HIVI, UNAZITAMBUA DALILI AMBAZO ZIKIKUTOKEA ZITAKUONYESHA KAMA KAZI ULIYOPO NI SAHIHI KWAKO AU LA? SOMA UJIELIMISHE
Jiulize,
viatu ulivyovaa ni siazi yako na kama ndio ni aina yako?
Miongoni mwetu tunatumia asilimia 75 ya muda wetu kwa siku katika kazi.
Kwahiyo kuwa katika kazi ambayo haikupi faraja inaweza ikakuletea matatizo katika maisha yako ya kila siku.
Umejaribu njia zote kujitahidi kuendana na hali lakini bado unaona wazi kabisa kwamba kuna kitu kinakosekana.
Ni ukweli usiopingika kuwa kazi yoyote ile kwa upande mwingine kuna kipindi inachosha.
Unachopaswa kujiuliza ni je,
hali hii unayojisikia ni ya muda au ni ya kudumu?
Kama ushawahi kukumbana na hali hiyo au kujiuliza hilo swali basi makala hii inakuhusu.
Sasa utajuaje kama kazi uliyopo sasa ulifanya uamuzi sahihi kuifanya au ulikosea?
Zifuatazo ni dalili ambazo unapaswa kuziangalia ili kufahamu na kutatua fumbo hili:
1.HUNA SHAUKU YA KUPANDA DARAJA:
Kama upo katika kazi unayoipenda kupanda daraja kwako kitakuwa kipaumbele chako cha kwanza kwani ndicho kitakuwa kipimo cha utendaji wako.
Hivyo hicho ni kitu utakachokuwa unapenda kikutokee.
Kila mfanyakazi hutegemea baada ya kazi apate ujira wake na kuonyesha uwezo wake katika kazi yake.
Lakini endapo haujawahi kujisikia hali ya kuonyesha uwezo wako ili kupata daraja jipya basi ujue hiyo si hali ya kawaida kuiacha kama ilivyo.
2.UNAJIONA UKO PEKE YAKO:
Kuwa mfanyakazi si kwenda eneo la kazi,
kukaa katika meza yako,
kufanya kazi yako na kurudi nyumbani.
Ni kushirikiana na kila mtu aliye eneo lako la kazi, kuchangamana nao, kujadiliana masuala ya kazi, na kutumiana katika kujipima uwezo wa kila mmoja wenu.
ikikosekana hali hii eneo la kazi hupoteza ladha ya kukalika.
Ikiwa umewahi kufanya juhudi za kuanza kuchangamana na kushirikiana na wenzako lakini imeshindikana mpaka leo.
Unapaswa ujiulize ni kwanini hali hiyo inatokea.
Inawezekana wenzako wanapishana kabisa na wewe kuanzia malengo mpaka sifa.
3.KILA WAKATI HUISHI KULALAMIKA
Hakuna kazi inayohakikisha kumfurahisha kila anayeifanya kila wakati.
Na lazima katika mabaya yote unakutana nayo lazima kuna machache mazuri yatakuwepo.
Lakini ukijikuta kila kitu unakilalamikia hakuna zuri unaloliona si kitu cha kukiachia hata kidogo,
lazima kutakuwa na tatizo kwako.
Kaa chini uitafakari kazi yako kisha jaribu kuangalia yapi unayaona zaidi mabaya au mazuri,
na endapo mabaya yakiwa mengi basi hiyo ni dalili tosha kwamba unapaswa utafute ustaarabu mwengine.
4.KIPAUMBELE CHAKO NI PESA TU:
Kama ulikuwa hujui pesa inaweza kukuridhisha kwa miezi kadhaa lakini ikishaisha kuridhika kutaegemea zaidi uhusiano wako na kazi unayofanya.
Pesa ni muhimu hilo kila mtu analitambua,
lakini hakutakuwa na thamani hata kidogo kufanya kazi usiyoipenda eti kwa kufuata pesa.
