“Usimamizi wa ubora, usalama, hadhi, mahusiano,
ushirikiano, na sera ya ofisi ni mambo muhimu ya kumfanya mfanyakazi aridhike
na mazingira yake ya kazi”
Mwisho wa kunukuu maneno ya msomi wa enzi hizo ndugu
Fredrick Herzeberg, ambaye alikuja kumwagia zege nadharia iliyofanyiwa utafiti
mwaka 1927 mpaka 1932 na Profesa Elton Mayo.
Profesa alifanya utafiti wa kuchunguza mazingira ya
kazi na tija, pindi alipoona mfumo wa kuwaweka watu wengi wenye historia
tofauti katika eneo moja la kazi.
Alisisitiza kuwa mahusiano mazuri kazini
huongeza tija ya kazi, kwani utendaji wa kila siku wa wafanyakazi unategemea
sana mahusiano baina yao.
ONYESHA
MTAZAMO CHANYA
Kuna kampeni ya usafi Dar es Salaam
ina msemo usemao “Usijifanye mstaarabu bali kuwa mstaarabu”. Hata katika
mtazamo pia unapaswa usijifanye una mtazamo chanya bali waoneshe wenzako kwa
vitendo kuwa wewe una mtazamo chanya.
Mathalani mfanyakazi mwenzako
amekumbana na tatizo katika utendaji wake na anaonyesha kuchanganyikiwa ila
wewe ukawa mtuliza dhoruba kwa kuwa chanya na tatizo lake na kumpa njia mbadala
za kutoka.
Nakwambia ukiwa hivi utakuwa
unawavutia wenzako kuja kwako pindi wanapokumbana na changamoto.
ONYESHA
SURA YA FURAHA KILA UTAPOTOA SALAMU
Unawezaje kuingia ofisini macho
chini, umeshusha mabega, bila hata ya kutoa salamu na unaenda moja kwa moja
kuanza kazi?
Kama hii ndio tabia yako, utaendelea
kuwaona wafanyakazi wenzako wakikuchunia au hata kukukwepa kila wakikuona.
Kuwa na tabia ya kutoa salamu kila unapokutana na
wafanyakazi wenzako huku ukionyesha uso wa furaha, hii itawapa ishara wenzako
kuwa unafuraha kuwa nao eneo moja la kazi.
JIBU
BARUA PEPE NA UJUMBE WA SIMU KWA WAKATI
Utajisikiaje pale ambapo
umemtumia mtu ujumbe uwe wa barua pepe au ujumbe wa kawaida wa simu na
anachukua muda mrefu kukujibu au asijibu kabisa?
Hii itaonyesha una dharau
kwa wenzako, na kwamba wao hawana umuhimu kwako. Jenga tabia ya ukarimu wa
kujibu ujumbe wa mtu kwa wakati, hii itakufanya uonekane unajali na itawapa
urahisi wao kukushirikisha taarifa muhimu kwa wakati.
KUBALI
UTANI ENEO LA KAZI
Simaanishi ukubali kila utani
utakaotaniwa hata ule unaovuka mipaka, bali ule utani ambao ni wa kawaida
usiovuka mipaka upalilie ili uwafanye wenzako wafurahie uwepo wako kwani
dhumuni kubwa la utani ni kufurahi pamoja.
Usishangae mtu huna hata mazoea nae
ila akaanza kukutania, hii ina maanisha anataka kupata picha wewe ni mtu wa
namna gani. Hasa ukizingatia kuwa ishazoeleka kuwa mtu wa utani ni rahisi
kuingilika kwa maongezi na si mtu wa kukasirika hovyo.
TENGENEZA
UAMINIFU
Unapokutana na wengine eneo la kazi
hakuna anayejua kuwa wewe ni muaminifu mpaka utakapofanya tendo la uaminifu
mbele yao. Hata siku moja mtu asikwambie kuwa yeye si mwizi kama eneo au mazingira
anayoishi hakuna cha kuiba.
