Jiulize, 
viatu ulivyovaa ni siazi yako na kama ndio ni  aina yako?
Miongoni mwetu tunatumia asilimia 75 ya muda wetu kwa siku katika kazi.
Kwahiyo kuwa katika kazi ambayo haikupi faraja inaweza ikakuletea matatizo katika maisha yako ya kila siku.

Umejaribu njia zote kujitahidi kuendana na hali lakini bado unaona wazi kabisa kwamba kuna kitu kinakosekana.
Ni ukweli usiopingika kuwa kazi yoyote ile kwa upande mwingine kuna kipindi inachosha.
Unachopaswa kujiuliza ni je, 
hali hii unayojisikia ni ya muda au ni ya kudumu?
Kama ushawahi kukumbana na hali hiyo au kujiuliza hilo swali basi makala hii inakuhusu.
Sasa utajuaje kama kazi uliyopo sasa ulifanya uamuzi sahihi kuifanya au ulikosea?

Zifuatazo ni dalili ambazo unapaswa kuziangalia ili kufahamu na kutatua fumbo hili:

1.HUNA SHAUKU YA KUPANDA DARAJA:

Kama upo katika kazi unayoipenda kupanda daraja kwako kitakuwa kipaumbele chako cha kwanza kwani ndicho kitakuwa kipimo cha utendaji wako.
Hivyo hicho ni kitu utakachokuwa unapenda kikutokee.
Kila mfanyakazi hutegemea baada ya kazi apate ujira wake na kuonyesha uwezo wake katika kazi yake.
Lakini endapo haujawahi kujisikia hali ya kuonyesha uwezo wako ili kupata daraja jipya basi ujue hiyo si hali ya kawaida kuiacha kama ilivyo.

2.UNAJIONA UKO PEKE YAKO:

Kuwa mfanyakazi si kwenda eneo la kazi, 
kukaa katika meza yako, 
kufanya kazi yako na kurudi nyumbani.
Ni kushirikiana na kila mtu aliye eneo lako la kazi, kuchangamana nao, kujadiliana masuala ya kazi, na kutumiana katika kujipima uwezo wa kila mmoja wenu.
ikikosekana hali hii eneo la kazi hupoteza ladha ya kukalika.
Ikiwa umewahi kufanya juhudi za kuanza kuchangamana na kushirikiana na wenzako lakini imeshindikana mpaka leo.
Unapaswa ujiulize ni kwanini hali hiyo inatokea.
Inawezekana wenzako wanapishana kabisa na wewe kuanzia malengo mpaka sifa.

3.KILA WAKATI HUISHI KULALAMIKA

Hakuna kazi inayohakikisha kumfurahisha kila anayeifanya kila wakati. 
Na lazima katika mabaya yote unakutana nayo lazima kuna machache mazuri yatakuwepo.
Lakini ukijikuta kila kitu unakilalamikia hakuna zuri unaloliona si kitu cha kukiachia hata kidogo,
lazima kutakuwa na tatizo kwako.
Kaa chini uitafakari kazi yako kisha jaribu kuangalia yapi unayaona zaidi mabaya au mazuri,
na endapo mabaya yakiwa mengi basi hiyo ni dalili tosha kwamba unapaswa utafute ustaarabu mwengine.

4.KIPAUMBELE CHAKO NI PESA TU:

Kama ulikuwa hujui pesa inaweza kukuridhisha kwa miezi kadhaa lakini ikishaisha kuridhika kutaegemea zaidi uhusiano wako na kazi unayofanya.
Pesa ni muhimu hilo kila mtu analitambua,
lakini hakutakuwa na thamani hata kidogo kufanya kazi usiyoipenda eti kwa kufuata pesa.

5.HAKUNA JIPYA UNALOJIFUNZA:

Katika kila kazi anayofanya mtu lazima kuna vitu vipya utakuwa unajifunza, 
na endapo unataka kuongeza uwezo wako wa kufanya kazi ili kupata uzoefu zaidi hiki pia kitakuwa kipaumbele chako.
Soko la ajira linakuwa siku hadi siku na hivyo hitaji la watu wenye uzoefu wa mambo mengi watakuwa hitaji namba moja.
Kama hauna tabia ya kujifunza vitu vipya katika kazi yako basi upo katika hatari kubwa sana ya kupitwa na wakati.
Haina maana kujisifu umekaa miaka mingi katika kazi yako lakini huna jipya ulilojifunza.