5.HAKUNA JIPYA UNALOJIFUNZA:
Katika kila kazi anayofanya mtu lazima kuna vitu vipya utakuwa unajifunza,
na endapo unataka kuongeza uwezo wako wa kufanya kazi ili kupata uzoefu zaidi hiki pia kitakuwa kipaumbele chako.
Soko la ajira linakuwa siku hadi siku na hivyo hitaji la watu wenye uzoefu wa mambo mengi watakuwa hitaji namba moja.
Kama hauna tabia ya kujifunza vitu vipya katika kazi yako basi upo katika hatari kubwa sana ya kupitwa na wakati.
Haina maana kujisifu umekaa miaka mingi katika kazi yako lakini huna jipya ulilojifunza.
6.HUJIONI KUKUA KATIKA KAZI YAKO:
Katika maisha kukua ni sifa mojawapo katika jambo lolote unalojihusisha nalo.
Hautaweza kuipenda kazi ambayo huoni dalili yoyote ya wewe kukua katika siku zijazo.
Kama kilele unachotaka kufikia hakiko
wazi kwako,
sioni ni jinsi gani utaweka juhudi kukifikia.
Kitu hiki hakitaishia kukunyima raha tu, bali kitachukua pia uwezo wako wa kujiamini.
Utaanza kuvurugikiwa na hasa hali itakuwa mbaya pale utakapo kuwa unakutana na watu ambao wamefanikiwa katika kazi zao.
7.HAUIONEI FAHARI KAZI YAKO:
Hata kwa kiasi gani ujitahidi kujiambia mwenyewe kuwa kazi unayofanya ni nzuri lakini hauna uthubutu wa kuitaja mbele ya wenzako.
Hivi itawezekana vipi mtu uone aibu kuielezea kazi yako mbele ya wenzako halafu uwe unaipenda?
8.UNAJIHUSISHA NA VITU VYA OVYO UKIWA KAZINI:
Kama unafanya kazi unayoipenda utakuwa unakwepa sana kukutana na mambo ya ovyo.
Muda mwingi utakuwa unawekeza nguvu yako katika kazi unayofanya na si kujihusisha na vitu visivyohusiana na kazi yako.
Endapo unapenda zaidi kukatisha kazi unayofanya ili kushabikia kitu cha ovyo kabisa hiyo ni dalili tosha hiyo kazi ujiulize tena.
9.HAUTUMII UWEZO WAKO:
Kazi nzuri ni ile inayokupa nafasi ya kujitumia uwezo wako kwa kiasi kikubwa.
Kama kazi unayojihusisha nayo haikupi nafasi ya kuonyesha uwezo wako wote basi anza kujitafakari kama ulipo ulipaswa uwepo hapo.
Afadhali ujue wazi kabisa kuwa kazi unayofanya umeizidi sifa kuliko iwe ya kawaida lakini uwezo wako ushindwe kuonekana.
Kazi inapofikia hatua hiyo maana yake nafasi ya wewe kukua kiujuzi itakuwa ndogo.
RAHA YA MAISHA NI KUFURAHIA KITU UNACHOFANYA,
IWE INAKUINGIZIA KIDOGO AU KIKUBWA FURAHA NDIO HUWA KIPAUMBELE.
KUFANIKIWA NI ZAIDI YA KUWA KIPATO KIKUBWA
NA MALI.
ANZA LEO KUTAMBUA KAZI UNAYOIPENDA NA UANZE KUISHI MAISHA YA MAFANIKIO KWA KUUTUMIA UWEZO WAKO KAMILI.
JE, WEWE NI MMOJA WA WATU WANAOTAKA KUSONGA MBELE KATIKA NJIA YA MAFANIKIO LAKINI MATUMAINI YANAPOTEA? SOMA UJIELIMISHE MAMBO YANAYOKUZUIA UYAFANYIE KAZI
Maisha yanabadilika; daima yanasonga.
Wewe kubakia hapo ulipo ni chaguo lako mwenyewe.
Na kuna msemo usemao; "Hatima yako inaamuliwa na chaguo lako na si nafasi inayotokea".