Vivyo hivyo huwezi kuwaambia watu wewe ni muaminifu
na mkweli kama haujawahi kuonyesha mbele yao tukio la uaminifu na ukweli.
Mathalani endapo umekosea jambo
Fulani na ukakubali na kukiri mbele ya wenzako, hii itawajengea picha kuwa wewe
ni muaminifu na msema kweli.
KUWA
MTU WA KUTOA MSAADA KWA WENZAKO
Kutoa msaada wa maarifa na utaalamu
katika eneo la nje ya muongozo wako wa kazi ni msaada tosha kwa mfanayakazi
mwenzako mwenye kuhitaji msaada wako.
Kwa mfano wewe unafahamu kutengeneza
kitu Fulani ambacho mfanyakazi mwenzako unamuona kimemuharibikia na anashindwa
kukitengeneza, ukijitokeza kumsaidia utakuwa umeimarisha uhusiano wako na yeye
na atakuona ni mtu mzuri kuishi nae eneo moja la kazi.
HESHIMU
TOFAUTI ZA UTAMADUNI KATI YAKO NA WENZAKO
Mazingira ya kazi katika zama hizi
yameendelea kuwaleta pamoja watu wenye historia tofauti, kuanzia malezi mpaka
jamii wanazotokea.
Jinsi wewe unavyokuwa unatumia muda
wako na kiwango cha umakini lazima kitatofautiana na wenzako.
Usiwe mtu wa kujilinganisha na
kuwaona wenzako ni watu wa ajabu kwakuwa hawapo kama wewe, bali fungua masikio
na macho yako kujifunza kitu kutoka kwao ambacho wewe huwezi kukifanya kama
wao.
Unapokuwa mtu wa kuheshimu tofauti
zako na za wengine, utawafanya na wao watamani kujifunza kitu kutoka kwako,
hivyo kuimarisha mahusiano yenu eneo la kazi.
KUWA
NA HESHIMA KWA WOTE
Kama unadhani heshima ni kuamkia
wakubwa tu hasa wale unaofanya nao kazi, basi nakuomba utafakari upya. Heshima
ni nguzo muhimu sana katika kujenga mahusiano bora eneo la kazi.
Kumheshimu
mwenzako ni pamoja na kujua mipaka ya kauli na maneno ya kuongea mbele yake
hata kama umemzidi cheo au umri.
Ukiwa na heshima kwa wengine
itakusaidia usiwe miongoni mwa watu wanaopenda kujadili watu wengine kwa mabaya.
Ukiwaonyesha heshima watavutika kuja kwako na mahusiano yenu yataimarika.
SHIRIKIANA
NA WENZAKO KATIKA VITU WANAVYOPENDA
Muulize mfanyakazi mwenzako kuhusu
vitu anavyopenda kufanya, aina ya muziki anaosikiliza, filamu amazoangalia, na
hata vitabu anavyosoma.
Baada ya kufahamu angalia chochote ambacho mnaendana
shirikiana nae, kwa mfano umegundua anapenda sana kuangalia mpira sio mbaya
kama ukijiunga nae kama na wewe ni muangaliaji pia.
SHIRIKI MITOKO NA WENZAKO
Kufahamiana na wafanyakazi wenzako nje
ya eneo la kazi ni jambo zuri sana. Ndio maana ofisi nyingi lazima utakuwa kila
baada ya muda Fulani wanaandaa tafrija ya kuwakutanisha wafanyakazi katika
bonanza ili kujenga mahusiano mazuri baina yao.
Hata kama ofisi haiandai matukio kama
hayo ila sio mbaya kama utakuwa unatumia muda wako japo kidogo kutoka na kwenda
mahali na wenzako kupata vinywaji au chakula nje ya muda wa kazi ili kuboresha
mahusiano mazuri.