6.HUJIONI KUKUA KATIKA KAZI YAKO:

Katika maisha kukua ni sifa mojawapo katika jambo lolote unalojihusisha nalo.
Hautaweza kuipenda kazi ambayo huoni dalili yoyote ya wewe kukua katika siku zijazo.
Kama kilele unachotaka kufikia hakiko 
wazi kwako,
sioni ni jinsi gani utaweka juhudi kukifikia.
Kitu hiki hakitaishia kukunyima raha tu, bali kitachukua pia uwezo wako wa kujiamini.
Utaanza kuvurugikiwa na hasa hali itakuwa mbaya pale utakapo kuwa unakutana na watu ambao wamefanikiwa katika kazi zao.

7.HAUIONEI FAHARI KAZI YAKO:

Hata kwa kiasi gani ujitahidi kujiambia mwenyewe kuwa kazi unayofanya ni nzuri lakini hauna uthubutu wa kuitaja mbele ya wenzako.
Hivi itawezekana vipi mtu uone aibu kuielezea kazi yako mbele ya wenzako halafu uwe unaipenda?

8.UNAJIHUSISHA NA VITU VYA OVYO UKIWA KAZINI:

Kama unafanya kazi unayoipenda utakuwa unakwepa sana kukutana na mambo ya ovyo.
Muda mwingi utakuwa unawekeza nguvu yako katika kazi unayofanya na si kujihusisha na vitu visivyohusiana na kazi yako.
Endapo unapenda zaidi kukatisha kazi unayofanya ili kushabikia kitu cha ovyo kabisa hiyo ni dalili tosha hiyo kazi ujiulize tena.

9.HAUTUMII UWEZO WAKO:

Kazi nzuri ni ile inayokupa nafasi ya kujitumia uwezo wako kwa kiasi kikubwa.
Kama kazi unayojihusisha nayo haikupi nafasi ya kuonyesha uwezo wako wote basi anza kujitafakari kama ulipo ulipaswa uwepo hapo.
Afadhali ujue wazi kabisa kuwa kazi unayofanya umeizidi sifa kuliko iwe ya kawaida lakini uwezo wako ushindwe kuonekana.
Kazi inapofikia hatua hiyo maana yake nafasi ya wewe kukua kiujuzi itakuwa ndogo.

RAHA YA MAISHA NI KUFURAHIA KITU UNACHOFANYA, 
IWE INAKUINGIZIA KIDOGO AU KIKUBWA FURAHA NDIO HUWA KIPAUMBELE.

KUFANIKIWA NI ZAIDI YA KUWA KIPATO KIKUBWA 
NA MALI.
ANZA LEO KUTAMBUA KAZI UNAYOIPENDA NA UANZE KUISHI MAISHA YA MAFANIKIO KWA KUUTUMIA UWEZO WAKO KAMILI.

Maisha yanabadilika; daima yanasonga. 
Wewe kubakia hapo ulipo ni chaguo lako mwenyewe.
Na kuna msemo usemao; "Hatima yako inaamuliwa na chaguo lako na si nafasi inayotokea".
Njia ya kufikia mafanikio inaweza kuwa ndefu lakini siku zote huwa pana.
Kama haupendezewi na jinsi maisha yako ya sasa yalivyo, 
una chaguo la kubadilisha hali hiyo na mambo yakawa mazuri.
Si lazima ufanye mabadiliko makubwa kwa wakati mmoja bali unaweza ukaanza kwa hatua moja na yenyewe ikazaa nyingine.

Lakini wengi wetu huwa tunakwama wakati wa kufanya maamuzi ya kujikwamua katika hali mbaya ambayo hatuitaki.
Na mambo yafuatayo yanaweza kuwa miongoni mwa sababu zinazotushikilia tusiweze kufikia malengo:

1.KUKWEPA MAJUKUMU

Endapo wewe ni mtu ambaye mambo yanapoenda vibaya unatafuta mtu wa kumlaumu basi ujue unajifunga pingu usiende mbele.
Na hili ndio eneo ambalo kama hautalirekebisha kusonga mbele kwako 
itakuwa ngumu.
Kwani uamuzi unaufanya wewe lakini jambo likienda vibaya unatafuta kosa kwa wengine.
Unatakiwa uwe mtu wa kuikubali hali iliyotokea, 
jifunze kupitia hiyo na usonge mbele kwa kuboresha utendaji.