Njia ya kufikia mafanikio inaweza kuwa ndefu lakini siku zote huwa pana.
Kama haupendezewi na jinsi maisha yako ya sasa yalivyo,
una chaguo la kubadilisha hali hiyo na mambo yakawa mazuri.
Si lazima ufanye mabadiliko makubwa kwa wakati mmoja bali unaweza ukaanza kwa hatua moja na yenyewe ikazaa nyingine.
Lakini wengi wetu huwa tunakwama wakati wa kufanya maamuzi ya kujikwamua katika hali mbaya ambayo hatuitaki.
Na mambo yafuatayo yanaweza kuwa miongoni mwa sababu zinazotushikilia tusiweze kufikia malengo:
1.KUKWEPA MAJUKUMU
Endapo wewe ni mtu ambaye mambo yanapoenda vibaya unatafuta mtu wa kumlaumu basi ujue unajifunga pingu usiende mbele.
Na hili ndio eneo ambalo kama hautalirekebisha kusonga mbele kwako
itakuwa ngumu.
Kwani uamuzi unaufanya wewe lakini jambo likienda vibaya unatafuta kosa kwa wengine.
Unatakiwa uwe mtu wa kuikubali hali iliyotokea,
jifunze kupitia hiyo na usonge mbele kwa kuboresha utendaji.
2.HOFU IMEKUSHINDA
Kama unafanya mambo makubwa na kila siku unapigania kutimiza ndoto zako lazima utakutana na hofu kubwa zitakazokufanya muda mwingine usijiamini.
Lakini hupaswi kuiruhusu hofu ikushinde kwani utakata tamaa mapema sana na mambo hayatoenda,
bali songa mbele kwa kile unachokiamini na hofu ipotezee kwa kuwa jasiri.
3.KUTOUTUMIA UWEZO WAKO
Wewe ndani yako uwe ushajua au bado kuna kitu ambacho ndicho umepewa uwezo wa juu zaidi kukifanya kwa ufanisi.
Lakini ukiwa unafanya jambo fulani ili uwaridhishe watu fulani tu utakuwa unajiingiza shimoni,
kwani mwisho wa siku utakuwa unajishughulisha na vitu ambavyo havitakufanya utumie uwezo wako kamili.
Anza kushughulikia namna ya kutumia uwezo wako halisi kwa kufanya unachokipenda.
4.KUSHIKILIA MAWAZO MABAYA
Kama ndani yako umejijengea tabia ya kukosoa na kutotaka kuangalia upande mzuri wa kitu basi unaangamiza hatua zako.
Usiishi kwa kuweka ndani yako maneno ya watu waliyoongea vibaya kukuhusu na ukayatumia kama ndio mwongozo wako.
Mawazo hasi ni kama magugu usipoyang'oa mizizi itaendelea kuchipua ndani yako na kukurudisha nyuma kila siku.
5.KUTOTHAMINI ULICHONACHO
Kama unashindwa kushukuru kile ulichonacho sasa basi huna haja ya kupata la ziada.
Kutothamini ulichonacho sasa kutakufanya usione uzuri wa maisha uliyonayo sasa na kujiangalia katika upande ule ambao umepungukiwa tu.
Inawezekana huna kila kitu ulichohitaji kuwa nacho kwa sasa lakini una kila kitu kitakachokuwezesha kusonga mbele.
Maisha yetu hayana ukamilifu lakini yana uzuri wake.
6.UNAITAFUTA FURAHA KUTOKA NJE
Utaalamu sio mkusanyiko wa maarifa; bali ni kujitambua kamili wewe ushakuwa nani.
Utajiri wa kweli hauhusiani na mali unazomiliki;
bali ni kusalimu amri kwa mahitaji yasiyo na mwisho.
Unachotafuta hakipo mahali kwingine
wala muda mwingine,
unachotafuta kipo hapa, na si kwingine
bali ndani yako.
