyewe, ila ikitokea umekosea usiache kuomba msaada na si kujipa moyo kwamba utaweza kurekebisha kimya kimya. Watu wenye tabia ya kurekebisha makosa kimya kimya bila kumshirikisha mtu mwengine, hujitahidi kwa bidi zote ili kuficha aibu ya kuonekana wamekosea.
Ukweli ni kwamba kosa ulilofanya unaweza kuliona dogo, lakini kumbe jinsi unavyoliweka kimya huku hupati suluhisho la haraka linakuwa kubwa lisilorekebishika kuliko ulivyotarajia. 

Katika mahojiano na chuo cha biashara cha Harvard, mwenyekiti wa kampuni ya Toyota Katsuaki Watanabe alielezea kwanini ni vyema kuweka wazi tatizo: “Tatizo lililofichwa ndio huja kuwa janga kubwa. Kama tatizo likiwekwa wazi kila mtu akalitambua, najisikia salama. Hii ni kwasababu tatizo linapowekwa katika lugha ya picha, hata kama watu wetu hawakulitanbua tangu mapema, watazisumbua akili zao kutafuta suluhisho.


” Unapoenda kumwelezea mkuu wako wa kazi kilichotokea, ukweli ni sera bora kuliko zote. Achana na udhuru wa kutaka kuwaangushia wengine tatizo lako ili muathirike wote bali kubali kulibeba mwenyewe na ueleze ukweli wa kilichotokea. Kama kuna kazi ulipewa na ukasahau kuifanya kwa wakati, mweleze mkuu wako na kama una sababu ya maana ya kwanini haukufanya weka wazi. 


Kama ulipewa kazi na wakati unaifanya haikwenda sawa, usiogope kama ulijitahidi kutumia nguvu na akili yako kutimiza wajibu wako. Usiache tatizo kubwa liwe kubwa Zaidi kwa kujifanya hakuna kilichotokea. Hakikisha unaonyesha na hata kuwaomba msamaha wale wote walioathirika na makosa yako. Ulichokifanya sio kwamba umedhamilia kwajili ya kumuumiza mtu,bali unatakiwa kuchukua mzigo wote wa lawama na na kuomba radhi mwisho wa siku. 

  LETA SULUHISHO MBADALA LA KUTATUA TATIZO
Nadhani hautapenda uwe mtu anayeleta matatizo katika eneo lako la kazi pasipo kuleta suluhisho,haijalishi hilo tatizo limeletwa na wewe au mtu mwengine.Unapokuwa umekosea jambo Fulani na ukajitahidi uwe na na njia chache za suluhisho tayari kichwani hii itakusaidia kupunguza ukubwa wa nyundo zitakazokushukia.


Katika mazingira ya siku hizi ya kazi, kama unataka kuwa mfanyakazi mwenye kuthaminiwa, usliwe mleta matatizo kwa meneja wako bali leta suluhisho. Unajua kwanini? Kwasababu kuna matatizo mengi meneja anatakiwa kutatua wenyewe, sasa hutakiwi kuwa sehemu ya tatizo.
Njoo na njia lukuki za kutatua makosa yako, na chagua moja unalohisi ndio sahihi kabisa. Weka katika maandishi kabisa kama kuna ulazima na uwe na majibu tayari kwaajili ya maswali utakayoulizwa na meneja wako. 

Mpe muhtasari meneja wako wa hilo suluhisho lako sahihi lakini pia uwe na masuluhisho mengine karibu ikiwa meneja wako hajakubaliana na suluhisho lako la kwanza.Ndio yawezekana kabisa umezamisha meli lakini haimaanishi usionyeshe juhudi za kuiokoa mbele ya meneja wako. Unaweza kutafunwa kama bazooka, lakini utakuwa sehemu salama kwa kuwa umeonyesha juhudi za kuokoa jahazi baada ya kukosea. 

  JISAMEHE MWENYEWE NA JIFUNZE KUPITIA MAKOSA
Kuyakabili makosa yako ni jambo gumu, lakini ni muhimu kujisamehe mwenyewe punde tu unapokuwa umekosea.Umekosea kweli, lakini sio kitu cha ajabu kila binadamu huwa anakosea kwa nafasi yake. Ufanye msamaha kuwa sehemu ya maisha yako kila siku,na unapojikuta umefanya kosa kubwa, jitahidi kufikiria namna ya kutatua tatizo badala ya kukaa kujilaumu kila wakati.

Wewe sio mtu wa kwanza kufanya kosa kubwa kama hilo, jaribu kufuatilia watu ambao unao waangalia kama mfano kwako na uwadadisi na utagundua kumbe makossa ni sehemu ya binadamu katika kufikia mambo mazuri na kuwa yote waliyopitia ni sehemu ya mchakato. 
  TENGENEZA UAMINIFU TENA KWA MENEJA WAKO
Baada ya kufanya kosa kubwa na meneja wako akaligundua hutakiwi kufikiria kuacha kazi badala yake jitahidi uonyeshe kwamba haujarudishwa nyuma na kosa lile bali una nafasi ya kufanya tena jambo linguine kwa usahihi. 


Anza kujenga uaminifu tena kwa mambo madogo madogo na sio ushikwe na munkari utake kuonyesha umahiri katika mambo makubwa ambayo huna uzoefu nayo na yanaweza kukurudisha tena katika kukosea.

Share this post:

Digg it StumbleUpon del.icio.us Google Yahoo! reddit

0 comments:

Post a Comment

 
Copyright 2013-2017 Lisha Ubongo
| Branded by www.pixelbase.co.tz