Maisha yanabadilika; daima yanasonga. 
Wewe kubakia hapo ulipo ni chaguo lako mwenyewe.
Na kuna msemo usemao; "Hatima yako inaamuliwa na chaguo lako na si nafasi inayotokea".
Njia ya kufikia mafanikio inaweza kuwa ndefu lakini siku zote huwa pana.
Kama haupendezewi na jinsi maisha yako ya sasa yalivyo, 
una chaguo la kubadilisha hali hiyo na mambo yakawa mazuri.
Si lazima ufanye mabadiliko makubwa kwa wakati mmoja bali unaweza ukaanza kwa hatua moja na yenyewe ikazaa nyingine.

Lakini wengi wetu huwa tunakwama wakati wa kufanya maamuzi ya kujikwamua katika hali mbaya ambayo hatuitaki.
Na mambo yafuatayo yanaweza kuwa miongoni mwa sababu zinazotushikilia tusiweze kufikia malengo:

1.KUKWEPA MAJUKUMU

Endapo wewe ni mtu ambaye mambo yanapoenda vibaya unatafuta mtu wa kumlaumu basi ujue unajifunga pingu usiende mbele.
Na hili ndio eneo ambalo kama hautalirekebisha kusonga mbele kwako 
itakuwa ngumu.
Kwani uamuzi unaufanya wewe lakini jambo likienda vibaya unatafuta kosa kwa wengine.
Unatakiwa uwe mtu wa kuikubali hali iliyotokea, 
jifunze kupitia hiyo na usonge mbele kwa kuboresha utendaji.

2.HOFU IMEKUSHINDA

Kama unafanya mambo makubwa na kila siku unapigania kutimiza ndoto zako lazima utakutana na hofu kubwa zitakazokufanya muda mwingine usijiamini.
Lakini hupaswi kuiruhusu hofu ikushinde kwani utakata tamaa mapema sana na mambo hayatoenda,
bali songa mbele kwa kile unachokiamini na hofu ipotezee kwa kuwa jasiri.

3.KUTOUTUMIA UWEZO WAKO

Wewe ndani yako uwe ushajua au bado kuna kitu ambacho ndicho umepewa uwezo wa juu zaidi kukifanya kwa ufanisi.
Lakini ukiwa unafanya jambo fulani ili uwaridhishe watu fulani tu utakuwa unajiingiza shimoni,
kwani mwisho wa siku utakuwa unajishughulisha na vitu ambavyo havitakufanya utumie uwezo wako kamili.
Anza kushughulikia namna ya kutumia uwezo wako halisi kwa kufanya unachokipenda.

4.KUSHIKILIA MAWAZO MABAYA 

Kama ndani yako umejijengea tabia ya kukosoa na kutotaka kuangalia upande mzuri wa kitu basi unaangamiza hatua zako.
Usiishi kwa kuweka ndani yako maneno ya watu waliyoongea vibaya kukuhusu na ukayatumia kama ndio mwongozo wako.
Mawazo hasi ni kama magugu usipoyang'oa mizizi itaendelea kuchipua ndani yako na kukurudisha nyuma kila siku.

5.KUTOTHAMINI ULICHONACHO

Kama unashindwa kushukuru kile ulichonacho sasa basi huna haja ya kupata la ziada.
Kutothamini ulichonacho sasa kutakufanya usione uzuri wa maisha uliyonayo sasa na kujiangalia katika upande ule ambao umepungukiwa tu.
Inawezekana huna kila kitu ulichohitaji kuwa nacho kwa sasa lakini una kila kitu kitakachokuwezesha kusonga mbele.
Maisha yetu hayana ukamilifu lakini yana uzuri wake.

6.UNAITAFUTA FURAHA KUTOKA NJE

Utaalamu sio mkusanyiko wa maarifa; bali ni kujitambua kamili wewe ushakuwa nani.
Utajiri wa kweli hauhusiani na mali unazomiliki;
bali ni kusalimu amri kwa mahitaji yasiyo na mwisho.
Unachotafuta hakipo mahali kwingine 
wala muda mwingine,
unachotafuta kipo hapa, na si kwingine 
bali ndani yako.
Jinsi unavyozidi kuitafuta nje ndivyo inazidi kujificha ndani zaidi.

7.UNATAFUTA URAHISI

Kuna siku utakuja kukaa chini na kutafakari ndipo utagundua kuwa kila chenye thamani ulichonacho sasa kulikuwa na changamoto kukipata.
Na hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa, 
kwasababu changamoto kubwa zinamuandaa mtu wa kawaida na mafanikio makubwa asiyategemea akipambana mpaka mwisho.
Mapambano siku zote yana sababu yake kutokea;
inawezekana kwa ajili ya kukupa uzoefu au kukufundisha.
Njia ya mafanikio haiwi na urahisi hata kidogo.

DUNIA INATOA NAFASI KWA KILA MTU KUONYESHA UWEZO WAKE NA AKAFIKIA MAFANIKIO ANAYOYAHITAJI.

JINSI TUNAVYOIONA INAZUNGUKA NDIVYO TUNAHITAJIKA KWENDA NAYO SAMBAMBA NA SI KUBAKI NYUMA YENYEWE IKISONGA MBELE.

ANZA LEO KUEPUKA MAMBO YALIYOTAJWA KATIKA HATUA HIZO JUU KUANZA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.

Share this post:

Digg it StumbleUpon del.icio.us Google Yahoo! reddit

0 comments:

Post a Comment

 
Copyright 2013-2017 Lisha Ubongo
| Branded by www.pixelbase.co.tz