2.HOFU IMEKUSHINDA

Kama unafanya mambo makubwa na kila siku unapigania kutimiza ndoto zako lazima utakutana na hofu kubwa zitakazokufanya muda mwingine usijiamini.
Lakini hupaswi kuiruhusu hofu ikushinde kwani utakata tamaa mapema sana na mambo hayatoenda,
bali songa mbele kwa kile unachokiamini na hofu ipotezee kwa kuwa jasiri.

3.KUTOUTUMIA UWEZO WAKO

Wewe ndani yako uwe ushajua au bado kuna kitu ambacho ndicho umepewa uwezo wa juu zaidi kukifanya kwa ufanisi.
Lakini ukiwa unafanya jambo fulani ili uwaridhishe watu fulani tu utakuwa unajiingiza shimoni,
kwani mwisho wa siku utakuwa unajishughulisha na vitu ambavyo havitakufanya utumie uwezo wako kamili.
Anza kushughulikia namna ya kutumia uwezo wako halisi kwa kufanya unachokipenda.

4.KUSHIKILIA MAWAZO MABAYA 

Kama ndani yako umejijengea tabia ya kukosoa na kutotaka kuangalia upande mzuri wa kitu basi unaangamiza hatua zako.
Usiishi kwa kuweka ndani yako maneno ya watu waliyoongea vibaya kukuhusu na ukayatumia kama ndio mwongozo wako.
Mawazo hasi ni kama magugu usipoyang'oa mizizi itaendelea kuchipua ndani yako na kukurudisha nyuma kila siku.

5.KUTOTHAMINI ULICHONACHO

Kama unashindwa kushukuru kile ulichonacho sasa basi huna haja ya kupata la ziada.
Kutothamini ulichonacho sasa kutakufanya usione uzuri wa maisha uliyonayo sasa na kujiangalia katika upande ule ambao umepungukiwa tu.
Inawezekana huna kila kitu ulichohitaji kuwa nacho kwa sasa lakini una kila kitu kitakachokuwezesha kusonga mbele.
Maisha yetu hayana ukamilifu lakini yana uzuri wake.

6.UNAITAFUTA FURAHA KUTOKA NJE

Utaalamu sio mkusanyiko wa maarifa; bali ni kujitambua kamili wewe ushakuwa nani.
Utajiri wa kweli hauhusiani na mali unazomiliki;
bali ni kusalimu amri kwa mahitaji yasiyo na mwisho.
Unachotafuta hakipo mahali kwingine 
wala muda mwingine,
unachotafuta kipo hapa, na si kwingine 
bali ndani yako.
Jinsi unavyozidi kuitafuta nje ndivyo inazidi kujificha ndani zaidi.

7.UNATAFUTA URAHISI

Kuna siku utakuja kukaa chini na kutafakari ndipo utagundua kuwa kila chenye thamani ulichonacho sasa kulikuwa na changamoto kukipata.
Na hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa, 
kwasababu changamoto kubwa zinamuandaa mtu wa kawaida na mafanikio makubwa asiyategemea akipambana mpaka mwisho.
Mapambano siku zote yana sababu yake kutokea;
inawezekana kwa ajili ya kukupa uzoefu au kukufundisha.
Njia ya mafanikio haiwi na urahisi hata kidogo.

DUNIA INATOA NAFASI KWA KILA MTU KUONYESHA UWEZO WAKE NA AKAFIKIA MAFANIKIO ANAYOYAHITAJI.

JINSI TUNAVYOIONA INAZUNGUKA NDIVYO TUNAHITAJIKA KWENDA NAYO SAMBAMBA NA SI KUBAKI NYUMA YENYEWE IKISONGA MBELE.

ANZA LEO KUEPUKA MAMBO YALIYOTAJWA KATIKA HATUA HIZO JUU KUANZA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.