Je, unajua waajiri wakati mwingine hulipa kiwango kikubwa
Cha mshahara kwa kuwa mwajiriwa ana elimu sahihi na uzoefu? Je, unaweza kuwa na
uwezo wa kupata mshahara mkubwa kwa kufanya kazi moja katika kampuni kubwa? Ni
dhahiri, hivi vinaweza kuwa baadhi ya vitu vya nguvu katika mazungumzo wakati wa
mapitio ya utendaji wako, usaili wa
kazi, au ombi kwa ajili ya kupandishwa cheo.
Waajiri kawaida hurekebisha taarifa za malipo wakati wa
kuamua kiasi gani cha kumlipa mfanyakazi wa kufanya kazi maalumu. Baada ya wao
kuamua thamani ya nafasi kwa kutafiti taarifa juu ya viwango vya malipo kwa
ajili ya kazi hiyo kulinganishwa katika makampuni mengine yanayofanya shughuli
sawa na wao, ila watakubali kubadilisha kwa kuzingatia elimu na uzoefu wa
mwombaji.
Miaka ya uzoefu
Kwa kawaida, ukiwa na uzoefu zaidi huchangia kulipwa kiwango
cha juu cha mshahara. Vile vile, kama nafasi imetangazwa na anahitajika mtu
mwenye uzoefu wa miaka 10 katika kazi fulani, na wewe huna wala haukidhi
mahitaji hayo, ukibahatika ukapata hiyo kazi tambua lazima utalipwa kiwango
kidogo.
Elimu
Uwiano kati ya elimu yako na kiwango kinachohitajika kwa
ajili ya kazi kwa kawaida huathiri mshahara utakaolipwa. Pia, ubora wa elimu
unaweza kuathiri mshahara. Kupata shahada kutoka katika kozi inayoheshimika,
kawaida ina ushawishi chanya juu ya kulipwa kwako, wakati kupata shahada kutoka
katika chuo ambacho huchukuliwa dhaifu hupunguza uwezo wako wa kupata mshahara
mkubwa.
Utendaji wa kitaalamu
Tangu kitambo waajiri wengi hutumia msingi wa maamuzi yao
kulipa mshahara angalau kwa kiwango cha juu kwa kuzingatia utendaji wa mtu
binafsi, hiki ndio kipimo cha kutofautisha
viwango vya mshahara wakati wa kutaka kuongeza mshahara au cheo. Hata
wakati unapoomba kazi mpya, habari hii inaweza kuwa muhimu kwa mwajiri wako,
kwani inatoa picha kamili juu ya uwezo wako.
Mkuu wako wa kazi
Mchango wako na uhusiano wako wa kiutendaji katika mafanikio
ya kampuni yako, endapo mkuu wako wa kitengo cha kazi ana nafasi kubwa katika
maamuzi ya kampuni, mapendekezo yake kuhusiana na malipo yako yana nafasi
kidogo ya kupingwa wakati wa mapitio.
Idadi ya wanaoripoti kwako
Jinsi unavyokuwa na idadi ya wafanyakazi wengi wa
kuwasimamia na kuleta ripoti kwako, ndivyo utakavyoweza kulipwa kiwango cha juu
katika kazi fulani. Bila shaka, ngazi yako ya mafanikio inategemea msingi wa
utendaji wa wafanyakazi ambao unawasimamia.
Kutunukiwa na vyama
vya Kitaalamu
Vyeti na uanachama katika bodi za kitaalamu au vyama
vya biashara unaweza kuwa chagizo chanya kuathiri juu ya kulipwa kwako kwa kiwango
cha juu. Hata hivyo, kama kazi uliyopata na hauna vyeti vinavyohitajika, kulipwa
kwako lazima kuanzie kiwango kidogo. Baadhi ya waajiri wanahimiza wafanyakazi
wao watafute vyeti vyenye vigezo.
Tofauti ya zamu
Katika kazi fulani, wafanyakazi wanaweza kutarajiwa kufanya
kazi katika nyakati ambazo si muda ambao ni mzuri na unaopendwa na wengi.