Jinsi unavyozidi kuitafuta nje ndivyo inazidi kujificha ndani zaidi.
7.UNATAFUTA URAHISI
Kuna siku utakuja kukaa chini na kutafakari ndipo utagundua kuwa kila chenye thamani ulichonacho sasa kulikuwa na changamoto kukipata.
Na hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa,
kwasababu changamoto kubwa zinamuandaa mtu wa kawaida na mafanikio makubwa asiyategemea akipambana mpaka mwisho.
Mapambano siku zote yana sababu yake kutokea;
inawezekana kwa ajili ya kukupa uzoefu au kukufundisha.
Njia ya mafanikio haiwi na urahisi hata kidogo.
DUNIA INATOA NAFASI KWA KILA MTU KUONYESHA UWEZO WAKE NA AKAFIKIA MAFANIKIO ANAYOYAHITAJI.
JINSI TUNAVYOIONA INAZUNGUKA NDIVYO TUNAHITAJIKA KWENDA NAYO SAMBAMBA NA SI KUBAKI NYUMA YENYEWE IKISONGA MBELE.
ANZA LEO KUEPUKA MAMBO YALIYOTAJWA KATIKA HATUA HIZO JUU KUANZA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.
HIVI, UNAZIFAHAMU SABABU MBOVU KABISA AMBAZO HUPASWI KUZITUMIA ILI KUFUNGA NDOA NA MTU? SOMA UJIELIMISHE
Ndoa inasemekana ni baraka pale wachumba wanapokuwa wamependana kwa dhati,
na kwa hiari yao wanaona ni muda muafaka kuwa kitu kimoja kama mke na mume.
Lakini kwa upande mwingine ndoa inakuwa ni balaa na kupoteza maana pale wachumba wanapoamua kuingia katika ndoa bila sababu za msingi wala vigezo vya maana kati yao.
Yaani kila mmoja anaingia na sababu na mkakati wake tofauti na alionao mwenzake.
Hebu tupeane sababu mbovu kabisa ambazo kama utazitumia kama kigezo cha kufunga ndoa na mtu basi andika umeumia:
1.UMRI WANGU UNAZIDI KUWA MKUBWA:
Hasa wanawake eneo hili ndio linawagusa sana kwani mara nyingi wanajitahidi kukimbizana na muda,
na wanaweka mkakati kabisa kwamba nikifikisha umri fulani lazima niwe ndani ya ndoa.
Ya inawezekana unatumia kigezo cha kuwahi kabla hujapoteza muonekano lakini nakuambia wazi kabisa kama unaingia katika ndoa kwasababu hii, andika maumivu siku zijazo.
Si kwamba usipoolewa basi wewe si mwanamke na kwamba ni mbaya, hapana
ndoa ni taasisi ambayo si kila mtu amepewa uwezo wa kuwa mwanachama kwahiyo ikija nafasi ya wewe kuwa mwanachama ingia bila matatizo lakini si kujidai unakimbizana na muda.
2.MALI AU UTAJIRI WA MWANAUME/MWANAMKE:
Kipindi cha nyuma jamii ilishazoea kwamba mwanamke kuolewa na mtu hata asiyempenda kwa kigezo cha mali za huyo jamaa ni kitu cha kawaida,
lakini bwana siku hizi hadi wanaume nao kigezo hiki wanakitumia ili kutoka kimaisha.
Na ombea huyo unayemdanganya asijue kabla hujafaidika kwani akijua atakuwahi na utakuwa umekosa ulichotaka.
Na wengi wao wanakumbana na mateso makubwa sana wanapoingia katika ndoa na mtu kwasababu ya mali za huyo mwenzake.
3.NILINGANE NA RAFIKI ZANGU:
Sababu hii huwa ni asili kwani mara nyingi binadamu tumekuwa na hulka ya kujilinganisha na wenzetu.
Sasa unapotaka kuingia katika ndoa kwa haraka kwa kuwa tu rafiki yako ameolewa juzi unajitia matatizoni mwenyewe.