Ndoa inasemekana ni baraka pale wachumba  wanapokuwa wamependana kwa dhati,
 na kwa hiari yao wanaona ni muda muafaka kuwa kitu kimoja kama mke na mume.
Lakini kwa upande mwingine ndoa inakuwa ni balaa na kupoteza maana pale wachumba wanapoamua kuingia katika ndoa bila sababu za msingi wala vigezo vya maana kati yao.
Yaani kila mmoja anaingia na sababu na mkakati wake tofauti na alionao mwenzake.

Hebu tupeane sababu mbovu kabisa ambazo kama utazitumia kama kigezo cha kufunga ndoa na mtu basi andika umeumia:

1.UMRI WANGU UNAZIDI KUWA MKUBWA:

Hasa wanawake eneo hili ndio linawagusa sana kwani mara nyingi wanajitahidi kukimbizana na muda,
na wanaweka mkakati kabisa kwamba nikifikisha umri fulani lazima niwe ndani ya ndoa.
Ya inawezekana unatumia kigezo cha kuwahi kabla hujapoteza muonekano lakini nakuambia wazi kabisa kama unaingia katika ndoa kwasababu hii, andika maumivu siku zijazo.
Si kwamba usipoolewa basi wewe si mwanamke na kwamba ni mbaya, hapana
ndoa ni taasisi ambayo si kila mtu amepewa uwezo wa kuwa mwanachama kwahiyo ikija nafasi ya wewe kuwa mwanachama ingia bila matatizo lakini si kujidai unakimbizana na muda.


2.MALI AU UTAJIRI WA MWANAUME/MWANAMKE:

Kipindi cha nyuma jamii ilishazoea kwamba mwanamke kuolewa na mtu hata asiyempenda kwa kigezo cha mali za huyo jamaa ni kitu cha kawaida,
lakini bwana siku hizi hadi wanaume nao kigezo hiki wanakitumia ili kutoka kimaisha.
Na ombea huyo unayemdanganya asijue kabla hujafaidika kwani akijua atakuwahi na utakuwa umekosa ulichotaka.
Na wengi wao wanakumbana na mateso makubwa sana wanapoingia katika ndoa na mtu kwasababu ya mali za huyo mwenzake.

3.NILINGANE NA RAFIKI ZANGU:

Sababu hii huwa ni asili kwani mara nyingi binadamu tumekuwa na hulka ya kujilinganisha na wenzetu.
Sasa unapotaka kuingia katika ndoa kwa haraka kwa kuwa tu rafiki yako ameolewa juzi unajitia matatizoni mwenyewe.
Wengi sana wanapata mshawasha pale wanapohudhuria sherehe za harusi za ndugu na marafiki na shamra shamra za ukumbini kwa usiku huo zinawadanganya na kudhani hiyo ndio ndoa na huku kichwani akijenga wazo la yeye pia kutafuta mtu kwa haraka ili afanye kama mwenzake.

4.NJIA YA KUIMARISHA UHUSIANO:

Hapa wengi wanatumia sababu hii kulazimisha ndoa pale wanapoona mahusiano yao katika kipindi hicho sio mazuri sana kwahiyo wanaona njia pekee ni kuingia katika ndoa haraka ili kubadilisha mazingira pengine mambo yatanyooka na kumtuliza mwenzake.
Kama utatumia sababu hii kujifunga kitanzi basi umeingia chaka kwani sio sababu ya msingi kukufanya ulazimishe ndoa.
Kama katika kipindi hiki cha uchumba mnatofautiana si kwamba ndoa ndio itawafanya muwe na mtazamo mmoja kihisia na maamuzi.

5.NATAKA TUWE KARIBU ZAIDI:

Wachumba ambao wanaishi mbali mbali wanadhani kuingia katika ndoa haraka ni njia ya kumaliza umbali baina yao.
Na maamuzi haya mtu anaweza kuyafanya hata kwa kuhama mji na kuhamia alipo mwenzake na kuanza kulazimisha ndoa hata kama mwenzake hajaonyesha utayari.
"Oh! nimechoka kuwasiliana naye kwenye simu kila siku bora nimfuate huko huko aliko na nimlazimishe anioe"
Kweli yawezekana unaumia lakini lazima uzingatie umbali wenu unaletwa na nini,
 na ukishagundua shirikiana na huyo mwenzako namna ya kutatua ndio utajua kama na yeye yuko tayari na huo mpango wako au la
na sio kumvamia alipo na kulazimisha mambo.