Wafanyakazi wa nyakati hizi ni kawaida kulipwa kiwango cha juu kutokana na
gharama kubwa za kijamii na kimwili kushiriki katika kufanya kazi nje ya
"masaa ya kawaida ya kazi." Katika kazi ambazo hakuna zamu za kuingia
kazini, tofauti ya malipo ni kidogo.
“Hakuna binadamu mkamilifu”, huu msemo hatujaanza kuusikia leo, ila ni wachache kati yetu tunaoweza kuupa maana yake kamili pale ambapo kuna kosa limefanyika iwe na mtu mwengine au sisi wenyewe. Ukiwa unajua kuupa maana msemo huu hautakuwa mgumu kusamehe au kujisamehe na kutafuta njia mbadala za kutatua hilo tatizo kwa kuwa unatambua wazi binadamu hatuwezi kufanya jambo sahihi kila siku.
Wote ni mashahidi tulipokuwa tunaangalia mashindano ya Copa Amerika Lionel Messi katika hatua za awali alijituma sana kuifikisha nchi yake fainali na wote walimwona shujaa, lakini siku ya mwisho alikosa penati iliyowafanya kukosa kombe.
Wote tunajua maamuzi aliyochukua baada ya mechi, alitangaza kujiuzulu kwani alikosa msamaha kwake mwenyewe kwakuwa alijihisi alipaswa kuwa mkamilifu kwa kuwa anajua watu wanamwona kama mtu asiyekosea.
Kukosea tumeumbiwa wanadamu, na mara nyingi tunapogundua tumekosea katika eneo letu la kazi, tunajikuta tunaingia hatia mioyoni mwetu na hatujui tunaweza kumudu vipi hali hiyo.
KUBALI KOSA LAKO, NA MSHIRIKISHE MTU ANAYESTAHILI KUAMBIWA
Kama upo eneo la kazi na umefanya kosa, ni lazima kuna watu wataathirika na tukio lako. Jinsi unavyochukua muda mrefu kuelezea ulichokosea kwa litakaye mwathiri, ndivyo litakavyochukua muda mrefu kurekebisha makossa uliyofanya. Inaogofya kukubali kuchukua lawama za makosa uliyotenda, hasa ukizingatia unajua wazi kuna mtu atakukasirikia baada ya kusema ukweli, lakini nakwambia ni bora kulamba ncha ya kisu na kusema mapema kuliko kusubiri madhara yawe makubwa.
Kama unajiona unaweza kurekebisha vitu wewe mwenyewe, bila kusimamiwa wala kuelekezwa na mtu, haitakuumiza kujaribu mwenyewe, ila ikitokea umekosea usiache kuomba msaada na si kujipa moyo kwamba utaweza kurekebisha kimya kimya. Watu wenye tabia ya kurekebisha makosa kimya kimya bila kumshirikisha mtu mwengine, hujitahidi kwa bidi zote ili kuficha aibu ya kuonekana wamekosea.
Ukweli ni kwamba kosa ulilofanya unaweza kuliona dogo, lakini kumbe jinsi unavyoliweka kimya huku hupati suluhisho la haraka linakuwa kubwa lisilorekebishika kuliko ulivyotarajia.
Katika mahojiano na chuo cha biashara cha Harvard, mwenyekiti wa kampuni ya Toyota Katsuaki Watanabe alielezea kwanini ni vyema kuweka wazi tatizo:
“Tatizo lililofichwa ndio huja kuwa janga kubwa. Kama tatizo likiwekwa wazi kila mtu akalitambua, najisikia salama. Hii ni kwasababu tatizo linapowekwa katika lugha ya picha, hata kama watu wetu hawakulitanbua tangu mapema, watazisumbua akili zao kutafuta suluhisho.
”
Unapoenda kumwelezea mkuu wako wa kazi kilichotokea, ukweli ni sera bora kuliko zote. Achana na udhuru wa kutaka kuwaangushia wengine tatizo lako ili muathirike wote bali kubali kulibeba mwenyewe na ueleze ukweli wa kilichotokea.
