Muziki uko kila mahali tunapoenda,
iwe umeusikia kupitia redio, 
katika mgahawa, nyumba za ibada au katika maeneo ya starehe.
Hakuna utafiti wowote uliowahi kufanywa ambao uliweza kuthibitisha madhara yanayotokana na mtu kusikiliza muziki,
ila tafiti nyingi zimeegemea katika kutoa faida za muziki katika maisha yetu ya kila siku.
Haijalishi aina gani ya muziki unaipenda sana kusikiliza ilimradi unaupenda utakusaidia kitu tu.

Hebu tuangalie faida japo chache ambazo zinaletwa na kusikiliza muziki.

1.KUTUNZA KUMBUKUMBU

Haijalishi sasa hivi una umri gani lakini kila mara kuna wimbo ukiusikia lazima utakukumbusha matukio yaliyopita ambapo wakati unapitia kipindi hicho wimbo huo ndio ulikuwa unapigwa.
Na utajikuta unaanza kufurahi na kuzidi kuziimarisha kumbukumbu zako za matukio ya zamani.
Si kitu cha ajabu kumsikia mtu akisikia wimbo fulani unaanza kusema "Aah! wimbo wangu huo!" 

2.KUIMARISHA UMAKINI

Ukiwa ni msikilizaji mzuri wa nyimbo mara nyingi unatengeneza tabia ya kusikiliza wimbo kuanzia mashairi hadi midundo yake na hii si kazi rahisi hata kidogo kwani unatakiwa umakini wa hali ya juu kufanya jambo hili.
Cha ajabu utamkuta mtu anaupenda wimbo lakini hajui hata mashairi yanazungumzia nini,
 tabia itakufanya hata uwezo wako wa kusikiliza mtu anapoongea uwe mdogo kwani kitendo cha kusikiliza na kutafsiri papo kwa papo kina umuhimu sana katika ulimwengu wa kujifunza.

3.HULETA HISIA ZA UTULIVU

Muziki sio lazima uwe na midundo,
lakini hata mashairi tupu yanaweza kukuletea utulivu unaoufanya ubongo upumzike vizuri.
Na ndio maana unapomuimbia mtoto mdogo hachelewi kulala.
Na watu wazima mara nyingi husinzia na kupumzika haraka wanaposiliza nyimbo za taratibu kwani ndizo ambazo zinaupa ubongo hisia nzuri kwa muda huo.

4.HUONGEZA NGUVU WAKATI WA SHUGHULI

Mathalani unapokuwa unafanya shughuli fulani ambayo ni kutumia nguvu nyingi muziki husaidia kuongeza utendaji kazi wako muda huo.
Na ndio maana hata washauri wa mazoezi wanapenda kuwaeleza wateja wao wanapofanya mazoezi ya kukimbia au yoyote ya kutumia viungo ni vyema wakaweka muziki ambao utakuwa unawasindikiza ili wasichoke haraka.

5.UNAONGEZA MANENO

Hata kama wewe ni mtumiaji mzuri wa lugha yako  lakini kuna maneno unaweza ukawa hujawahi hata kuyatumia katika maisha yako.
Sasa unapokuwa msikilizaji mzuri wa mashairi ya nyimboi inakusaidia kuongeza maneno na maana zake.

6.CHANGAMOTO ZA UWEZO WA KUHOJI

Muziki mara zote kama unausikiliza kwa makini unakuletea changamoto za kujiuliza kama kinachoimbwa ni sawa au sio sawa.
Na kitu pekee kitakachokupa uwezo wa kutambua hilo ni uwezo wako wa kuhoji mashairi kutokana na tafsiri yako uliyopata.
Na ndio maana sitashangaa kumkuta mtu anaimba mashairi ya lugha yake lakini hajui hata aliyeimba alikuwa ana maanisha nini.

7.KUTIA HAMASA

Mara kwa mara si kitu cha ajabu kukuta unasikiliza wimbo ambao mashairi yake yanakugusa moja kwa moja,
na bahati nzuri anatoa na suluhisho la tatizo humo humo.
Na hali hiyo itakufanya ujione hauko peke yako mwenye hisia kama hizo hivyo kukutia hamasa ya kusonga kusonga mbele.
Na ndio maana kuna nyimbo kuzisahau kwako inakuwa ni ndoto kwani katika kipindi fulani cha maisha yako ulikugusa kiukweli.

8.HUONGEZA UBUNIFU

Muziki wenyewe tu ni kazi ya ubunifu kuanzia melodi ya mashairi hadi midundo yake.
Japo si kila msikilizaji wa muziki anaweza kuja kuwa msanii lakini utafiti unaonyesha watu wengi waliokuja kuwa wasanii wa muziki walikuwa wasilikzaji wazuri wa muziki.
Hata watu wengine wanaofanya kazi nyingine za sanaa wanatumia muziki kama chombo moja wapo cha kuwaongezea ubunifu kwa mfano waandishi, wachoraji, wachezaji au wanaofanya kazi za kutumia umakini mkubwa wa ubongo.

9.HUBADILISHA HALI YA UBONGO

Muziki unaweza ukakusaidia kubadilisha hali unayojisikia iwe ya huzuni, mawazo, upweke, hofu au hata hasira.
Na ndio maana wataalamu wanashauri ikiwa uko na hali mojawapo nilizozitaja hapo juu uwe unatumia njia ya kuimba nyimbo unazozipenda kukurudisha katika hali yako ya kawaida.

10.HUONGEZA UFANISI WA KAZI

Haijalishi kazi gani unayofanya,
ukimya utakufanya akili yako ihamie kwingine ambako utaufanya ubongo upoteze umakini na shughuli unayofanya muda huo.
Ila kwa kutumia aina ya muziki unaoupenda utaifanya akili ijisikie vizuri na hata kuzuia kuchoka haraka.

NAJUA KUNA WATU SI WAPENZI WA KUSIKILIZA MUZIKI KABISA.

NA MAKALA HII HAIPO KWA AJILI YA KUKUSHAWISHI UANZE TABIA AMBAYO HUKUWAHI KUWA NAYO KABLA ILA IPO KWA AJILI YA WALE WAPENZI WA MUZIKI ILI WAUTUMIE MUZIKI HUO KATIKA KUBORESHA SHUGHULI ZAO.

Share this post:

Digg it StumbleUpon del.icio.us Google Yahoo! reddit

0 comments:

Post a Comment

 
Copyright 2013-2017 Lisha Ubongo
| Branded by www.pixelbase.co.tz