6.NIONDOKE KATIKA NYUMBA YA FAMILIA:

Sababu nyingine mbovu ni hii hapa na jua wazi si sababu nzuri kuitumia ili kuingia katika maisha ya ndoa.
Kuwa na subira ni kitu kizuri, 
kama uliweza kulelewa hapo nyumbani kwenu kwa miaka mingi ndoa isiwe kigezo cha kukuondoa.
Kweli kiumri umekua na unatamani uwe kwako ambako utakuwa una maamuzi ya leo unafanya nini au unapika nini.
Na hapa inatokea mara nyingi pale msichana anapotembelea sehemu anayoishi mvulana na kukuta jamaa kiasi fulani kajipanga na anatamani ahamie hapo haraka kwa kumlazimisha ndoa,
 kwani anaona kashapata njia ya mkato. 

7.KISASI KWA ULIYEACHANA NAYE:

Hapa napo wananasa wengi sana, 
yaani utakuta mtu anaachana na mchumba mwezi mmoja nyuma na kwakuwa alimpenda na anataka kumlipizia kisasi basi analazimisha kuingia katika ndoa na mtu mwengine ambaye hajakaa naye hata mwaka kumfahamu.
Hii ni moja ya sababu ya kijinga zaidi kutumia ili kufunga ndoa kwa haraka,
kwani hautakuwa unamkomoa huyo unayetaka umkomoe bali utakuwa unajiingiza katika matatizo wewe mwenyewe.

NDOA NI KITU KIZURI KATIKA MAISHA PALE INAPOKUWA IMEUNGANISHWA NA UPENDO WA DHATI,
UVUMILIVU NA MALENGO SAWA BAINA YA WANANDOA.

JINSIA, HESHIMA AU UTU WAKO HAUTATAMBULISHWA NA NDOA YA KULAZIMISHA ISIYO NA MALENGO SAHIHI.
KUWA MVUMILIVU NA UVUTE SUBIRA,
KAMA UNASTAHILI KUINGIA KATIKA NDOA UTAINGIA TU LAKINI USILAZIMISHE.

Watu wenye aibu ndani yao wanafahamu fika kuwa kuna mambo mazuri yanawapita lakini wanahisi hawana jinsi ya kubadilisha hali hiyo.
Aibu kimahesabu ni sawa na:
AIBU = KUKOSA FURSA + KUKOSA FURAHA + KUFAHAMIANA NA WATU WACHACHE

Aibu ni kizuizi kikubwa sana kwa mwenye nayo kufikia mambo mazuri katika jamii.
Lakini naomba nikuambie hata kama wewe ni mmoja wao kuanzia leo 
unaweza kubadilisha hali hiyo kwa kutumia hatua zifuatazo:

1.MTAZAMO WAKO JUU YA WATU WENGINE

Watu wenye aibu mara nyingi wanajaribu kujitofautisha na 
watu wapya wanaokutana nao na kuwapa hadhi inayowazidi wao.
Hali hiyo itakufanya ujione huna jipya la kumueleza au kuzungumza mbele ya watu hao.
Unachopaswa kufanya ni 
kumuona kila mtu mpya unayekutana naye kama wa kawaida na hana alichokuzidi na kwamba hata yeye kuna vitu hajui 
au hana ambavyo wewe unavyo.

2.TAMBUA HATA WENGINE WANA AIBU PIA

Usijiweke peke yako kama ndio mtu mwenye aibu kupita wote na kwamba wengine 
hawako kama wewe.
Kuanzia leo tambua kuwa kila mtu ameumbwa na aibu ndani yake pale anapokutana na mtu mpya kwahiyo ukiwa 
mbele ya watu wapya 
jua hata wao pia wanakuonea aibu kwa kuwa hawajui ulichonacho ni nini.

3.KUSANYA TAARIFA NYINGI KICHWANI

Mtu mwenye aibu siku zote hujiona hana chochote cha maana 
kuwashirikisha wengine.
Kuna wengine wanakuwa kweli hawana vitu vya kuzungumza mbele za watu wengine na kuna wengine ni 
kujidharau tu na kuona taarifa walizo nazo hazina maana.
Jaribu kuwa na tabia ya kusoma vitu vipya na kuwaeleza watu wengine 
na hapo utafanya uwezo wako wa kusimama au kujitokeza mbele ya watu wengine kuwa mkubwa kwa kuwa kichwani 
una kitu cha kuwashirikisha.