Kama kuna kazi ulipewa na ukasahau kuifanya kwa wakati, mweleze mkuu wako na kama una sababu ya maana ya kwanini haukufanya weka wazi.
Kama ulipewa kazi na wakati unaifanya haikwenda sawa, usiogope kama ulijitahidi kutumia nguvu na akili yako kutimiza wajibu wako. Usiache tatizo kubwa liwe kubwa Zaidi kwa kujifanya hakuna kilichotokea.
Hakikisha unaonyesha na hata kuwaomba msamaha wale wote walioathirika na makosa yako. Ulichokifanya sio kwamba umedhamilia kwajili ya kumuumiza mtu,bali unatakiwa kuchukua mzigo wote wa lawama na na kuomba radhi mwisho wa siku.
LETA SULUHISHO MBADALA LA KUTATUA TATIZO
Nadhani hautapenda uwe mtu anayeleta matatizo katika eneo lako la kazi pasipo kuleta suluhisho,haijalishi hilo tatizo limeletwa na wewe au mtu mwengine.Unapokuwa umekosea jambo Fulani na ukajitahidi uwe na na njia chache za suluhisho tayari kichwani hii itakusaidia kupunguza ukubwa wa nyundo zitakazokushukia.
Katika mazingira ya siku hizi ya kazi, kama unataka kuwa mfanyakazi mwenye kuthaminiwa, usliwe mleta matatizo kwa meneja wako bali leta suluhisho. Unajua kwanini? Kwasababu kuna matatizo mengi meneja anatakiwa kutatua wenyewe, sasa hutakiwi kuwa sehemu ya tatizo.
Njoo na njia lukuki za kutatua makosa yako, na chagua moja unalohisi ndio sahihi kabisa. Weka katika maandishi kabisa kama kuna ulazima na uwe na majibu tayari kwaajili ya maswali utakayoulizwa na meneja wako.
Mpe muhtasari meneja wako wa hilo suluhisho lako sahihi lakini pia uwe na masuluhisho mengine karibu ikiwa meneja wako hajakubaliana na suluhisho lako la kwanza.Ndio yawezekana kabisa umezamisha meli lakini haimaanishi usionyeshe juhudi za kuiokoa mbele ya meneja wako. Unaweza kutafunwa kama bazooka, lakini utakuwa sehemu salama kwa kuwa umeonyesha juhudi za kuokoa jahazi baada ya kukosea.
JISAMEHE MWENYEWE NA JIFUNZE KUPITIA MAKOSA
Kuyakabili makosa yako ni jambo gumu, lakini ni muhimu kujisamehe mwenyewe punde tu unapokuwa umekosea.Umekosea kweli, lakini sio kitu cha ajabu kila binadamu huwa anakosea kwa nafasi yake.
Ufanye msamaha kuwa sehemu ya maisha yako kila siku,na unapojikuta umefanya kosa kubwa, jitahidi kufikiria namna ya kutatua tatizo badala ya kukaa kujilaumu kila wakati.
Wewe sio mtu wa kwanza kufanya kosa kubwa kama hilo, jaribu kufuatilia watu ambao unao waangalia kama mfano kwako na uwadadisi na utagundua kumbe makossa ni sehemu ya binadamu katika kufikia mambo mazuri na kuwa yote waliyopitia ni sehemu ya mchakato.
TENGENEZA UAMINIFU TENA KWA MENEJA WAKO
Baada ya kufanya kosa kubwa na meneja wako akaligundua hutakiwi kufikiria kuacha kazi badala yake jitahidi uonyeshe kwamba haujarudishwa nyuma na kosa lile bali una nafasi ya kufanya tena jambo linguine kwa usahihi.
Anza kujenga uaminifu tena kwa mambo madogo madogo na sio ushikwe na munkari utake kuonyesha umahiri katika mambo makubwa ambayo huna uzoefu nayo na yanaweza kukurudisha tena katika kukosea.
Subscribe to:
Posts (Atom)