Wengi sana wanapata mshawasha pale wanapohudhuria sherehe za harusi za ndugu na marafiki na shamra shamra za ukumbini kwa usiku huo zinawadanganya na kudhani hiyo ndio ndoa na huku kichwani akijenga wazo la yeye pia kutafuta mtu kwa haraka ili afanye kama mwenzake.
4.NJIA YA KUIMARISHA UHUSIANO:
Hapa wengi wanatumia sababu hii kulazimisha ndoa pale wanapoona mahusiano yao katika kipindi hicho sio mazuri sana kwahiyo wanaona njia pekee ni kuingia katika ndoa haraka ili kubadilisha mazingira pengine mambo yatanyooka na kumtuliza mwenzake.
Kama utatumia sababu hii kujifunga kitanzi basi umeingia chaka kwani sio sababu ya msingi kukufanya ulazimishe ndoa.
Kama katika kipindi hiki cha uchumba mnatofautiana si kwamba ndoa ndio itawafanya muwe na mtazamo mmoja kihisia na maamuzi.
5.NATAKA TUWE KARIBU ZAIDI:
Wachumba ambao wanaishi mbali mbali wanadhani kuingia katika ndoa haraka ni njia ya kumaliza umbali baina yao.
Na maamuzi haya mtu anaweza kuyafanya hata kwa kuhama mji na kuhamia alipo mwenzake na kuanza kulazimisha ndoa hata kama mwenzake hajaonyesha utayari.
"Oh! nimechoka kuwasiliana naye kwenye simu kila siku bora nimfuate huko huko aliko na nimlazimishe anioe"
Kweli yawezekana unaumia lakini lazima uzingatie umbali wenu unaletwa na nini,
na ukishagundua shirikiana na huyo mwenzako namna ya kutatua ndio utajua kama na yeye yuko tayari na huo mpango wako au la
na sio kumvamia alipo na kulazimisha mambo.
6.NIONDOKE KATIKA NYUMBA YA FAMILIA:
Sababu nyingine mbovu ni hii hapa na jua wazi si sababu nzuri kuitumia ili kuingia katika maisha ya ndoa.
Kuwa na subira ni kitu kizuri,
kama uliweza kulelewa hapo nyumbani kwenu kwa miaka mingi ndoa isiwe kigezo cha kukuondoa.
Kweli kiumri umekua na unatamani uwe kwako ambako utakuwa una maamuzi ya leo unafanya nini au unapika nini.
Na hapa inatokea mara nyingi pale msichana anapotembelea sehemu anayoishi mvulana na kukuta jamaa kiasi fulani kajipanga na anatamani ahamie hapo haraka kwa kumlazimisha ndoa,
kwani anaona kashapata njia ya mkato.
7.KISASI KWA ULIYEACHANA NAYE:
Hapa napo wananasa wengi sana,
yaani utakuta mtu anaachana na mchumba mwezi mmoja nyuma na kwakuwa alimpenda na anataka kumlipizia kisasi basi analazimisha kuingia katika ndoa na mtu mwengine ambaye hajakaa naye hata mwaka kumfahamu.
Hii ni moja ya sababu ya kijinga zaidi kutumia ili kufunga ndoa kwa haraka,
kwani hautakuwa unamkomoa huyo unayetaka umkomoe bali utakuwa unajiingiza katika matatizo wewe mwenyewe.
NDOA NI KITU KIZURI KATIKA MAISHA PALE INAPOKUWA IMEUNGANISHWA NA UPENDO WA DHATI,
UVUMILIVU NA MALENGO SAWA BAINA YA WANANDOA.
JINSIA, HESHIMA AU UTU WAKO HAUTATAMBULISHWA NA NDOA YA KULAZIMISHA ISIYO NA MALENGO SAHIHI.
KUWA MVUMILIVU NA UVUTE SUBIRA,
KAMA UNASTAHILI KUINGIA KATIKA NDOA UTAINGIA TU LAKINI USILAZIMISHE.
Subscribe to:
Posts (Atom)