4.ONGEZA KUJIKUBALI

Ukiwa na tabia ya kujidharau mwenyewe na kujiona huna thamani 
mbele ya wengine utafanya aibu ikuteke 
daima.
Thamini uwezo wa pekee 
ulionao na upe thamani kuwa hakuna mwengine alionao kwahiyo hata wewe 
unaweza kuwaonyesha maajabu wasiyoyajua.
Ukijiweka katika kundi 
hili hautakuwa muoga wa kuwasiliana 
na watu wapya kila siku.

5.ACHA KUZIAMINI HISIA HASI

Mtu mwenye hofu siku zote anatengeneza hisia ndani yake kuwa baada
 ya yeye kufanya au kusema jambo fulani
 basi watu wengine watafanya
 kitu fulani kwake.
Mathalani anaweza akaanza kuhisi kuwa baada ya yeye kukosea kitu 
watu watamcheka au kumsema vibaya
 kwa wengine.
Na anapoiamini hiyo picha kichwani kwake anaongeza aibu na kushindwa kuitumia fursa iliyopo mbele yake.
Na mara nyingi hizi hisia huwa hazina ukweli wowote katika matukio
 halisi ila ni hofu tu anayojijengea mwenyewe.
Anza kujitengenezea hisia chanya kuwa watu watakupongeza kwa kujaribu.

KUNA MSEMO USEMAO: 
"AIBU YAKO NDIO UMASIKINI WAKO"
HAINA UBISHI UKIENDEKEZA TABIA YA KUONA AIBU MBELE ZA WATU KAMWE HAKUNA FURSA UTAKAYOPATA.

TAMBUA PIA: "MAFANIKIO YA MTU YAPO MIKONONI MWA MTU"
NI KUPITIA BINADAMU WENZETU NDIO TUNAFIKIA NDOTO NA MAFANIKIO KATIKA MAISHA YETU HIVYO USIIACHE AIBU IKUTENGE NA NDOTO YAKO.

Muziki uko kila mahali tunapoenda,
iwe umeusikia kupitia redio, 
katika mgahawa, nyumba za ibada au katika maeneo ya starehe.
Hakuna utafiti wowote uliowahi kufanywa ambao uliweza kuthibitisha madhara yanayotokana na mtu kusikiliza muziki,
ila tafiti nyingi zimeegemea katika kutoa faida za muziki katika maisha yetu ya kila siku.
Haijalishi aina gani ya muziki unaipenda sana kusikiliza ilimradi unaupenda utakusaidia kitu tu.

Hebu tuangalie faida japo chache ambazo zinaletwa na kusikiliza muziki.

1.KUTUNZA KUMBUKUMBU

Haijalishi sasa hivi una umri gani lakini kila mara kuna wimbo ukiusikia lazima utakukumbusha matukio yaliyopita ambapo wakati unapitia kipindi hicho wimbo huo ndio ulikuwa unapigwa.
Na utajikuta unaanza kufurahi na kuzidi kuziimarisha kumbukumbu zako za matukio ya zamani.
Si kitu cha ajabu kumsikia mtu akisikia wimbo fulani unaanza kusema "Aah! wimbo wangu huo!" 

2.KUIMARISHA UMAKINI

Ukiwa ni msikilizaji mzuri wa nyimbo mara nyingi unatengeneza tabia ya kusikiliza wimbo kuanzia mashairi hadi midundo yake na hii si kazi rahisi hata kidogo kwani unatakiwa umakini wa hali ya juu kufanya jambo hili.
Cha ajabu utamkuta mtu anaupenda wimbo lakini hajui hata mashairi yanazungumzia nini,
 tabia itakufanya hata uwezo wako wa kusikiliza mtu anapoongea uwe mdogo kwani kitendo cha kusikiliza na kutafsiri papo kwa papo kina umuhimu sana katika ulimwengu wa kujifunza.

3.HULETA HISIA ZA UTULIVU

Muziki sio lazima uwe na midundo,
lakini hata mashairi tupu yanaweza kukuletea utulivu unaoufanya ubongo upumzike vizuri.
Na ndio maana unapomuimbia mtoto mdogo hachelewi kulala.
Na watu wazima mara nyingi husinzia na kupumzika haraka wanaposiliza nyimbo za taratibu kwani ndizo ambazo zinaupa ubongo hisia nzuri kwa muda huo.

4.HUONGEZA NGUVU WAKATI WA SHUGHULI

Mathalani unapokuwa unafanya shughuli fulani ambayo ni kutumia nguvu nyingi muziki husaidia kuongeza utendaji kazi wako muda huo.
Na ndio maana hata washauri wa mazoezi wanapenda kuwaeleza wateja wao wanapofanya mazoezi ya kukimbia au yoyote ya kutumia viungo ni vyema wakaweka muziki ambao utakuwa unawasindikiza ili wasichoke haraka.

5.UNAONGEZA MANENO

Hata kama wewe ni mtumiaji mzuri wa lugha yako  lakini kuna maneno unaweza ukawa hujawahi hata kuyatumia katika maisha yako.
Sasa unapokuwa msikilizaji mzuri wa mashairi ya nyimboi inakusaidia kuongeza maneno na maana zake.

6.CHANGAMOTO ZA UWEZO WA KUHOJI

Muziki mara zote kama unausikiliza kwa makini unakuletea changamoto za kujiuliza kama kinachoimbwa ni sawa au sio sawa.
Na kitu pekee kitakachokupa uwezo wa kutambua hilo ni uwezo wako wa kuhoji mashairi kutokana na tafsiri yako uliyopata.
Na ndio maana sitashangaa kumkuta mtu anaimba mashairi ya lugha yake lakini hajui hata aliyeimba alikuwa ana maanisha nini.

7.KUTIA HAMASA

Mara kwa mara si kitu cha ajabu kukuta unasikiliza wimbo ambao mashairi yake yanakugusa moja kwa moja,
na bahati nzuri anatoa na suluhisho la tatizo humo humo.
Na hali hiyo itakufanya ujione hauko peke yako mwenye hisia kama hizo hivyo kukutia hamasa ya kusonga kusonga mbele.
Na ndio maana kuna nyimbo kuzisahau kwako inakuwa ni ndoto kwani katika kipindi fulani cha maisha yako ulikugusa kiukweli.

8.HUONGEZA UBUNIFU

Muziki wenyewe tu ni kazi ya ubunifu kuanzia melodi ya mashairi hadi midundo yake.
Japo si kila msikilizaji wa muziki anaweza kuja kuwa msanii lakini utafiti unaonyesha watu wengi waliokuja kuwa wasanii wa muziki walikuwa wasilikzaji wazuri wa muziki.
Hata watu wengine wanaofanya kazi nyingine za sanaa wanatumia muziki kama chombo moja wapo cha kuwaongezea ubunifu kwa mfano waandishi, wachoraji, wachezaji au wanaofanya kazi za kutumia umakini mkubwa wa ubongo.

9.HUBADILISHA HALI YA UBONGO

Muziki unaweza ukakusaidia kubadilisha hali unayojisikia iwe ya huzuni, mawazo, upweke, hofu au hata hasira.
Na ndio maana wataalamu wanashauri ikiwa uko na hali mojawapo nilizozitaja hapo juu uwe unatumia njia ya kuimba nyimbo unazozipenda kukurudisha katika hali yako ya kawaida.

10.HUONGEZA UFANISI WA KAZI

Haijalishi kazi gani unayofanya,
ukimya utakufanya akili yako ihamie kwingine ambako utaufanya ubongo upoteze umakini na shughuli unayofanya muda huo.
Ila kwa kutumia aina ya muziki unaoupenda utaifanya akili ijisikie vizuri na hata kuzuia kuchoka haraka.

NAJUA KUNA WATU SI WAPENZI WA KUSIKILIZA MUZIKI KABISA.

NA MAKALA HII HAIPO KWA AJILI YA KUKUSHAWISHI UANZE TABIA AMBAYO HUKUWAHI KUWA NAYO KABLA ILA IPO KWA AJILI YA WALE WAPENZI WA MUZIKI ILI WAUTUMIE MUZIKI HUO KATIKA KUBORESHA SHUGHULI ZAO.

 
Copyright 2013-2017 Lisha Ubongo
| Branded by www.pixelbase.co.tz